2015-07-20 10:45:00

Mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa katika kupambana na magonjwa ya mlipuko!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jopo ya Watu Mashuhuri Duniani wanaotafuta njia za kuiwezesha dunia kujiandaa vizuri kwa majanga ya magonjwa ya kuambukiza , Ijumaa, Julai 17, 2015, amemaliza mikutano ya raundi ya pili ya Jopo hilo mjini Geneva, Uswis. Rais Kikwete na Wanajopo wenzake wamemaliza raundi ya pili ya mikutano ya Jopo hilo kwa kukutana na mabingwa magwiji ambao wengi wao wamo na wamekuwemo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola.

Katika miezi mitatu ya mwaka 2014, ugonjwa huo uliua watu 11,000 katika nchi za Afrika Magharibi za Guinea, Liberia na Sierra Leone. Mabingwa hao waliokutana na Jopo hilo kwenye Makao Makuu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ni kutoka Kamisheni ya Ulaya, Shirika la EPRUS la Ufaransa, Shirika la Kujihami la Nchi za Ulaya Magharibu la NATO, Shirika la GOAR la WHO, Shirika la Chakula Duniani (WFP), Shirika la Umoja wa Mataifa la OCHA na wajumbe kutoka nchi za Marekani na Uingereza.

Kwa zaidi ya saa mbili, Rais Kikwete na wanajopo wenzake, wamesikiliza maelezo ya wataalam hao ambao kwa pamoja walihusika na mapambano dhidi ya Ebola, ugonjwa ambao umeanza kuibuka upya katika nchi hizo tatu za Afrika Magharibi.  Jopo la Rais Kikwete halichunguzi ugonjwa wa Ebola na madhara yake, lakini wajumbe hao waliombwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Mheshimiwa Ban Ki Moon, wakati anawateua Aprili 2, mwaka huu, kutumia uzoefu wa dunia katika kukabiliana na ugonjwa huo kutoa mapendekezo yao.

Baada ya kuwasikiliza wataalam hao, wajumbe wa Jopo wamekubaliana kuwa vikao vyao vijavyo vitafanyika katika nchi zilizoathiriwa na Ebola za Guinea, Liberia na Sierra Leone mwanzoni mwa mwezi ujao. Aidha, baada ya kumalizika kwa mkutanao wa Jopo, Rais Kikwete amekutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Bi. Margaret Chan kwenye makao makuu ya shirika hilo.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka Watanzania wanaofanya kazi katika mashirika ya kimataifa nje ya nchi kuwasaidia Watanzania wenzao wenye sifa na uwezo kuweza kujiunga na mashirika hayo ya kimataifa. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali haiwadai chochote Watanzania wanaoishi nje na kufanya kazi nje ya nchi bali kuweza kuisaidia nchi yao na ndugu zao pale inapopatikana nafasi. Rais Kikwete aliyasema hayo usiku wa Alhamisi, Julai 16, 2015, wakati alipokutana na kuzungumza na Watanzania wanaoishi katika Uswisi chini ya chama chao cha TAAS – Tanzania Association in Switzerland kwenye Hoteli ya Intercontinental, mjini Geneva.

“Saidieni ndugu zenu nyumbani, lakini pia saidieni wenzenu wenye sifa ya kuweza kupata kazi katika mashirika ya kimataifa. Wenzetu katika nchi nyingi za Afrika, hasa Afrika Magharibi wanafanya hivyo, ndio maana wamejaa katika mashirika hayo ya kimataifa. Sisi tuna haya na hatufanyi hivyo,” alisema Rais Kikwete.

Kuhusu matarajio ya Serikali kwa Watanzania wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake haiwadai chochote.  “Sisi hatuwadai chochote. Nyie endeleeni kufanya kazi nje na kujenga maisha yenu, kazi ya maendeleo ya nchi mtuachie sisi, tunaiweza. Ushauri wangu ni wasaidieni ndugu zenu nyumbani. Dola 100 ya Marekani kila mwezi zina uwezo wa kusomesha mtoto shule.” Baada ya mazungumzo na Watanzania hao, Rais Kikwete aliwafuturisha Watanzania hao ikiwa ni futari ya mwisho kwa Rais Kikwete na Watanzania, akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Na mwandishi maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.