2015-07-23 13:58:00

Benki ya Dunia yaishika mkono Nigeria ili kukoleza maendeleo!


Kutokana na madhara yanayoendelea kusababishwa na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram nchini Nigeria, Benki ya Dunia imeamua kutoa kiasi cha dolla za Kimarekani billioni 2.1 ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa Nigeria, hususan eneo lililoko Kaskazini Mashariki. Hili ni eneo ambalo limeathirika sana kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na kikundi cha Boko Haram kiasi cha kutishia usalama na maisha ya wananchi wengi wa Nigeria.

Makubaliano haya yamefikiwa huko New York Marekani, mara baada ya Rais Muhammadu Buhari kuhitimisha ziara yake ya kikazi nchini Marekani ambako amekutana na kuzungumza na Rais Barack Obama wa Marekani, Shirika la Afya Duniani pamoja na Benki ya Dunia. Rais Obama katika mazungumzo yake, alikaza kusema, Marekani itaendelea kuunga mkono harakati za kupambana na vitendo vya kigaidi, hadi ushindi uweze kupatikana.

Fedha iliyotolewa na Benki ya Dunia inapania pamoja na mambo mengine kusaidia harakati za ujenzi wa miundo mbinu sanjari na kupambana na vitendo vya kigaidi. Boko Haram bado inaendelea kuwa ni tishio kwa usalama, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Nigeria na nchi jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.