2015-07-23 14:37:00

Familia za Kikristo ziwe ni chemchemi na vitalu vya kulelea miito mitakatifu


Familia za Kikristo zinapaswa kuwa ni shule ya utakatifu, haki na amani; chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, utakaowasindikiza watoto kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani kwa njia ya wito wa Kipadre na Kitawa. Wazazi na walezi kamwe wasiwe ni vikwazo na vizingiti vya miito kwa watoto wao, bali wawaoneshe njia, dira na mwelekeo wa kumtumikia Mungu na jirani.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, Alhamisi tarehe 23 Julai 2015 wakati alipokuwa anatoa Daraja Takatifu la Upadre kwa Shemasi Emmanuel Kelvin Tembo wa Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakapuchini. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa la Bikira Maria wa Fatima, Parokia ya Mpwawa, Jimbo Kuu la Dodoma.

Askofu mkuu Kinyaiya anasikitika kusema kwamba, kadiri ya siku zinavyoendelea kuyoyoma, wazazi na walezi wanaonekana kuwa ni vikwazo na vizingiti katika ukuaji na udumifu wa miito ya Kipadre na Kitawa ndani ya Kanisa. Wazazi na walezi wanapaswa kutambua kwamba, familia ni chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa, kumbe wajibu na dhamana yao ya kwanza ni kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mifano bora ya kuigwa katika sala, maadili na utakatifu wa maisha.

Askofu mkuu Kinyaiya anasema, mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache, kumbe ni wajibu na jukumu ya Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma kufunga na kusali, ili kumwomba Bwana wa mavuno aweze kupeleka watenda kazi ambao ni wachapakazi, watakatifu na waadilifu; viongozi ambao wako tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.

Dhamana ya Uinjilishaji ni ya Wakristo wote,lakini Wakleri wanawajibika kwa namna ya pekee kabisa, kumbe, Kanisa linawahitaji Wakleri wengi watakaohamasisha wakristo kutoka kifua mbele, tayari kutangaza Injili ya Furaha kwa watu wa mataifa. Madaraja matakatifu yaliyowekwa na Mama Kanisa ni kusaidia mchakato wa kuwaandaa wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa, wanaopaswa kusindikizwa kwa njia ya sala na majitoleo.

Askofu mkuu Kinyaiya anakaza kusema, Jimbo kuu la Dodoma hadi wakati huu limebahatika kuwa na Majandokasisi 21 kuanzia falsafa hadi taalimungu, hali ambayo haioneshi matumaini makubwa kwa siku za usoni kutokana na ukubwa wa Jimbo kuu la Dodoma na mahitaji ya Familia ya Mungu. Padre Emmanuel Kelvin Tembo ametakiwa kuhakikisha kwamba anaishi kikamilifu wito wake wa Kipadre na Kitawa kwa kumwambata Yesu Kristo, Bwana, Mwalimu na Mchungaji mwema, ili aweze kuwa kweli ni kiongozi, mwema na mtakatifu, mfano bora wa kuigwa na Familia ya Mungu.

Askofu mkuu Kinyaiya anasema, dhamana aliyokabidhiwa Padre Emmanuel Kelvin Tembo ya kuwa ni mhudumu wa Mafumbo ya Kanisa ni changamoto kubwa ya kuhakikisha kwamba, anakuwa na ndoto, sera na mikakati ya kufanikisha azma ya kuwatangazia Watu wa Mungu Habari Njema ya Wokovu na kuwashirikisha Mafumbo ya Kanisa. Kwa njia ya utakatifu wa maisha unaojikita katika maneno na matendo, watu wamfahamu Mwenyezi Mungu na kwa njia yake, hatimaye, waweze kumwona na kushiriki maisha ya uzima wa milele.

Na Rodrick Minja,

Dodoma, Tanzania. 








All the contents on this site are copyrighted ©.