2015-07-22 07:29:00

Changamoto zinazoendelea kujitokeza katika sekta ya mawasiliano ya jamii!


Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, hivi karibuni limehitimisha kongamano la kitaifa lililowakusanya waandishi wa habari 500 kutoka sehemu mbali mbali za Brazil ili kwa pamoja kuweza kutafakari kuhusu kanuni maadili katika sekta ya mawasiliano ya jamii. Vijana wengi wameshiriki katika kongamano hili kwani kwa sehemu kubwa wao ndio walengwa.

Askofu Josè Darci Nicioli, Mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil anasema kwamba, kuna changamoto nyingi zinazoendelea kujitokeza katika sekta ya mawasiliano ya jamii, kutokana na ukweli kwamba, sayansi na teknolojia ya mawasiliano imepanuka kiasi cha kuufanya ulimwengu kuwa kama kijiji, jambo ambalo lina: faida na hasara zake hususan miongoni mwa ulimwengu wa vijana wa kizazi kipya.

Kanuni maadili na utu wema usipozingatiwa, njia za mawasiliano ya jamii zinaweza kugeuka kuwa ni janga kubwa katika maisha ya mwanadamu kimaadili, kwani huko vijana wanajifunza mambo mengi, mazuri kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kiroho na kimwili, lakini wakati mwingine wanachota “takataka na sumu” ya maisha ya: kiroho, kimwili, kimaadili na kiutu. Njia za mawasiliano ya jamii hazina budi kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kamwe zisitumiwe na wajanja wachache kwa ajili ya kujitafutia masilahi na faida binafsi.

Wakati mwingine, njia za mawasiliano zimetumika kuhudumia sera na siasa za makundi ya watu ndani ya jamii. Yote haya yanaifanya Jumuiya ya Kimataifa kuwa makini zaidi na kwa Kanisa kwa upande wake, linapaswa kutangaza kweli za Kiinjili zinazomwambata Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Njia za mawasiliano kwa upande wa Kanisa zinalenga kulisaidia Kanisa katika mchakato wa utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu, ili watu kweli waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya Familia ya Mungu inayowajibika.

Hii ni changamoto kwa Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushuhudia kweli hizi katika hija ya maisha yao ya kila siku. Kanisa linapaswa kutenda na kushuhudia nguvu ya Roho Mtakatifu inayoliongoza katika maisha na utume wake. Katika kongamano hili la kitaifa, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa ni kielelezo na mfano wa rejea katika mawasiliano yanayopania si kujitangaza wala kujitafutia ujiko, bali kushuhudia ile nguvu ya upendo wa Kristo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kuonesha kwa matendo nguvu ya kimaadili inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa anapotangaza kweli za Kiinjili.

Baba Mtakatifu ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa upendo ndani ya Kanisa na kwa njia yake, Familia ya Mungu inachangamotishwa kutoka kimasomaso kwa ajili ya kumshuhudia Kristo, ili aweze kufahamika, kupendwa na kutumikiwa na wengi zaidi.

Kwa upande wake, Padre Rafael Vieira, mjumbe wa Tume ya Mawasiliano, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil anakaza kusema, kongamano hili limekuwa ni fursa ya kushirikishana kanuni maadili na utu wema, ili kuweza kuitenda kazi hii kwa ari na moyo mkuu, daima kwa kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Brazil kama zilivyo nchi nyingine duniani inahitaji kuwa na dira na mwanga thabiti unaojikita katika kanuni maadili na utu wema mintarafu masuala ya mawasiliano ya kijamii. Kanuni maadili zinazopaswa kutekelezwa na mtu mmoja mmoja katika jamii, wafanyakazi, serikali na wote ambao wana wajibu wa mbele ya jamii.

Wanahabari Wakristo kwa kushirikiana na watu wenye mapenzi mema, wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda wa ukweli, uwazi na kanuni maadili katika masuala ya mawasiliano ya jamii. Wawe ni watu wanaongozwa na dhamiri nyofu wakati wote wanapotekeleza dhamana na wajibu wao katika jamii inayowazunguka. Vijana wameshiriki kwa wingi katika kongamano hili la kitaifa na wamejifunza walau kanuni maadili zinazopaswa kuwa kweli ni dira na mwongozo katika matumizi ya njia za mawasiliano ya kijamii, ili ziweze kuwasaidia katika ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili.

Itakumbukwa kwamba, Kanisa ni chombo cha matumaini kwa vijana na kwamba, njia za mawasiliano ya kijamii zinapania pamoja na mambo mengine kuwasaidia vijana kuwa na imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Vijana wanao wajibu mkubwa mbele yao, kumbe wanapaswa kufikiri na kutenda kwa kuzingatia kanuni maadili, ukweli, ustawi na mafao ya wengi, mambo msingi kwa ajili ya ustawi wa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuwatangazia watu Injili ya Furaha na kweli za Kiinjili zinazofumbatwa katika uzuri na utakatifu wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.