2015-07-25 14:54:00

Jamani wee! Acheni Mungu aitwe Mungu! Wito una maajabu yake!


Kwako Ee Bwana, mimi ni udongo wa mfinyanzi, nifinyange unavyotaka. Ni maneno ya Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba wakati wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 40 tangu alipopewa Daraja Takatifu la Upadre kunako tarehe 28 Julai 1974. Tarehe 11 Julai 1999 akawekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida. Tarehe 15 Januari 2013 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Desiderius Rwoma anakiri kuhusu mchango mkubwa uliotolewa na wazazi wake katika maisha na majiundo yake kuelekea wito wa kipadre. Anasema hakuna kitu anachopenda duniani kama Upadre wake, matunda ya majiundo makini katika safari ya maisha yaliyojikita katika sala, ibada na uchaji wa Mungu uliokuwa unashuhudiwa ndani ya familia yake.

Tangu akiwa mdogo, alitamani na akapenda kutumia Altareni. Akachaguliwa kufanya mtihani wa kujiunga na Seminari ndogo ya Rutabo, Jimbo Katoliki Bukoba, lakini akasahau kwenda kufanya mtihani, huo ukawa ni mwanzo wa kufifia kwa ndoto yake ya kuwa Padre. Hakukata tamaa, akaendelea na maisha kwa kutumikia Altareni na sala. Alipoingia Darasa la nane, akaitwa kwenda kujiunga na Seminari ndogo, tayari kuanza safari ya wito wake kama Jandokasisi.

Hata katika umaskini wa familia yake, wazazi walimhakikishia kwamba, ”Aliye na baba ana jiwe na aliye na mama ana jiwe la kusagia”. Wazazi walihakikisha kwamba, mtoto wao anapata walau sehemu ya mahitaji ya kwenda nayo shuleni, mambo mengine, Mungu mwenyewe atajua. Kwa neema ya Mungu, akabahatika kupata Daraja takatifu la Upadre hapo tarehe 28 Julai 1978. Usikose kujiunga na Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakapokujuza, yale yaliyojiri katika maisha na utume wake kama Padre, Askofu wa Jimbo Katoliki Singida na sasa Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba! Wanasema, Jamani, acheni Mungu aitwe Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.