2015-07-23 08:41:00

Msimgeuze Yesu kuwa "Mamantilie pangu pakavu", Gawaneni rasilimali kwa haki!


Hali halisi ya takwimu ya watu na mgawanyo wa raslimali ya ulimwengu mzima ni kwamba: Asilimia moja (1%) tu ya watu wote ulimwenguni wanamiliki zaidi ya asilimia hamsini (50%) ya raslimali yote ya ulimwengu. Nusu ya raslimali iliyobaki (50%) haijagawika sawa kati ya asilimia tisini na tisa (99%) iliyobaki ya watu. Katika nusu ya raslimali iliyobaki ni asilimia ishirini (20%) tu ya watu wanamiliki raslimali asilimia arobaini (40%) ya utajiri. Asilimia themanini (80%) ya watu wote wanamiliki raslimali asiliamia tano (5%) tu. Asilimia iliyobaki ya watu hawana kitu. Ukifanya takwimu kama hizo katika nchi yako utagundua pia kwamba, hakuna mgawanyo wa haki wa raslimali, ndiyo maana unakuta matabaka ya “watu wenye nacho na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” na raslimali haitoshi kwa wote.

Ziko namna mbalimbali zinazotumika katika kugawana raslimali. Namna ya kwanza ni ya kimasoko. Namna ya pili ni kujitegemea. Namna ya tatu ni ufadhili unaoongozwa na kanuni auni. Injili ya leo inaziainisha aina hizo na kudokeza jinsi bora ya kugawana raslimali zetu ili ziweze kututosha sote na kubaki. Kusudi tuelewe kuwa fasuli hii inahusu mgawanyo wa raslimali ya ulimwengu huu na siyo juu ya Ekaristi peke yake, hebu tuone utata wa fasuli hii.

Utata wa kwanza umelala katika kichwa chake. “Yesu anawashibisha mkutano mkuu.” Je, lengo la Yesu lilikuwa ni kuwashibisha tu watu? Endapo Yesu alifanya muujiza wa kuongeza mikate na kuwashibisha watu, basi binadamu kwa upande wetu hatuna kitu cha kufanya zaidi isipokuwa “kukaa kiwetewete mtama wa mama waliwa na ndege” na kusubiri kudra ya Mwenyezi Mungu. Utata wa pili ni kuwa, kituko hiki cha mikate kimeelezwa mara sita tofauti katika Injili zote. Kwa mfano Mwinjili Yohane anataja mikate mitano na samaki wawili. Wakati mwingine anasema ilikuwa mikate saba. Kuhusu mahali, mmoja anasema ilikuwa jangwani wakati Mwinjili Yohane anasema ilikuwa kwenye uwanda wa nyasi za kijani.

Kuhusu idadi ya watu, wengine wanasema kulikuwa watu elfu nne na hapa anasema walikuwa watu elfu tano. Kuhusu makombo ya mikate, wengine wanasema walikusanya makapu saba, kumbe leo anasema walikusanya vikapu kumi na viwili. Halafu kuhusu umati wote ule hata haijulikani ulitokea wapi na kumfuata Yesu kwa siku tatu mfululizo. Halafu yawezekanaje kijana mdogo tu peke yake awe na mikate mitano na samaki wawili. Aidha iliwezekanaje jioni ile Yesu peke yake afaulu kugawa mikate kwa watu elfu tano, kisha yakusanywe mabaki na kujaza vikapu kumi na viwili, navyo haijulikani walivipata wapi usiku ule.

Kumbe,  kutokana na mautata haya yote yawezekana kabisa kwamba vituko vile vya mkate viliwahi kweli kufanyika mara sita tofauti, lakini pia yawezekana kulifanyika muujiza mmoja tu ila kila  mwinjili alieleza alivyoona yeye inafaa ili kutoa ujumbe muhimu katika maisha yetu.  Kwa vyovyote lengo la Yesu ni kutufunza jinsi ya kuongeza mikate hadi itutoshe sote, yaani jinsi ya kugawana raslimali kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Kwa hiyo, kijana huyu ametajwa hapa kama alama tu, yaani kumwonesha mfuasi bora na mnyofu wa Kristo anayeona mali aliyonayo yanatoka kwa Mungu.

Mikate ya shayiri ni kama mabumunda au “kibombogwa” ilikuwa ni zao linalomea na kukomaa haraka kusudi litumike na watu wa kawaida na maskini, kwa sababu watu matajiri walikuwa wanakula mikate ya ngano bora. Mikate hiyo na samaki ni raslimali ya kawaida na inatolewa kwa upendo na mtoto mnyofu asiye na ubinafsi, uchoyo wala roho ya kwanini!

Baada ya kuona utata huo, sasa tujipate miwani ili tuweze kusoma vyema fasuli hii. Mwinjili anataka tuione Injili hii katika mazingira ya Kipasaka anaposema: “Na Pasaka Sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu.” (Yoh. 6:4). Kisha anatupa madokezo yanayoturejesha kwenye Pasaka ya Wayahudi. Mosi, “Baada ya hayo Yesu alikwenda zake ng’ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia.” (Yoh. 6:1). Biblia inaposema “kuvuka bahari” inarejea kwa Wayahudi walipoivuka Bahari ya Sham toka utumwani Misri. Yesu anawaongoza watu toka utumwani hadi nchi huru ya ahadi. 

Pili, “Na mkutano mkuu wakamfuata.” Musa alifuatwa na watu wengi kutokana na ishara mbalimbali alizozifanya mbele ya Farao na Jangwani. Kuhusu Yesu “Mkutano mkuu wakamfuata Yesu, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa.” (Yoh. 6:2). Kadhalika Yesu anavuka bahari akifuatwa na watu elfu tano ni mfano wa Musa aliyevuka bahari ya Shamu kwa miguu. Tatu, “Naye Yesu akakwea mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake.” Musa alikwea mlimani Sinai, akaonana na Mungu. Mlimani wanapanda watu huru wanaofuata sera za Kristo.

Baada ya kupata miwani hiyo ya kipasaka, sasa tumwone Yesu anavyotugeuzia kibao. “Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula?” Yesu analiibua swali hili lili kumsanifu Filipo huku akilidokeza mwenyewe jibu anapolitumia neno “kununua,” ili kuonesha namna watu wanavyogawana raslimali za ulimwengu huu, yaani kwa njia ya masoko kwa kununuliana na kuuziana. Hii ni mantiki ya kawaida ya kugawana raslimali ambapo tajiri anapanga bei na maskini analazimika kuinunua akitaka kuishi. Kwa vyovyote masoko ni mfumo wa kitumwa, ni ukoloni, ni ukandamizaji unaosababisha magomvi na vita duniani.

Filipo anafanya mahesabu harakahara kisha anajibu: “Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu.” (Mk. 6:7). Hapa Filipo anajaribu kutoa utatuzi wa kwanza unaotofautiana kidogo na huu aliodokeza Yesu. Yaonekana aliwahi kufanya kazi ya „Caritas” ambako kadiri ya utamaduni wa Kiyahudi wa kufadhili ilibidi kugawa kiasi hicho cha denari toka kwenye mali yako ili kusaidia maskini. Hii ndiyo hali halisi ya ufadhili katika ulimwengu wa leo, ya kugawa sehemu fulani tu ya utajiri wako kwa maskini. Njia hii inakuza matabaka, na wengi wanafaidika kwa kupitia migongo ya maskini kwa jina la ufadhili kama zilivyo NGO nyingi.

Pendekezo jingine la kugawa raslimali linadokezwa katika Injili ya Luka pale mitume wanapomwomba Yesu “awaruhusu watu waende mjini kujinunulia chakula wanachohitaji.” Huu ni mfumo wa kujitegemea yaani kila mmoja anajiju mwenyewe. Pendekezo la mwisho linatoka kwa Andrea anayesema “Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili,” kisha anajikatisha tamaa mwenyewe anaposema “lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa?” Hivi ndivyo matajiri na watu wengi wanavyokata tamaa juu ya mali kwamba haitoshi. Lakini Yesu akasema: “Waketisheni watu,” yaani wapumzisheni.

Hili ni rejeo jingine la Pasaka. “Kuketi” kwa kigiriki ni Anapiptein maana yake kulala kwa kujilegeza kwenye majani kama isemavyo zaburi “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu, katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza” (Zaburi 23:1-2). Namna hiyo ya kuketi kwa kujilegeza walifanya Wayahudi wakati wa kusherekea Pasaka, kuonesha wako huru. Kisha “Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru,” maana yake kuinua macho kwa Mungu na kumkiri. Baada ya kutoa shukrani “akawagawia walioketi.” Hapa haisemwi kama amefanya muujiza wa kuongeza mikate, bali ameichukua ile mikate aliyopata anashukuru na kuigawa.

Kumbe, inatubidi kumshukuru Mungu na halafu kugawa kwa wengine utajiri aliotukirimia. Yesu hakufika kuongeza chakula (mkate) bali kuonesha jinsi ya kugawana chakula kwa haki ili kila mmoja aweze kupata chakula na kuridhika. Kama isemavyo barua kwa Timoth. “Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguvu tunaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.” (ITim 6:6-10).

Hatimaye, “Yesu hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake.” Bahati iliyoje, watu wamehamasika na ufadhili walioupata wa kujazwa mikate, wna imani kubwa na Yesu, na wanamtaka ashike dola mara moja. Watu hawa wanamtafuta Mungu anayeweza kuwatendea miujiza na kuwatatulia matatizo yao bure. Kumbe hawakujua kwamba Yesu alitaka kuwafundisha wafanye hivyo wao wenyewe.

Ndugu zangu watu wote tunawakilishwa na umati huu wa watu elfu tano. Tunaishi katika ulimwengu wenye chakula (shayiri na samaki) na raslimali ya kutosha kwa wote na kubaki. Lakini sasa hazitoshi na wengi ni maskini wanakufa njaa kwa vile tunatawaliwa na ubinafsi, ulafi na kuhamakia ukuu. Yesu anataka kututoa katika ulimwengu huu wa utumwa na kutuingiza katika ulimwengu mpya wa ufalme wa Mungu. Tusimgeuze Yesu kuwa “mamantilie pangu pakavu” wa kutujaza tu chakula au kama matajiri wa kutujaza mapesa. Yesu amefika kutufundisha jinsi ya kugawana raslimali za dunia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.