2015-07-25 11:21:00

Kanzu liwe ni vazi la Ibada na kielelezo cha utakatifu wa maisha!


Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania linajiandaa kwa kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 200 tangu Mtakatifu Gaspar del Bufalo alipoanzisha Shirika hili nchini Italia sanjari na tukio la kuzindua Kanda mpya ya Shirika la Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania, hapo tarehe 8 Agosti 2015, Jimbo kuu la Dodoma. Yafuatao ni mahubiri yaliyotolewa na Padre Reginald Mrosso, Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania wakati akiwapatia vazi la Ibada na utambulisho wa kifrateri, majandokasisi saba, Jumamosi tarehe 25 Julai 2015, Parokiani Chibumagwa, Jimbo Katoliki la Singida.

Ndugu zangu; tumekusanyika hapa katika adhimisho la sadaka takatifu ya misa kuwapongeza na kuwasindikiza kwa sala na sadaka zetu katika safari yao ya wito ndugu zetu MAFRATERI BENJAMIN A. MWINUKA, ETSON KUNYANJA, KARLO E. MLELWA, PRINCEPIUS MTABUZI, SENEN PIUS, TITTO PHILLIP NA WINCHISLAUS L. LUVAKUBANDI. Hawa wamemaliza mwaka wa pili wa malezi katika nyumba yetu ya Malezi ya Mtakatifu Fransisko Saverio iliyoko Parokia ya Chibumagwa, Jimbo Katoliki la Singida, Tanzania na wanajiandaa kuanza masomo ya taalimungu katika Chuo cha JUCO.

Wanapewa mavazi rasmi ya kifrateri na kukabidhiwa rasmi Katiba ya shirika letu, tayari kuanza safari ya majiundo ya kimissionari ndani ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania. Tumshukuru Mungu kwa zawadi ya wito aliyowajalia ndugu zetu hawa.

Maisha ya wito – maana yake ni maisha ya imani ya kumfuata Mungu na ni itikio la mtu katika uhuru wake akimfuata Roho wa Mungu na akitaka kutimiza mapenzi ya Mungu Baba tu. Historia ya kanisa inaongozwa na Mungu mwenyewe anayemwita mwanadamu na kumtuma aende akafanye kazi aliyomwagiza. Yafaa nini mtu kuupata ulimwengu wote na kuiangamiza nafsi yake? Mathayo 19,16. Kila mmoja wetu anatambua jinsi ilivyo vigumu kuondokana na mazoea yetu, hali tulizozea, mila na desturi zetu, hali zetu, mavazi yetu tuliyozoea n.k. Uamuzi wenu huu unatoa majibu juu ya uwezekano wa kufanya tofauti katika ulimwengu huu geugeu. Lakini si kufanya tofauti tu kwa sababu ya kufanya tofauti – tofauti mnayotaka kuonesha leo hii ni katika kumtumikia Mungu kwa ushuhuda wenu wa maisha. Hongereni sana.

Imani hufungua njia ya matembezi na kutuongoza katika histori ya maisha yetu. Na ili kuweza kuelewa imani ni nini, hatuna budi kuhadithia ule mzunguko wake, njia ya wanadamu waamini, kama tunavyoona katika Agano la Kale. Kwa namna ya pekee tunamwona Abrahamu, baba yetu wa imani. Anapewa jukumu maalumu. Mungu anamwita, anajifunua kama Mungu anayeongea naye na anayemwita kwa jina. Imani huendana na kusikiliza/kusikia.

Abrahamu hakumwona Mungu, lakini anasikia sauti yake. Kwa njia hii, imani huchukua nafasi/tabia/hali ya nafsi ya mwanadamu. Hivyo Mungu huyo hafungwi na wakati, nafasi, mahali n.k bali huhusianishwa na mtu, Mungu wa Abrahamu, Isaka, Yakobo na anafanya agano na mtu. Imani huwa ni jibu kwa Neno hilo la Mungu kwake yeye anayeongea nasi. Na. 8 – Mwanga wa Imani. Ninyi pia leo mnaingia katika mzunguko huo wa mpango wa Mungu wa ukombozi. Hata mmoja wenu asijivunie nguvu zake mwenyewe. Hutafika mbali. Imani si mtaji wa maskini,kwamba ni nguvu zake mwenyewe, kama waimbavyo wanamuziki, bali ni mtaji wa Mungu na mpango wake mzima wa ukombozi. Mababu wa imani wawe changamoto kwenu.

Leo tunapoungana na Kanisa zima na tunapoadhimisha matendo makuu ya Mungu katika watakatifu wake kama mtakatifu Yakobo hatuna budi kumshukuru Mungu kwa ukuu wake. Kuweni imara na thabiti katika imani kama aliyokuwa nayo mtakatifu huyu. Tangu alipopata wito wake hakurudi nyuma. Tunaambiwa kuwa wakati ya mateso yake makali askari mmoja alipoona uvumilivu wake na ushupavu wake katika kushuhudia imani ya Kikristo, aliungama imani ya Kikristo. Na kwa kuungama imani mbele ya baraza, naye askari yule akauawa pamoja naye. Huu ndio ushuhuda thabiti.

Leo mnavaa vazi jipya la kifrateri na mnaalikwa kuvua utu wa zamani – vaeni utu mpya –Efe. 4:22.... Mtakatifu Gaspar alivaa kanzu la kifrateri akiwa na umri wa miaka 10. Rej. “St. Gaspar, saint of the People” Uk.16.... tunaambiwa kuwa alitambua fika maana ya vazi lile. Alihakikisha daima linabaki safi na jeupe na mama yake anasema kwa tabasamu – kwa kanzu lako hili mwanangu umeniongezea kazi ya kufua nguo. Alionekana nadhifu katika vazi lake hili na watu walimwita Mtakatifu mdogo na wengine walisema huyu ni Mtakatifu Lui mwingine.

Mababu wa kale wanaeleza tendo la kuvaa nguo mpya kama alama ya unyofu na unyenyekevu, tendo la kuweka kando unyonge wa nguo zao za kidunia, na kuwa tayari kumvaa Mungu mwenyewe na kwa utakatifu wa maisha yao watambulike mbele ya watu kuwa wamewekwa wakfu ili kumtumikia Mungu. Wito wa Elisha – tunasikia habari juu ya maisha mapya ya Elisha. Anapotupiwa vazi la kinabii na nabii Eliya, anaacha yote na kutoa alivyokuwa navyo , anawapatia watu na maisha yake yanabadilika, akawa mhudumu wa Eliya. 1 Fal. 19: 19 ..... Vazi hili lisitumike kama mapambo bali vazi la kazi.

Sijui wanamitindo wetu wa wakati wa sasa watasema nini kuhusu mtazamo huu. Twafahamu wazi kuwa wao hutumika tu na kupitia kwao nguo zinapata jina, umaarufu, soko n.k. na baadaye mwenye bidhaa hizo anapata utajiri wa mali na fedha. Wanatumika kama watu wa mshahara, vitendea kazi tu na baadaye wao wanazeeka na kupoteza hata ile nafasi ya kutumika kama kitendea kazi.

Mavazi haya mnayopewa leo si hivyo. Ninyi si vitendea kazi bali mnapaswa kuwa watenda kazi. Tazameni maisha mapya ya Nabii Elisha. Mnapewa vitendea kazi Katika makabila yetu – tunakumbuka kuwa lilipowaliwa vazi fulani, pia ilimaanisha kitu/tukio/alama fulani n.k – kwa ajili ya shughuli fulani mfano mfalme, wanandoa, mashujaa, maaskari, wacheza ngoma, waombolezaji, wanawali, marehemu (maiti) n.k Basi nanyi mtambulike na watu na wakati wote kuwa wafuasi wake Kristo kwa vazi lenu hili. Nami nawaalika ninyi na sisi wote hapa tumfuate Bwana.

Tumsifu Yesu Kristo. Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.