2015-07-21 14:06:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 17 ya Mwaka B wa Kanisa: Ekaristi


Mpendwa mwana wa Mungu, tunasonga mbele na Tafakari Neno la Mungu katika Dominika ya XVII ya mwaka B wa Kanisa. Neno la Mungu latupa ujumbe mzito unaohusu uwezo wa Mungu. Kwa uwezo wake Mungu anafanya yasiyowezekana machoni pa watu yawezekane. Anawalisha watu 5,000 kwa mikate mitano na samaki viwili. Mitume wanamashaka namna gani Bwana ataweza kuwatosheleza watu wengi namna hii. Mashaka haya yanatuonesha kuwa hawajaelewa bado kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.

Katika somo la kwanza kutoka katika kitabu cha II cha Wafalme tunaona tendo la ukarimu linalotendwa na mtu mmoja kutoka Baalishalisha. Anampa Nabii Elisha kiasi cha chakula, yaani mikate 20 na masuke ya ngano kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya njaa iliyokuwepo wakati huo katika Israeli. Kwa kiasi hiki cha chakula Nabii Elisha atawalisha mamia ya watu na kitaweza kubaki. Huu ni mwujiza kati ya miujiza ambayo Nabii Elisha anaifanya katika Agano la kale.

Nini maana ya jambo hili? Ni kwamba mwandishi ataka kutufundisha juu ya uwezo wa Mungu usiopimika na hivi yeyote amtegemeaye Mungu hatapungukiwa na kitu wakati wa taabu na njaa. Kwa ujumbe huu tunaalikwa kuweka maisha yetu mikononi mwa Mungu, kuwa na imani thabiti katika yeye, tukikumbuka kuwa imani kidogo tu yaweza kuhamisha milima. Pili ujumbe huu watuleta moja kwa moja katika Agano jipya ambapo tunakutana na Ekaristi Takatifu, mkate usioisha, mkate wa uzima wa milele, chakula kilichoshuka kutoka mbinguni.

Katika somo la Pili, Mtume Paulo anapowaandikia Waefeso anawaalika kuwa wanyenyekevu na wapole, wakichukuliana kwa upendo na msamaha na hivi kwa namna hiyo kujenga umoja kamili katika Roho Mtakatifu mwalimu wa mapendo. Hii ni tabia ya maisha mapya tuyapatayo kwa njia ya ubatizo, mwaliko ukiwa ni kuwahudumia wengine. Tokana na tabia hii ya maisha mapya  basi wote watakuwa mwili mmoja na roho moja katika Kristo kwa njia ya ubatizo mmoja. Katika kujenga umoja ndiko kuna uwezekano wa kutenda miujiza kama alivyofanya Nabii Elisha, aliyejiimarisha katika umoja na Mungu wake.

Katika Injili, Mwinjili Yohane anatualika kuendelea kutafakari uwezo wa Mungu katika maisha yetu. Tunamwona Bwana yuko Tiberia, bahari ya Galilaya na huko watu wengi wanamfuata kwa sababu ya ishara mbalimbali alizozitenda na hasa kwa kuwaponya wagonjwa. Bwana yuko huko na siku za Pasaka zinakaribia na hivi yatupasa kukumbuka kuwa Wayahudi karibu wanaadhimisha kukombolewa kwao toka Misri. Watu wanamfuata kama ambavyo Wayahudi walikuwa wakimfuata Musa katika safari yao toka utumwani. Jambo hili linatupa tayari picha yakuwa Bwana ni Mkombozi wetu toka utumwa wa njaa, dhambi na mambo mengine kama hayo.

Mpendwa, ni kwa namna gani wazo hilo la ukombozi linatufikia? Wazo hili linatufikia kwa njia ya mwujiza wa kuwalisha watu 5,000 kwa mikate mitano na samaki wawili?. Mitume wanamwambia Bwana awaambie watu waende vijijini wakatafute chakula wao wenyewe, haya ni mawazo ya ubinafsi ambayo yako ndani ya Mitume, lakini badala yake Bwana anawaambia waketisheni watu na wapeni chakula, haya ni mawazo ya umoja na mshikamano toka kwa Bwana ambayo ndiyo Mtume Paulo anatufundisha katika somo la pili akiyachota toka kwa Bwana.

Mitume walikuwa katika mawazo ya ubinafsi, je sisi twaweza kuanguka katika shida gani? Ni kweli twaweza kuanguka katika shida ya kumwona Bwana kama mfalme mwenye nguvu, mabavu na si mfalme wa amani. Twaweza kuzama katika ubinafsi uliolala katika kujipendelea na hivi katika uchakachuaji wa kila hali ili mradi mambo yangu yafanikiwe.

Mpendwa tendo la kuwalisha watu 5,000 mikate na samaki wachache laonesha uwezo wa Mungu kama ulivyojionesha katika Agano la Kale. Katika tukio la kuwalisha watu kuna viambata mbalimbali ambavyo vyatusaidia kuelewa vema Injili ya Bwana. Mikate na samaki vilitolewa na mtoto mdogo, Mwinjili akilenga kutukumbusha wajibu wa kuwa kama watoto wadogo kwa ajili ya kuurithi uzima wa milele.

Tendo la kutolewa mikate na mtoto pia latupa picha ya kujitoa kwa kila mmoja wetu, yaani ni lazima kushirikisha vipaji vyetu tulivyonavyo kwa ajili ya wengine na hapa ndipo tunajenga familia mwili mmoja na roho moja katika Kristu. Mpendwa watu walioketishwa wakala na kusaza, ni kiashilio na alama nzito juu ya uwezo na upendo wa Mungu usioisha, usio na mipaka na ulio kwa ajili ya wote. Twaweza kusema pia, Kristo ni mkate usioisha na hivi toka mawio hata machweo katika Bwana tutakula na kushiba na kusaza mpaka mwisho wa nyakati.

Kumbuka Injili ya Matayo 28:18-20, niko pamoja nanyi mpaka ukamilifu wa dahari. Hata hivyo ili tuweze kushiriki vema mkate wa milele lazima tujipange vema, yaani mapendo katika jumuiya, kwa Mungu na imani dumifu katika Bwana wetu Yesu Kristo.

Mpendwa unayenisikiliza Bwana ni Hostia safi isiyo na doa, mkate wa mbinguni ulio kwa ajili ya wokovu wa wote, chakula kisichoisha milele na milele, Amina. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.