2015-07-20 09:24:00

Kanisa ni kwa ajili ya maskini pamoja na maskini katika azma ya Uinjilishaji


Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Yangon, lililoko nchini Mynmar, anasema Kanisa Katoliki nchini humo hivi karibuni, limeadhimisha Jubilee ya Miaka 500 ya Ukristo, changamoto kwa Mama Kanisa kuendelea kusimama kidete kuwahudumia, kuwalinda na kuwatetea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ni dhamana na wajibu wa Kanisa kujifunga kibwebwe kutetea utu na heshima ya binadamu pamoja na kujielekeza kutafuta mafao na maendeleo ya wengi. Kanisa linapaswa kuwa ni kwa ajili ya maskini pamoja na maskini, kwani hawa ni amana na chachu ya Uinjilishaji mpya, watu ambao hata katika unyonge wao wanaweza kukumbatia, kushuhudia na kumwilisha imani katika matendo.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Maung Bo ni kati ya Makardinali walioteuliwa na hatimaye kusimikwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko ambaye analihamasisha Kanisa kujielekeza zaidi pembezoni mwa jamii, ili kuwaonjesha Watu wa Mataifa Injili ya Furaha na Matumaini, inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Kardinali Maung Bo ndiye Kardinali wa kwanza baada ya miaka 500 ya Ukristo nchini Mynmar.

Katika kipindi chote hiki, Kanisa limepitia katika hali ngumu ya maisha na wengi wanaona kuwa kweli huu ni muujiza wa uwepo endelevu wa Yesu Kristo kati ya waja wake wakati wa raha na mahangaiko, jambo la msingi ni kutokata tamaa kutokana na madhulumu na nyanyaso ambazo pengine Wakristo wanakutana nazo katika maisha yao kama ilivyo kwa sasa huko Mashariki ya Kati au Nigeria.

Wakristo nchini Mynmar wanaunda idadi ndogo sana ya wananchi wote, lakini ni kundi ambalo limekuwa na mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Mynmar katika sekta mbali mbali za maisha, hususan katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Kanisa linaendelea kujielekeza katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kitamaduni na kisiasa, ili kweli utu na heshima ya binadamu, mafao na ustawi wa wengi vipewe msukumo wa pekee katika sera na mikakati ya kitaifa.

Kanisa linaendelea kujitamadunisha na kutamadunishwa na tunu msingi za ma kabila mbali mbali nchini Mynmar pamoja na kujikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha haki na amani kwa kushirikiana na waamini wa dini mbali mbali nchini humo. Wananchi wengi wanakabiliwa na umaskini wa hali na kipato, kiasi kwamba, wananchi wengi wanaweza kujikuta wakitumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Umaskini nchini Mynamar ni janga la watu kujitakia wenyewe kwa kutafuta haki msingi kwa njia ya fujo na vurugu. Kanisa kwa kushirikiana na wadau wengine halina budi kujifunga kibwebwe kutetea haki jamii, ili kungo’a vizingiti vinavyokwamisha ustawi na maendeleo ya wananchi wengi. Amani itaendelea kuwa ni kitendawili nchini humo anasema Kardinali Maung Bo, hadi pale umaskini wa watu utakapopatia tiba ya mwarobaini na hatimaye, kupewa kisogo, kwa njia ya elimu makini, huduma bora za afya na majiundo endelevu kwa vijana wa kizazi kipya.

Hapa Serikali inapaswa kuliangalia Kanisa kama mdau mwenza katika mchakato wa maboresho ya huduma za kijamii na wala si kama adui anayepaswa kushikishwa adabu. Ili kupata amani ya kudumu na endelevu, Kanisa halina budi kushiriki kikamilifu kwani hii ni sehemu ya utume na dhamana yake kwa Watu wa Mataifa.

Kardinali Charles Maung Bo, ambaye ni Mtawa wa Shirika la Wasalesiani anasema kwamba, nchini mwake kuna watawa zaidi ya 2500 wanaotekeleza utume wao miongoni mwa Familia ya Mungu nchini Mynmar. Ni kundi linalojisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, hususan katika sekta ya elimu na afya.

Baba Mtakatifu Francisko analihamasisha Kanisa kusonga mbele kwa imani na matumaini, kwa kutoka kifua mbele ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha, Matumaini na Uhai, tayari kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Kanisa linaendelea kuongezeka kwa idadi ya waamini pamoja na ubora unaojionesha katika ushuhuda wa maisha, kwani waamini wanafundwa na kufundikwa.

Hili ni Kanisa anasema Kardinali Charles Maung Bo kwa ajili ya maskini pamoja na maskini, kwani maskini wako mstari wa mbele kusaidiana katika safari ya maisha kwa njia ya mshikamano wa udugu na upendo. Huu ni utume unaotekelezwa na Jeshi la Makatekista lenye watu zaidi ya 300 wanaohudumia wahamiaji, wageni na watu wasiokuwa na makazi maalum, ili wote hawa waweze kuonja ile Furaha ya Injili. Kanisa nchini Mynmar linaendelea kujielekeza katika mchakato wa Uinjilishaji kwa mihimili ya Uinjilishaji, ili wale watakaoinjilishwa waweze kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji kwa watu wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.