2015-07-25 09:58:00

Maonesho ya vyuo vikuu Tanzania ni fursa kwa wanafunzi kufanya maamuzi mapema!


Serikali ya Tanzania imepiga hatua katika kuimarisha miundo mbinu kwenye sekta ya elimu ili kuiwezesha nchi kuendelea na mikakati ya kuhakikisha kuwa kila mtanzania anapata elimu ya viwango vya juu kwenye enzi hii ya utandawazi.  Hayo yamesemwa na makamu wa Rais wa Tanzania Dr. Mohamed Gharib Bilal tarehe 23 Julai 2015 alipokuwa akifungua rasmi maonesho ya mwaka huu ya vyuo vikuu ambayo yanafanyika kwenye ukumbi wa kitaifa wa Mwalimu JK Nyerere jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais ameviomba vyuo vikuu vijikakamue katika masuala ya tafiti na uchapishaji wa matokeo ya tafiti hizo kwa manufaa ya jamii nzima ya binadamu na kuhakikisha kwamba, nchi haipungukiwi na rasilimali watu waliotayarishwa vizuri kitaaluma na kimaadili.  Alisema kwamba, kuna umuhimu wa kushikana mikono kwa taasisi za ndani ya nchi na zile za kigeni ili kujifunza na kuiendeleza ndoto ya Tanzania ya kuwapatia wananchi wake elimu bora.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho hayo, Mkurugenzi msaidizi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dr. Chacha Musabi amesema kwamba maonesho hayo huandaliwa kila mwaka na Tume ya Vyuo Vikuu ya Tanzania (TCU), ikishirikiana na Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi (MOEVT) nchini Tanzania.  Lengo la maonesho hayo ni pamoja na kuwapatia fursa wanafunzi watarajiwa kuvifahamu vyuo vikuu na hivyo kuweza kufanya maamuzi ya kufaa wanapoelekea kukamilisha masomo yao ya sekondari na kujiandaa kujiunga na mafunzo ya elimu ya juu na vyuo vikuu.

Pamoja na vyuo vilivyojitokeza kwenye maonesho hayo ni Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge kilichoko mjini Moshi, ambacho ni kimoja kati ya vyuo vichanga zaidi nchini Tanzania.  Kwa mara ya nne chuo hiki kimeshiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo ya vyuo vikuu yanayoendelea jijini Dar es Salaam.  Chuo cha Mwenge kilichoko mjini Moshi karibu na Mlima Kilimanjaro ambao ndio mlima mrefu zaidi Afrika, sasa ni Chuo kikuu cha kujitegemea baada ya kupata hati ya kujitegemea hapo mwaka 2014. 

Chuo hiki kinamilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na kinatoa elimu ya juu kwenye masuala ya elimu, sayansi, elimu ya jamii, elimu ya biashara, sayansi ya compyuta na mengineyo.  Chuo kinapokea wanafunzi kutoka mikoa yote ya Tanzania na hata kutoka nje ya nchi hiyo.

Maonesho ya vyuo vikuu yamevipa vyuo kama kile cha Mwenge fursa ya kujitangaza na kujifunza kutoka kwenye vyuo vingine vilivyobobea ndani na nje ya Tanzania nchini Tanzania. Mwaka  2015 maonesho hayo yamehudhuriwa na vyuo 78 ikiwa vyuo 64 ni vya ndani ya Tanzania, na vyuo 13 ni vya kimataifa.  Chuo cha Kikatoliki cha Mwenge kimepata fursa ya kuuza program zake ikiwemo program mpya ya shahada ya uzamivu kwenye masuala ya elimu (PHD in Education) itakayoanza kutolewa kuanzia Mwezi Septemba, 2015.

Akishiriki kwenye maonesho hayo, Naibu Mkuu wa Chuo cha Kikatoliki cha Mwenge, Taaluma, Dr. Modest Levira amesema kwamba, ofisi yake inafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba Chuo Kikatoliki cha Kikatoliki cha Mwenge kinafikia malengo yake ya kuwa chuo bora zaidi Afrika Mashariki na ya kati, kwenye masuala ya elimu, utafiti na huduma kwa jamii.  Amesema kwamba dira ya Chuo hicho “Lux Mundi” au “Mwanga wa dunia” inaonyesha mwelekeo wa chuo hicho katika kuwatayarisha wasomi waliobobea na watakaoweza kutoa huduma kwa jamii mahali popote, sio tu nchini Tanzania, bali pia ulimwengu mzima.

Na Sr. Bridgita Samba Mwawasi,

Dar Es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.