2015-07-23 09:37:00

Mchakato wa maboresho ya sekta ya mifugo nchini Tanzania!


Ifuatayo ni hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa uzinduzi wa mchakato wa maboresho ya sekta ya sekta ya mifugo nchini Tanzania. Amegusia hali ya sekta ya mifugo Tanzania; maboresho ya mifugo, shukrani kwa wadau na hatimaye hitimisho linalowataka watanzania kuondokana na ufugaji wa kuhamahama na kuanza kuingia katika ufugaji wa kisasa na wafugaji wakiwa na maisha bora zaidi kuliko ilivyo sasa. Kwa mengi zaidi endelea!

Nakushukuru Mheshimiwa Titus Kamani, Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa kunialika kuzindua Mpango wa Modenaizesheni ya Sekta ya Mifugo ujulikanao kama ‘Tanzania Livestock Modernization Initiative’. Nakupongeza sana wewe na wataalamu katika Wizara yako na wadau wote walioshiriki katika kutayarisha na kufanikisha Mpango huu tunaouzindua leo. Nawashukuru pia wadau wa ndani na nje waliohudhuria uzinduzi huu. Uwepo wao unatupa uhakika juu ya utayari wao wa kushirikiana nasi katika utekelezaji wa mpango huu.

Hali ya Sekta ya Mifugo Nchini

Mabibi na Mabwana, Tanzania ina utajiri mkubwa wa mifugo barani Afrika. Tanzania ni nchi ya tatu kwa utajiri wa mifugo ikizifuatia nchi za Sudan na Ethiopia. Takwimu za mwaka 2014 zinaonyesha kuwa, Tanzania ina mifugo milioni 25. 8 ambapo, asilimia 97 ya mifugo yote hiyo ni mifugo ya asili. Pamoja na wingi huo, sekta ya mifugo ilichangia asilimia 4.4 ya pato la taifa mwaka 2013 ikiwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 3.8 tu. Aidha asilimia 37 ya Watanzania wanategemea sekta hii kama shughuli yao kuu ya kiuchumi.

Utajiri huu wa mifugo haujaweza kujitafsiri vizuri katika kuinua hali ya maisha ya wafugaji wetu. Kwa sababu hiyo inaifanya shughuli ya ufugaji kuonekana kuwa ni ya kimasikini inayofanywa na masikini. Nilisema wakati wa kampeni na wakati wa kuzindua Bunge la Tisa Desemba 30, 2005 kuwa, hali hii haikubaliki, na kwamba hatutaiacha iendelee hivyo. Nikaelezea dhamira yangu ya kuona kuwa tunaondokana na ufugaji ulio nyuma na duni na kuelekea katika ufugaji wa kisasa wenye tija na kumuongezea mfugaji mapato na hali nzuri ya maisha ya wafugaji.

Nikasema, lazima tuupitie upya mnyororo wa thamani wa sekta ya mifugo, tuboreshe mifugo yetu, tuwe na malisho ya uhakika, huduma bora za ugani ziwepo, huduma ya kinga na tiba ipatikane, utafiti uendelezwe na masoko ya uhakika yapatikane, kwa mazao na bidhaa za mifugo. Lengo ni kuongeza mazao, thamani yake na mapato ya wafugaji.

Kwa sababu hiyo, mwaka 2010 tukaanzisha Programu ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo (LSDP) ambayo ililenga kutoa msukumo mkubwa kwa maendeleo ya sekta ya mifugo. Nilifanya hivyo, baada ya kubaini kuwa Sekta ya mifugo haikuwa ikipewa uzito na kipaumbele stahiki ilipokuwa chini ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP). Pamoja na uamuzi huo, niliunda pia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kusimamia uendelezaji wa sekta hii.

Mafanikio ya Miaka 10 ya Sekta ya Mifugo

Mabibi na Mabwana, Matunda ya utekelezaji wa Program ya Kuendeleza Mifugo yameanza kuonekana. Tumewekeza katika miundombinu ya ufugaji kwa kujenga malambo 1,008, majosho 2,364 na maabara za kisasa za mifugo 104 nchi nzima. Tumechimba visima virefu 101, malambo 370 na kukarabati majosho 499. Sasa tunayo majosho 3,637 ikilinganishwa na majosho 2,177 mwaka 2005. Kwa upande wa kuongeza utaalam na ubora wa mifugo, tumechukua hatua ya kuongeza maafisa ugani kutoka 2,270 mwaka 2005 had 6,041 mwaka 2015 na kuongeza vituo vya uhamilishaji kutoka kimoja mwaka 2005 hadi 8 mwaka 2015 na kuwezesha ng’ombe 955,360 kuhamilishwa katika kipindi cha miaka 10.

Matokeo makubwa yamepatikana pia katika ushirikishaji wa sekta binafsi katika kuwekeza kwenye sekta ya mifugo. Awali shughuli hizi za kuendeleza sekta hizi zilichukuliwa kama shughuli za serikali peke yake. Kutokana na uwekezaji wa sekta binafsi, katika kipindi cha miaka 10 tumeweza kuongeza viwanda vya kusindika maziwa kutoka 22 mwaka 2005 hadi 74mwaka 2015. Viwanda vya kuzalisha vyakula vya mifugo vimeongezeka kutoka 6 mwaka 2005 hadi 80 mwaka 2015 vikiwa na uwezo wa kusindika tani milioni 1.4 kwa mwaka. Uzalishaji wa malisho ya mifugo (hei) umefikia marobota 957,860 kutoka 178,100 mwaka 2005. Viwanda na machinjio ya kisasa mapya 9 yamejengwa katika kipindi hiki. Na usindikaji wa ngozi umeongezeka kutoka vipande 790,000 mwaka 2005 hadi vipande milioni 3.78 mwaka 2014.

Mpango wa Modenaizesheni ya Mifugo

Mabibi na Mabwana; Mafanikio tuliyoyapata yanatia moyo na kutufungulia njia ya kuelekea kwenye ufugaji wa kisasa. Uzinduzi wa Modenaizesheni ya Sekta ya Mifugo Tanzania leo ni ushahidi wa kutosha wa azma yetu ya kujenga juu ya mafanikio tuliyoyapata katika kuweka mazingira ya sekta ya mifugo kukua na kuendeleza miundo mbinu ya kuwezesha ukuaji wa kasi na kisasa wa mifugo nchini. Tunatumia msingi huo sasa kumuendeleza mfugaji, ambaye kuendelea kwake ndio ufunguo wa kuendeleza ubora wa mifugo yenyewe.

Nimefurahi kuwa katika warsha ya siku tano (5) iliyofanyika ya kuandaa Modenaizesheni ya Sekta ya Mifugo, mlijadili vikwazo vinavyozuia maendeleo ya sekta ya mifugo. Mambo yanayosababisha tija na kuwa uzalishaji mdogo yametambuliwa na mapendekezo ya kuyapatia ufumbuzi yametolewa. Uwezo mdogo wa koosafu za mifugo ya asili (Low genetic potential) na ufugaji wa kienyeji ni miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa na washiriki kwa njia ya kisasa na kisayansi. Mmefanya vizuri sana kushirikisha wataalamu wa kutoka ndani na nje ya nchi, taasisi za elimu na wadau wengine wenye uzoefu mbalimbali kuhusu mifugo na ufugaji. Nimefurahi sana kuona kuwa wawakilishi wa wafugaji wameshiriki katika warsha hiyo, kwani hawa hasa ndiyo walengwa wa kwanza wa program hii na yote tuyafanyayo kuhusu ufugaji.

Mabibi na Mabwana,

Uboreshaji huu umelenga kuendeleza mifumo ya ufugaji, malisho ya mifugo na uzalishaji wa mifugo; pia kuboresha kosafu na mbari za mifugo yetu na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo, kupitia usindikaji wa ngozi, nyama na maziwa na ufungashaji na usafirishaji wa bidhaa za mifugo na masoko. Kuendeleza shughuli ya utafiti, mafunzo, huduma za ugani; na zile za kinga na tiba ya mifugo. Miongoni mwa makusudio ya msingi ni kuboresha koosafu za mifugo yetu ya asili ili kupunguza muda wa kubadilika na kuweza kutoa nyama nyingi, maziwa mengi na ngozi bora zaidi. Hii itawezekana kwa kutumia teknolojia za kisasa za uhamilishaji na uhawilishaji kiinitete (Embryo transfer), ambazo zinapendekezwa kutumika pamoja na kuongeza lishe ya mifugo.

Kazi iliyo mbele yetu ni kutekeleza program hii ili itupeleke katika mapinduzi ya sekta ya mifugo. Serikali iko tayari kwa utekelezaji wa program hii maana itachangia sana katika utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka 5 (2016-2020) utakaojikita katika maendeleo ya viwanda. Ukuaji wa viwanda vya usindikaji wa bidhaa za mifugo na ngozi utategemea sana ubora na tija ya mifugo yenyewe. Kwa sababu hiyo, tutaendelea kuendeleza sekta hii kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo na kwa kuendelea kuchochea ushiriki wa sekta binafsi. Tunaomba wadau wetu walioshiriki kuandaa mpango huu, nao kutimiza sehemu ya wajibu wao.

Shukrani kwa Wadau

Mabibi na Mabwana,

Kwa namna ya kipekee nawashukuru Balozi wa Denmark na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (International Livestock Research Institute) kwa kugharamia warsha hiyo na uzinduzi huu. Aidha, nawashukuru vyuo vikuu vilivyohusika katika maandalizi, na taasisi ya kimataifa ya“International Conservation Caucus Foundation (ICCF) na jamii ya wafanyabiashara kwa kuchangia kuitengeneza program hii. Nawashukuru wabia wetu wa maendeleo mbalimbali, taasisi za fedha zikiwemo Benki ya Dunia kwa kuonesha nia ya kusaidia utekelezaji wa Program ya kuboresha ya Sekta ya Mifugo Tanzania.

Hitimisho

Mabibi na Mabwana,

Mimi naamini tunaweza kufanya vizuri zaidi huko mbele tukitekeleza vizuri mipango na program hii. Mimi naamini siku si nyingi sana, mfugaji na shughuli ya ufugaji itakuwa yenye thamani kubwa na kuheshimika sana hapa nchini. Mimi naamini inawezekana kabisa nasi kuondokana na ufugaji wa kuhama hama na kuingia katika ufugaji wa ranchi za kisasa kama walivyondokana nao wenzetu wengine duniani hasa wa Ulaya na Marekani. Ni ndoto yangu kuona nchi yetu ina wafugaji walionawiri na ng’ombe walionona na sio kama ilivyo sasa ambapo mfugaji amekonda na ng’ombe amekonda. Mpango huu wa Modenaizesheni ninaouzindua leo, ndio barabara ya uhakika ya kutufikisha huko.

Ndugu zangu wafugaji, nafurahi kuwa naondoka nikiwa nimeiacha sekta ya mifugo katika mwelekeo mzuri. Baada ya kusema maneno hayo, kwa furaha napenda sasa kutamka rasmi kuwa “Modenaizesheni ya Sekta ya Mifugo Tanzania”imezinduliwa.

ASANTE KWA KUNISIKILIZA








All the contents on this site are copyrighted ©.