2015-07-24 07:52:00

Mameya waunda umoja kupambana na uchafuzi wa mazingira, utumwa na rushwa!


Baada ya Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii kuwakusanya mameya kutoka katika majiji makuu duniani ili kujadili sera na mikakati ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na utumwa mamboleo hapa mjini Vatican, mameya 70 wametoa azimio la kuunda Umoja wa Mameya ili kukuza maendeleo endelevu. Umoja huu unatarajiwa kuzinduliwa rasmi wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Marekani, Septemba  2015.

Taarifa zinaonesha kwamba, tukio hili la kihistoria litazinduliwa rasmi hapo tarehe 24 Septemba 2015 kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani, mkesha wa ziara ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Mameya pamoja na mambo mengine wanataka kujifunga kibwebwe kupambana na rushwa, baa la umaskini pamoja na biashara haramu ya binadamu.

Azimio la kuunda umoja wa  mameya limetolewa mjini Vatican kwa kufuata utashi wa mameya waliokutana na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya jitihada zake  za kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni matumaini ya mameya hawa kwamba, umoja huu utaweza kuwashirikisha viongozi wengi zaidi, tayari kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu wa mwandamu unaodharirishwa kutokana na uchafuzi wa mazingira, baa la umaskini pamoja na biashara haramu ya binadamu.

Mameya wanataka kujifunga kibwebwe kupambana na baa la njaa, kwa kuwahakikishia wananchi wao usalama wa chakula, uhakika wa tiba, elimu makini, mahitaji msingi ya binadamu pamoja na usawa kati ya watu; mambo msingi katika kudumisha mchakato wa maendeleo endelevu.

Mameya wanatambua athari na madhara makubwa yanayosababishwa na biashara haramu ya binadamu inayoendelea kukua na kupanuka mwaka hadi mwaka kutokana na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka. Mameya wanataka kuhakikisha kwamba, wanapambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; rushwa na ufisadi; mambo ambayo yanakwamisha mchakato wa maendeleo endelevu na mafao ya wengi. Huu ni mwaliko wa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira, ili kupunguza hewa ya ukaa kama sehemu ya mkakati wa Jumuiya ya Kimataifa ya kulinda na kutunza mazingira, nyumba ya wote.

Mameya kwa namna ya pekee katika azimio hili wanaongozwa na Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, unaoitaka Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa ajili ya kutunza mazingira. Hapa kuna haja ya kuwa na rasilimali fedha ili kuweka sera na mikakati ya muda mrefu itakayosaidia kulinda na kudumisha mazingira.

Utu, heshima, haki msingi za binadamu na kazi nzuri ni kati ya mambo ambayo yatashughulikiwa na wanachama wa umoja wa mameya duniani. Ni wajibu wa jamii kushikamana na kuwasaidia maskini wanaoendelea kuongeza katika miji mingi duniani kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, kwa kuheshimu na kuthamini utu wao kama binadamu. Huu ni wajibu ambao pia unapaswa kutekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbali mbali.

Sekta ya elimu ya juu na vyuo vikuu inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa ugunduzi, tayari kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu. Tarehe 24 Septemba 2015 wakati wa mkesha wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mameya kutoka majiji mbali mbali duniani, wataweka rasmi sahihi kwenye hati ya uzinduzi wa umoja wa mameya duniani kwa ajili ya kupambana uchafuzi wa mazingira; umaskini, biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo, rushwa na ufisadi.

Baba Mtakatifu Francisko amepokea azimio hili kwa mikono miwili kwa kuwataka wadau mbali mbali kushirikiana kwa karibu zaidi ili kudumisha ekolojia ya binadamu; tayari kutoka kifua mbele ili kupambana na uchafuzi wa mazingira, nyumba ya wote, hali inayotishia usalama na maisha ya watu wengi duniani.

Ni fursa ya kupambana na biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo pamoja na viungo vya binadamu, biashara ambayo kwa sasa ni kashfa kubwa kwa utu na heshima ya binadamu; mambo yanayosababisha kinzani na utengano wa kijamii. Ni dhamana na wajibu wa mameya kufanya kazi kwa kushirikiana, ili kwa pamoja kuweza kufikia malengo yanayobainishwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa kila mji na jiji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.