2015-07-21 07:41:00

Balozi za Marekani na Cuba zafunguliwa rasmi


Baada ya miaka hamsini kupita, Serikali ya Marekani na Cuba zimeanzisha tena mahusiano ya kidiplomasia kwa balozi za nchi hizi mbili kupeperusha bendera za mataifa yao, tukio ambalo linahitimisha rasmi vita baridi iliyosababisha madhara makubwa kwa ustawi na maendeleo ya watu. Tukio hili la kihistoria limehudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi wa Marekani na Cuba.

Balozi Bruno Rodrìguez ndiye aliyekuwa balozi wa kwanza wa Cuba kutembelea Marekani kunako mwaka 1959, ameshiriki tukio hili kuwakumbusha walimwengu mahali walipotoka. Marekani imewakilishwa na Balozi Roberta Jacoboson, mwakilishi wa Marekani Amerika ya Kusini.

Tukio hili la kihistoria la kurejesha tena mahusiano kati ya Marekani na Cuba lilitangazwa kunako tarehe 17 Desemba 2014 kati ya Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Raul Castro wa Cuba. Tangu wakati huo, mchakato wa kurejesha tena mahusiano baina ya nchi hizi mbili ukaanza, ingawa bado kuna kasoro zinazopaswa kufanyiwa kazi, ili kuleta matunda yanayokusudiwa na pande hizi mbili. Hii ni hatua ya kwanza ya kurejesha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Marekani na Cuba anasema Rais Castro.

Awamu ya pili ya mahusiano ya kidiplomasia itajikita zaidi katika masuala ya usafiri wa anga; utunzaji bora wa mazingira, mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara na ushirikiano wa kiuchumi. Bado kuna haja ya kuboresha uhuru wa watu kujieleza; uhuru wa kuabudu pamoja na uhuru wa vyombo vya habari, mambo ambayo yanapewa kipaumbele cha pekee na Serikali ya Marekani. Wananchi wa Marekani wanadai kiasi cha dolla za kimarekani billioni nane, baada ya Serikali ya Kikomunisti kutaifisha mali yao kunako mwaka 1959.

Vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba kunako mwaka 1962 ni kati ya changamoto kubwa zinazomkabili Rais Barack Obama wa Marekani katika mchakato wa kurejesha tena mahusiano ya Kidiplomasia kati ya Marekani na Cuba. Rais Raul anakaza kusema, kufutwa kwa vikwazo vya kiuchumi ni hatua kubwa na ya muhimu sana katika mchakato wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Cuba na Marekani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.