2015-07-21 08:45:00

Kanisa nchini Zambia linajipambanua kwa huduma makini kwa Familia ya Mungu!


Askofu mkuu Telesphore George Mpundu, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, hivi karibuni amesikika akikaza kusema, Kanisa Katoliki nchini Zambia, litaendelea kushikamana na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama sehemu ya maisha na utume wake unaojikita katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Askofu mkuu Mpundu ameyasema hayo, wakati alipokuwa anazungumza kwenye Hospitali ya Kumbu kumbu ya Kardinali Adam iliyoko Jimbo kuu la Lusaka, Zambia. Hii ni hospitali ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kumbu kumbu ya Kardinali Adam Kozlowieck, Kardinali wa kwanza kutangazwa na Kanisa nchini Zambia. Hospitali hii inaendelea kutoa huduma makini kwa wagonjwa nchini Zambia.

Askofu mkuu Mpundu anasema, Kanisa linashirikiana bega kwa bega na Wizara ya Afya nchini Zambia kwa ajili ya kutoa huduma katika sekta ya afya, kwa gharama wanayoweza kumudu wananchi wengi wa Zambia. Serikali ya Zambia inalishuruku na kulipongeza Kanisa Katoliki kwa kuchangia walau asilimia 60% ya huduma ya afya nchini Zambia, hususan kwenye maeneo ya vijijini ambako hata Serikali haijafaulu kufika.

Kanisa liko mstari wa mbele katika huduma na ustawi wa jamii nchini Zambia, utume unaotekelezwa kwa njia ya mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki kwa kushirikiana na wadau mbali mbali ndani na nje ya Zambia. Hospitali ya taifa ya Bauleni, imekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, kwa kusaidia kutoa dawa za kurefusha maisha pamoja na kudhibiti maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto mchanga wakati wa kuzaliwa.

Kuna zaidi ya vituo 200 vya afya vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Zambia kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, wazee na watoto yatima. Huu ni mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaopania kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.