2015-07-20 13:41:00

Nafasi ya Wakleri na Watawa iko miongoni mwa maskini!


Baba Mtakatifu Francisko wakati akiwa nchini Bolivia, alikutana na wakleri, watawa na majandokasisi katika shule ya Wasalesiani wa Don Bosco. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu aliwataka watawa kuhakikisha kwamba, wanaimarisha tasaufi ya maisha yao ya kuwekwa wakfu; tayari kutoka kimasomaso ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wawe ni wahudumu mahiri wa Injili ya furaha na kamwe wasitekeleze dhamana na wajibu huu kwa shingo upande.

Kwa upande wake, Askofu msaidizi Roberto Bordi, Mwenyekiti wa Idara ya Wakleri na Watawa, Baraza la Maaskofu Katoliki Bolivia anakaza kusema, wao nafasi yao iko kati ya waamini, lakini zaidi miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wakleri na watawa wanapenda kujisadaka kwa ajili ya kumhudumia binadamu: kiroho na kimwili pamoja na kuendelea kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati.

Askofu msaidizi Roberto Bordi amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Wakleri, Watawa na Majandokasisi wako kila pembeĀ  ya maisha ya mwanadamu: mijini na vijijini; wakitekeleza dhamana na utume wao kama Wamissionari wanaotumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao unaojikita katika huduma makini kwenye sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Huko ndiko wanakotekeleza dhamana ya kuwasindikiza watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Hii ni dhamana endelevu inayojikita katika utekelezaji wa maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa na Mwaka wa Watawa Duniani. Mikakati yote hii imebainishwa vyema katika utume wa Familia, unaopania kuzijengea uwezo familia ili ziweze kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya Familia inayojikita katika Injili ya Uhai; utume kwa vijana pamoja na kuhamasisha miito mitakatifu kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani.

Wakleri na watawa wanaendelea kutekeleza utume wao miongoni mwa Familia ya Mungu nchini Bolivia kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaokwenda sanjari na huduma msingi zinazotolewa na Mama Kanisa katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Wakati mwingine, Wakleri na Watawa wanatindikiwa nguvu na rasilimali fedha na vitu katika mchakato wa utekelezaji wa dhamana na majukumu yao miongoni mwa familia ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.