2015-07-21 08:22:00

Fanyeni ekolojia ya toba inayojikita katika mwono wa familia ya binadamu!


Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuusoma na kuutafakari Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” kama sehemu ya majiundo makini ya tasahufi ya Kikristo inayohusu utimilifu wa ekolojia ya mwanadamu.

Anasema, kuna watu wanaozaliwa na kukulia katika maeneo machafu yanayohatarisha maisha yao; wengine wanakumbana na majanga asilia ya ukame wa kutisha au mafuriko; mambo ambayo yanaendelea kusababisha ukosefu wa haki msingi za binadamu, lakini ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu aliumba dunia inayopendeza kwa ajili ya matumizi ya binadamu, lakini mwanadamu amekuwa ni chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira kutokana na ulaji wa kupindukia unaohataarisha maisha ya mtu: kiroho na kimwili, changamoto kwa binadamu kuanza mchakato unaomwajibisha katika utunzaji bora wa mazingira.

Baba Mtakatifu Francisko katika waraka wake wa kitume juu ya utunzaji bora wa mazingira anafafanua kwa kina na mapana mahusiano yaliyopo kati ya Mwenyezi Mungu na familia ya binadamu na kwamba, binadamu amepewa dhamana ya kutunza mazingira kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo yake kwa wakati huu na kwa ajili ya kizazi kijacho, ili kujenga na kudumisha Familia ya binadamu inayojikita katika utu na umoja. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kufanya ekolojia ya toba inayojikita katika mwono wa Familia ya binadamu, inayotunza mazingira.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufanya mabadiliko makubwa katika mtindo wa maisha  kwa kutoa sadaka; kwa kuondokana na uchoyo na badala yake kujenga moyo wa ukarimu; badala ya kutupa chakula, kuguswa na mahangaiko ya wengine kwa kushirikiana nao. Lengo ni kuondokana na tabia ya kutojali shida na mahangaiko ya wengine, ili kuanza mchakato wa majadiliano katika familia ya binadamu unaojikita katika dhana ya kutambua kwamba, binadamu amekabidhiwa kutunza na wala si mmiliki wa kazi ya uumbaji sanjari na kusikilizana kwa makini na katika ukweli. Hii ni fursa ya kuchunguza dhamiri kwa kuangalia mafanikio na mapungufu, ili kufanya marekebisho yanayokusudiwa.

Kardinali Tagle anakaza kusema, ndani ya Caritas Internationalis ameshuhudia nguvu ya upendo inayomwilishwa ili kukabiliana na changamoto za kiulimwengu; kwa kujikita katika mshikamano na watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; ili kuwasaidia watu kutambua utu na hesima yao kama binadamu. Caritas sehemu mbali mbali za dunia imeshiriki katika ujenzi wa makazi bora ya watu na kuwasaidia watoto kwenda shule ili kujipatia elimu ambayo ni mkombozi wa maisha. Kwa hakika, Caritas ni Neno hai la Mungu linalomwilishwa miongoni mwa maskini kama chemchemi ya upendo na matumaini yanayokusudia kuleta mabadiliko makubwa katika maisha. 

Caritas haina budi pia kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kufanya mabadiliko yanayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika katika Waraka wake wa kichungaji juu ya utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote. Hapa kuna haja ya kuunganisha: rasilimali, kushirikishana habari na kusaidiana, ili kuwa na matumaini ya pamoja.

Kardinali Tagle anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuleta mageuzi katika maisha, kwa njia ya toba na wongofu wa mtu binafsi, sanjari na kusaidia ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kuwafikia watu wengi zaidi, hasa maskini wanaoteseka kwa uharibifu wa mazingira uliofanywa na watu wengine. Ujumbe huu uwafikie wanasiasa na watunga sera ambao wana uwezo wa kufanya maamuzi katika maisha ya watu, ili kweli waweze kuwajibika barabara.

Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu kuhusu utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote ni ushuhuda kwamba, Kanisa kwa miaka mingi limekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira, lakini kwa sasa waamini wanaalikwa kuumwilisha ujumbe huu katika maisha na vipaumbele vyao kuwa ni sehemu ya tasaufi ya utimilifu wa ekolojia ya binadamu, ili kuangalia na kuthamini uzuri unaofumbatwa katika kazi ya uumbaji.

Waamini wanapaswa kupyaisha tasaufi yao ya maisha ya kiroho kwa kuwaalika wasomi, watunga sera, walimu, wasanii na wanasayansi kushikamana kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi; kuheshimu na kuthamini utu wa binadamu, hususan maskini na wasiokuwa na sauti. Upendo wa Mungu unaendelea kujionesha kwa namna ya pekee katika kazi ya uumbaji, changamoto ya kushikamana na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.