2015-07-23 10:14:00

Ushuhuda wa Kikristo unapaswa kujikita katika kanuni maadili na utu wema


Kardinali Reinhard Marx, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani kwa kushirikiana na Bwana Alois Gluk, Rais wa Kamati kuu ya Wakatoliki nchini Ujerumani, kwa pamoja wanawataka Wakatoliki, wafanyabiashara, wachumi na wamiliki wa taasisi za fedha nchini Ujerumani kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuwekeza katika miradi inayozingatia kanuni maadili na kwa ajili ya maendeleo endelevu. Hii ni changamoto kwa Wakatoliki kuhakikisha kwamba, wanashuhudia imani yao katika uhalisia wa maisha kwa kuzingatia kanuni maadili na maendeleo endelevu.

Kardinali Marx anasema kati ya mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee ni Injili ya uhai, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza utu na heshima ya binadamu pamoja na haki zake msingi. Waamini wanapaswa pia kuhakikisha kwamba, wanawajengea wafanyakazi wao mazingira bora ya kazi pamoja na kuwapatia ujira stahiki, ili kuweza kutekeleza majukumu ya kifamilia na kijamii. Pale inapowezekana, wawekezaji wasaidia pia mchakato wa maendeleo kwa ajili ya nchi changa zaidi duniani sanjari na utunzaji bora wa mazingira.

Kwa upande wake, Bwana Alois Gluk anasema, Kanisa linaangaliwa kwa namna ya pekee jinsi ambavyo linatumia rasilimali zake na kutokana na umakini wake, hapo Kanisa linaweza kuwajengea watu imani na matumaini. Taasisi za Kanisa zinazosimamia masuala ya fedha na maendeleo ya watu hazina budi kujikita katika kanuni maadili, ukweli na uwazi; na yote yawe ni kwa ajili ya malengo yaliyoainishwa na Mama Kanisa na wala si kwa ajili ya mafao ya mtu binafsi. Rushwa, wizi na ufisadi wa mali ya Kanisa ni kashfa inayowaletea waamini masikitiko makubwa.

Wawekezaji wanaotumia jina la Kanisa wanapaswa kuachana na miradi inayodhalilisha uhai, utu na heshima ya binadamu. Si vyema kwa Wakatoliki kujihusisha na biashara za utengenezaji wa silaha; mawasiliano yanayojikita katika masuala ya picha chafu au utengenezaji wa watoto katika chupa au kujipatia faida kubwa kutokana na fedha ya rushwa na ufisadi. Mambo yote haya yanatia kasoro katika ushuhuda na maisha ya mwamini. Kardinali Marx wakati wa uzinduzi wa mwongozo huu kwa ajili ya wafabiashara, wachumi na wamiliki wa miradi mbali mbali anakaza kusema, hii ni sehemu ya utekelezaji kwa njia ya matendo wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko juu ya utunzaji bora wa mazingira “Laudato si” yaani, “Sifa iwe kwako” juu yya utunzaji wa nyumba ya wote.

Waraka huu una utajiri mkubwa anasema Kardinali Marx, kwani unakazia umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira; unachambua na kupembua mifumo ya uchumi na umuhimu wa kujikita katika mshikamano na udugu, ili kuwa na sera na mikakati ya kiuchumi yenye mwelekeo mpya unaojikita katika maendeleo endelevu na ustawi wa wengi. Uwekezaji unaozingatia kanuni maadili unapaswa kuwa ni sehemu ya maisha na vinasaba vya Kanisa katika sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji. Hapa viongozi wa Kanisa pamoja na wafanyakazi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali fedha, vitu na watu wanatakiwa kuwa makini sana na mambo yote haya.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, kanuni maadili inaongoza sera na mikakati ya uwekezaji pamoja na shughuli zote za uchumi. Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani limeamua kutoa mwongozo huu kwa kuzingatia kwamba, kutokana na utandawazi pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia, dunia inaonekana kuwa kama kijiji. Rasilimali fedha, vitu na watu zinavuka mipaka, kwa kutafuta faida kubwa. Lakini, Wakatoliki wanapaswa kujiuliza, wanawekeza wapi mtaji wao?

Mwongozo huu ni matunda ya ushirikiano kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani na waamini walei wanaotekeleza dhamana na majukumu yao katika sekta ya vitega uchumi, fedha na maendeleo, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Malengo yanapaswa kupembuliwa kwa kina kwa kuzingatia kanuni maadili na Mafundisho Jamii. Umakini mkubwa unatakiwa tangu pale mtu anapochagua bidhaa na watu wanaomhudumia kuhakikisha kwamba wanakidhi vigezo vilivyotolewa.

Faida inayopatikana inapaswa pia kujikita katika mafao ya wengi; kuangalia kwa makini madhara yanayosababishwa na vitega uchumi vilivyopo katika mazingira na afya za watu. Miradi na vitega uchumi vilenge katika kusaidia mchakato wa kupambana na baa la umaskini duniani, kutunza mazingira na ekolojia ya binadamu. Utekelezaji wa mwongozo huu unaweza kulisaidia Kanisa kuwajengea watu imani katika masuala ya uchumi, maendeleo na utunzaji bora wa mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.