2015-07-23 11:49:00

Kanisa limesikiliza, limeona na kuamua jinsi ya kushughulikia kilio cha maskini


Wajumbe kutoka katika Jumuiya ambazo zinaathirika kutokana na sekta ya madini Barani Afrika, Amerika na Asia, wamehitimisha mkutano wao wa faragha uliohitimishwa na Baraza la Kipapa la haki na amani hivi karibuni hapa mjini Roma. Ni mkutano ambao umeliwezesha Kanisa kusikiliza kilio cha watu wanaoathirika kutokana na uchumbaji wa madini usiozingatia mafao na ustawi wa wengi; kiliocha mauaji, nyanyaso na madhulumu; kilio cha uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji.

Huu ni mkutano ambao pia umewawezesha wajumbe kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki wanaotekeleza dhamana na utume wao miongoni mwa waathirika wa uchimbaji wa madini usiozingatia utu na heshima ya binadamu. Umehudhuriwa na wajumbe wa Caritas na Shirikisho la Kimataifa la Mashirika ya Maendeleo ya Kanisa Katoliki, CIDSE. Wajumbe baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 19 Julai 2015 walipata nafasi ya kuangalia kwa kusikiliza shuhuda zilizotolewa na wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Wamesikiliza na kushirikishana habari zinazopatikana kutoka kwenye migodi na machimbo ya madini na athari zake kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya migodi na machimbo; uhalifu na uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji unaofanywa na makampuni makubwa ya uchimbaji wa madini, kiasi hata cha kutishia usalama na maisha ya wananchi wanaoishi jirani na machimbo haya.

Wamesikiliza jinsi ambavyo wakulima na wafugaji wamelazimika kuyahama makazi na mashamba yao ili kupisha shughuli za uchimbaji wa madini kuendelea. Wameguswa na jinsi ambavyo Makampuni haya yanapata faida kubwa lakini kwa hasara ya uchumi, maendeleo na afya za wananchi husika. Kuna baadhi ya migodi na machimbo ya madini yamekuwa ni chanzo kikuu cha uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji na wale wanaojitokeza kudai haki za wananchi wanashughulikiwa bila utani kana kwamba, ni chuma chakavu!

Hata pale ambapo utafiti umefanywa na kubainisha kwamba, watu wameathirika kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini, bado wananyimwa fidia. Kuna watu wanatekwa na kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa imani za kishirikina na hata wakati mwingine kunyamazishwa ili wasiendelee kuwa ni kero kwa wawekezaji. Kuna baadhi ya mashuhuda wamekiri na kusema kwamba, wametupwa gerezani bila kufunguliwa mashitaka kama njia ya kuwashikisha adabu na kuwafumba midomo.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Kardinali Peter Turkson na kusomwa wakati wa ufunguzi wa mkutano huu wa siku tatu, uligusia kwa kiasi kikubwa kilio hiki cha watu wanaoteseka kutokana na athari za uchimbaji wa madini kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Watu hawa kwa kiasi kikubwa wamesaidiwa na Kanisa pamoja na watu wenye mapenzi mema. Kanisa limeendelea kuwa kweli ni sauti ya wanyonge kwa kufanya kilio cha maskini na wale wanaonyanyaswa, kuteswa na kudhulumiwa ili waweze kuonekana na haki kutendeka. Katika mkutano huu, watu wameshuhudia ujasiri unaooneshwa na wanawake katika kulinda na kutetea heshima ya watu wao, kiasi hata cha kuhatarisha usalama wa maisha yao.

Wajumbe wa mkutano huu, baada ya “kuangalia”, awamu ya pili wamejikita katika mchakato unaowataka “kuamua” dhana inayoambata Mafundisho Jamii ya Kanisa. Wameangalia jinsi ambavyo viongozi wa Kanisa mahalia wanavyoweza kutekeleza dhamana yao kwa kuwa na matumizi bora na sahihi ya ardhi; ushirikishwaji wa matumizi ya rasilimali ardhi. Kanisa la kiulimwengu linagusia kuhusu umuhimu wa kazi, baa la utumwa mamboleo, biashara haramu ya binadamu na umuhimu wa kuhakikisha usalama wa wafanyakazi.

Wajumbe baada ya kuangalia, kuamua, mwishoni wamejiwekea mikakati ya kutenda, yaani kutekeleza mambo msingi yaliyojadiliwa na kupitishwa kwenye mkutano huu, ili uweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Hapa kuna mapendekezo kadhaa yaliyotolewa na wajumbe, ili yaweze kufanyiwa kazi kwa kujikita zaidi na zaidi katika: majiundo; wananchi wafahamishwe sheria, haki na wajibu wao; waelimishwe pale ambapo wanaweza kukata rufaa ili kutetea mafao ya wengi; umuhimu wa kuwaandaa viongozi watakaosimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza haki msingi za binadamu katika maeneo husika.

Jamii ielimishwe umuhimu wa kuthamini na kuendeleza mazingira, nyumba ya wote kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi na kwamba, njia za mawasiliano ya jamii zitumike katika mchakato wa kubadilishana habari. Hapa wajumbe wanalipongeza Kanisa kwa kuwa mstari wa mbele katika kubadilishana nyaraka, ujumbe na mapendekezo hata pale ambapo kulikuwa na hatari kubwa.

Ni matumaini ya Kanisa kwamba, hatimaye, sekta ya madini itaweza kuboreshwa kwa kuwa na sheria zinazolinda haki msingi za binadamu, utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote katika ngazi mbali mbali. Wajumbe wanasema kwamba, ni wajibu na dhamana ya Serikali kuhakikisha kwamba, inatunga sheria zitakazosaidia kudhibiti utunzaji bora wa mazingira, haki msingi za binadamu pamoja na kutunza nidhamu ya makampuni ya wachimba madini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.