2015-07-25 07:55:00

Mtafuteni Mungu ili muweze kujiaminisha kwake!


Kadiri ya tafiti mbalimbali za kijamii idadi ya Wakatoliki ulimwenguni inakadiriwa kuwa ni asilimia ishirini. Idadi hii ambayo inaweza kuonekana kuwa ni kidogo inategemewa kuwa kama unga kidogo ambao umefichwa katika pishi na kuwekewa chachu ndogo ya Kristo. Maisha ya ushuhuda na kuwajibika kama wakristo ni sababu tosha na jambo la kututia matumaini kwamba Kristo anaendelea kuulisha ulimwengu wote, na watu wote “watakula na kushiba”. Kwa utangulizi huu mfupi, napenda kukukaribisha mpendwa katika Kristo kwa tafakari ya Neno la Mungu tunapoadhimisha Dominika ya 17 ya mwaka B wa Kanisa.

Katika somo la kwanza tunaona muujiza wa Nabii Elisha ambapo anawalisha watu wake aliongozana nao. Neno la Mungu linatuambia kuwa walikuwa watu mia moja. Mtumishi wa Nabii Elisha anaanza kuonesha mashaka: “Je, niwaandikie hiki watu mia?”. Ni uwakilishi wa kufikiri zaidi kibinadamu, yaani, kutompatia nafasi mwenyezi Mungu. Mtumishi huyu anawakilisha kundi lile ambalo haliwezi kuweka tumaini yao kwa mwenyezi Mungu. Nabii Elisha hakika ni mtu wa Mungu, hana wasiwasi, anajua kuwa Mungu yupo pamoja nao. Anaimba moyoni mwake pamoja na mzaburi: “waufumbua mkono wako, wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake”. Msukumo huu wa kiimani moyoni ndiyo unaompatia uhakika na kumjibu yule mtumishi wake: “uwape watu, ili wale; kwa kuwa Bwana asema hivi, watakula na kusaza”.

Muujiza huu tunaousikia katika somo la kwanza tunausikia pia katika somo la Injili. Hapa ni Kristo mwenyewe, Mwana wa Mungu, Mungu kweli na mtu kweli anatenda, anawalisha watu zaidi ya elfu tano kwa mikate mitano ya shayiri na samaki wawili. Sehemu hii ya Neno la Mungu inadokeza pande mbili tulizotafakari katika somo la kwanza hapo juu. Wapo Mitume wa Yesu ambao wanatishwa na uwiano uliopo kati ya kundi la watu na kiasi kidogo ama cha pesa au cha chakula walichokuwa nacho. Upande wa pili anasimama Kristo ambaye anaamini katika uwepo wa Mungu na katika nguvu za utendaji wake.

Somo hili la Injili linatupatia jambo la ziada, kwamba imani yetu juu ya uwepo wa Mungu inatosha kuonesha wema wake mkuu kwetu. “Yesu akasema, waketisheni watu”. Ni ishara ya kuwaambia kuwa kuweni na imani, ni kutaka kuwakumbusha ukuu wa Mungu ambao unatenda katika udogo wetu. Tunapoamini katika uwepo wa Mungu, Yeye hujenga katika vile vilivyomo ndani mwetu. Hapa tunataadharishwa kuepa kupima mambo katika jicho la kibinadamu na pia kuepuka ubinafsi. Mitume walifikiri kuwa kiasi kidogo cha fedha walichokuwanacho kingewatosha wao tu pengine na watu wengine wachache. Hii ilikuwa pia ni dalili ya uchoyo, ni tabia ya kutokuwa tayari kushirikishana na wengine.

Mtume Paulo katika somo la pili anatupatia njia ya kwenda: “mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo, na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani”. Huu ni wito wa kila mmoja wetu kuwa tayari kutumikia katika nafasi yake aliyopatiwa na Mungu tena kadiri ya maongozi ya Mungu na si katika tamaa na fikra za kibinadamu. Mshikamano katika maisha yetu kama Wakristo ni uthibitisho wa uwepo wa Mungu kati yetu na ulimwengu utaendelea kustaajabia wema wa Mungu na miujiza yake ikitendeka kati yetu.

Tukiwa na Mungu ndani yetu kwa hakika tutastaajabisha ulimwengu. Kristo leo hii bado anahitaji mikate mitano na samaki wawili tulionao ili kulisha kundi kubwa. Hivi ndivyo vipaji na karama ambazo tumekirimiwa bure na Mungu. Kila mmoja wetu anaalikwa kuwa tayari kutumikia kwa kadiri ya karama yake; kila mmoja anaalikwa kutumikia kwa kadiri ya nafasi yake; na lililo la muhimu zaidi ni kutumikia kwa kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Kristo anaposema “mtu akinipenda mimi na kulishika Neno langu, Baba yangu pia atampenda nasi tutakuja kukaa naye”, anataka kutuonesha faida ya kutenda yote kadiri ya Neno la Mungu. Uwepo wa Mungu katika jamii ya mwanadamu unaonekana zaidi pale mwanadamu anapolishika Neno lake na kuzitii amri zake. Huku ndiko kuufanya ufalme wa Mungu kuendelea kuwepo kati yetu kila siku. Utii wetu kwa Neno la Mungu kwa hakika kunamfanya Mungu kuwa pamoja nasi na kutuongoza katika kila tulitendalo. Hapo ndipo tunapoustaajabisha ulimwengu kwa ufanisi mkubwa unaotokana utendaji wetu huu.

Jamii yetu ya leo imegubikwa na mawazo ya ukinzani katika Neno la Mungu. Ni aghalabu kumwona mwanadamu wa leo anaweka tumaini lake kwa Mungu. Mwanadamu amehadaika kwa ajili ya kiburi chake na kuona nguvu na karama alizo nazo ni kwa sababu ya uwezo wake binafsi. Matokeo yake ni kuwa na jamii ambayo imejaa ubinafsi, jamii ambayo mmoja hajali uwepo wa mwingine. Hivyo hakuna anayekuwa tayari kujitoa muhanga kwa ajili ya wenzake, hakuna anayekuwa tayari kushirikishana na wenzake kile kidogo anachokirimiwa na mwenyezi Mungu.

Jamii yetu ya leo inatenda katika fikra za kibinadamu. Matokeo yake ni wingi wa matukio ya kukata tamaa. Wengi leo hii wanaingia katika msongo wa mawazo na hata kufikia hatua ya kujitoa uhai kwa sababu tu tarakimu moja katika akiba yake ya benki imedondoka, au kwa sababu tu yule alitegemea kuwa rafiki na msiri wake amemlaghai na kumwachia kidonda kikubwa maishani. Dunia yetu ya leo nayo haitoi fursa kwa mwanadamu kuona upande wa pili, yaani, kumtafuta Mungu na kujitegemeza kwake. Mwanadamu anabaki katika hali ya mateso na kukata tamaa akiwa peke yake bila kukumbuka  na kukiri pamoja na mtumishi wa Mungu Ayubu akisema: “najua kwa hakika mtetezi wangu yu hai”.

Tunaalikwa Dominika ya leo kuhuisha tena uwepo wa Mungu katika yetu. Kila mara tunapolisikia Neno lake na kushibishwa kwa chakula cha kimbingu, yaani, Ekaristi takatifu ni wakati wa kupyaisha tena uwepo wake ndani ya mioyo yetu. Hivyo ni wakati wa kumpatia Yeye “anayeshibisha kila kilicho hai matakwa yake” kazi zetu, familia zetu, jumuiya zetu na yote tuliyonayo ili kwa uwepo wake wengi washibishwe na tulichonacho haidhuru ni kidogo kiasi gani. Idadi yetu kama wakatoliki hapa ulimwenguni inatosha kabisa kuwa chachu kidogo ambayo itaweza kuchachusha donge kubwa. Tunapoitikia wito wa Mungu na tunapoisikia sauti yake tuitikie kweli kwa uhalisia katika maisha yetu ya kila siku.

Na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.