2015-07-21 10:24:00

Changamoto za maisha ya ndoa na familia kutoka Afrika zimesahauliwa!


Familia ni madhabahu ya Injili ya maisha na chembe hai ya jamii na Kanisa na mahali ambapo mwanadamu analelewa na kufundwa mambo msingi katika maisha: kupenda, kuheshimiwa, kuthaminiwa. Ni mahali pa kukuza na kudumisha utamaduni wa haki, amani na upatanisho. Ni mahali pa kuinjilisha na kujiinjilisha kwa njia ya ushuhuda wa Injili ya Familia inayoambata Injili ya uhai na kwamba, familia ni kielelezo na chemchemi ya maisha ya kiroho.

Ndani ya familia, watu hujifunza utulivu, maisha na dhamana ya kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Haya yote ni mambo msingi ambayo Familia ya Mungu Barani Afrika inapaswa kuyazingatia, wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, itakayoanza kutimua vumbi hapo tarehe 4 Oktoba hadi 25 Oktoba 2015 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo”.

Umaskini na janga la ukimwi ni kati ya changamoto kubwa zinazoendelea kuzikabili familia nyingi Barani Afrika. Mababa wa Sinodi ya kwanza ya Maaskofu wa Afrika walikazia umuhimu wa kujenga na kudumisha urafiki, uaminifu na udumifu; kwa kujikita katika maadili na utu wema. Ni changamoto ya kubadili tabia. Ukimwi ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi kwa kushirikiana na madaktari; malezi ya kijinsia, sheria asili, Neno la Mungu na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Lengo ni kushuhudia Injili ya Familia inayoambata Injili ya uhai.

Wasomi na wanazuoni wa Kikatoliki katika kongamano lililofanyika hivi karibuni Jijini Nairobi ili kujadili, fursa, matatizo na changamoto zinazozikabili familia Barani Afrika wanasema, janga la Ukimwi halikutajwa katika Hati ya kutendea kazi ya Maaskofu wakati wa Sinodi ya Familia, ingawa ni changamoto kubwa sana Barani Afrika. Ukeketaji na watoto kubebeshwa majukumu makubwa ya kifamilia kutokana na athari za magonjwa ya milipuko ni mambo ambayo hayakuangaliwa wakati wa kuandaa nyaraka mbali mbali kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia. Hii inatokana na ukweli kwamba, wawakilishi kutoka Afrika pengine hawakuayaona masuala haya kuwa ni sehemu ya matatizo na changamoto kubwa kwa utume wa familia Barani Afrika.

Askofu Kevin Dowling wa Jimbo Katoliki Rustenburg, Afrika ya Kusini alichambua kwa kina na mapana Injili ya Familia Barani Afrika, ili kuwasaidia waamini kuwa na sauti moja, ili hatimaye, waweze kusimama imara kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya Familia wakiwa na sauti moja kama alivyokaza kusema Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na nidhamu ya Sakramenti za Kanisa, aliyewataka wajumbe wa SECAM kuliwakilisha Bara la Afrika wakiwa na sauti moja.

Mwelekeo wa sasa wa familia unaonekana kana kwamba, unataka kumezwa na mwono tenge wa familia kutoka Barani Ulaya na Marekani kwa kujikita katika mahusiano kati ya watu na jamii. Ubinafsi na mielekeo tenge ya maisha ya ndoa na familia bado inajitokeza kwa kiasi kikubwa, kiasi cha kutishia ustawi na maendeleo ya Injili ya familia.

Familia Barani Afrika haina budi kujengeka katika msingi wa mahusiano bora kati ya watu yanayo imarisha jamii na kuwakumbatia wote kama kielelezo cha ukarimu na majitoleo. Ni wajibu wa wawakilishi wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM kusaidia kutoa picha na mwelekeo sahihi kuhusu: maisha, tunu, wito na utakatifu wa ndoa za Kikristo. Familia ya Mungu Barani Afrika inakumbushwa kwamba, athari za utandawazi na kumong’onyoka kwa maadili na utu wema zinaanza pia kutikisha misingi ya maisha ya ndoa na familia, kiasi cha kuona baadhi ya wanasiasa na wananchi katika ujumla wao wakishabikia ndoa za watu wa jinsia moja eti kuwa ni kielelezo cha uhuru wa mtu na haki msingi za binadamu.

Padre Agbonkhianmeghe Orobator kutoka kutoka Chuo kikuu cha Hekima, Nairobi anasema, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican unapaswa kuangaliwa kama mchakato wa maisha na utume wa Kanisa na wala si kama tukio linalojikita katika historia na wakati. Mchakato wa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Vatican unaendelea kusonga mbele, ili kumwilisha maazimio yaliyobainishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, miaka hamsini iliyopita. Wajumbe waliokuwa wanahudhuria mkutano huu wa siku tatu, wamepongeza mchango uliotolewa na wawezeshaji wakuu kiasi cha kupanua mawazo ya wajumbe katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CANAA.








All the contents on this site are copyrighted ©.