2015-07-24 09:28:00

Simameni kidete kutetea na kudumisha Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliotuma kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles katika maadhimisho ya Siku ya Uhai Kitaifa, anaitaka Familia ya Mungu nchini humo kusimama kidete kulinda, kutetea zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na kwamba, Kanisa halina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, daima likiambata Injili ya uhai na utamaduni wa mapendo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, tarehe 26 Julai 2015, litaadhimisha Siku ya Uhai Kitaifa kwa kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete, kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kuna watu wanaoendelea kuaminishwa kwamba, watu wenye magonjwa sugu hawana sababu ya kuendelea kuishi na matokeo yake wanataka watu hawa kuonewa huruma kwa njia ya kifo laini.

Huu ni uwongo unaokumbatiwa na utamaduni wa kifo. Haya ni maneno ambayo yaliwahi kusemwa na Baba Mtakatifu Francisko akiwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete, kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya Uhai. Maadhimisho haya ambayo hufanyika kila mwaka, yanaongozwa na kauli mbiu “Kuendeleza maisha, kupokea kifo”.

Maaskofu katika ujumbe huu wanakiri kwamba, katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika sayansi na tiba ya mwanadamu. Watu wanaosumbuliwa na magonjwa sugu wanaweza kupewa matibabu kwa muda mrefu, jambo ambalo kweli ni la kumshukuru Mungu. Lakini, wakati huo huo Maaskofu wanakaza kusema, mwanadamu tangu anapoazaliwa anaanza safari ya kuelekea katika kifo, iko siku atakumbana na kifo.

Madaktari na wataalam wamegundua njia na mbinu mbali mbali katika kufanya maamuzi juu ya hatima ya maisha ya mwanadamu; mbinu ambazo wakati mwingine zimekumbatia utamaduni wa kifo. Maaskofu wanakumbusha kwamba, jambo la msingi ni watu kutambua kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, wanahamasishwa na Mama Kanisa kupenda, kuheshimu na kushuhudia tunu hii msingi katika uhalisia wake.

Zawadi hii itunzwe kwa makini na kamwe isichezewe na wajanja wachache wanaotaka kujitajirisha kwa mateso na mahangaiko ya watu na kwamba, Mwenyezi Mungu atamwita mja wake kwa wakati muafaka. Maaskofu wanawaalika waamini kupokea Fumbo la Kifo kwa imani na matumaini kwa kukubali tiba zinazowasaidia kutunza na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu.

Familia ni mahali ambapo watu wanaweza kufanya maamuzi magumu katika maisha ya watu wao. Hapa kuna haja ya kufanya majadiliano ya kina, si tu kuwashirikisha madaktari na wataalamu kutoka katika sekta ya afya, lakini familia nzima inapaswa kuhusishwa kuhusu tiba na hatima ya maisha ya mgonjwa, ili familia iweze kutambua kile kinachoendelea kwa mgonjwa wao, tayari kumsindikiza mgonjwa huyu hatua kwa hatua. Lakini swali la msingi hapa ambalo wanafamilia wanapaswa kujiuliza: ni ikiwa kama maamuzi yatakayotolewa yanakumbatia Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, maisha ya nizawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inapaswa kulindwa, kuhudumiwa na kushuhudiwa katika hatua mbali mbali za ukuaji wa mwanadamu. Kamwe watu wasikumbatie utamaduni wa kifo kwa sera na ulaghai inaofanywa na baadhi ya watu ndani ya jamii kwa ajili ya mafao yao binafsi au kwa kuelemewa na ubinafsi na utandawazi usioguswa na mateso wala mahangaiko ya wengine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.