2015-07-25 10:48:00

Rais Kikwete atunukiwa tuzo ya utawala bora Afrika!


Jitihada za muongo mzima wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuimarisha na kudumisha Utawala Bora katika Tanzania zimetambuliwa kimataifa kwa Rais kutunukiwa Tuzo la Utawala Bora Barani Afrika mwaka 2015 (Good Governance in Africa.)

Rais Kikwete ametunukiwa Tuzo hiyo na Taasisi ya African Achievers Awards yenye makao yake makuu katika Afrika Kusini kutokana na kutambua mchango wake mkubwa katika kulea, kuimarisha, kuendeleza na kudumisha Utawala Bora katika Tanzania katika miaka yote 10 ya uongozi. Rais Kikwete anajiunga na watu wachache ambao wamepata kupokea tuzo hiyo tokea lilipotolewa kwa mara ya kwanza kwa Askofu Mkuu Desmond Tutu wa Afrika Kusini mwaka 2011 kwa kutambua mapambano yake katika kutetea haki za binadamu,usawa, haki na amani.

Rais Kikwete ameteuliwa kutoka miongoni mwa zaidi ya watu 1,202 ambao majina yao yaliwasilishwa kwenye Jopo la Kimataifa Linalojitegemea na lenye wajumbe kutoka Uingereza na Afrika Kusini kwa ajili ya uteuzi. Kutokana na tunuku hiyo, Rais Kikwete amealikwa kwenda Afrika Kusini kupokea tuzo hiyo katika sherehe kubwa inayofanyika jioni Jumamosi, Julai 25, 2015 kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Sandton (Sandton Convention Centre) mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

Kwa sababu ya kukabiliwa na shughuli nyingi hapa nyumbani, Rais Kikwete amemwomba Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Asha Rose Migiro, kumwakilisha katika sherehe ya kupokea tuzo hiyo ambako pia atatoa mada kuhusu “Umoja wa Afrika: Fursa na Changamoto (Africa’s Unity: Prospects and Challenges) kwa niaba ya Rais Kikwete. Tuzo za African Archievers Awardszinalenga kuwatambua watu binafsi na taasisi ambazo zimejitambulisha kwa michango yao kwa ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika.

Katika barua ya kumjulisha Rais Kikwete kuhusu uteuzi wake, Mtendaji wa African Achievers Awards, Bwana Rex Indaminabo amesema: “Uongozi wa African Achievers Awards unayo furaha kukujulisha juu ya uteuzi wako wa kupokea Tuzo la 2015 African Achievers Awards katika kundi la Utawala Bora Barani Afrika.” Ameongeza Mtendaji huyo: “Ni kwa furaha na heshima kubwa kuwa wajumbe wa Bodi ya Ushauri na Taasisi ya Uongozi na Menejimenti wanakuandikia kukupongeza kwa kuteuliwa kwenye orodha ya mwisho na hatimaye kuwa mshindi wa Tuzo la African Achievers Awards katika kundi la Utawala Bora katika Afrika.”








All the contents on this site are copyrighted ©.