2015-07-18 15:20:00

Watu wanahitaji kuona imani inayomwilishwa katika matendo!


Hati ya Kanisa “Africae Munus” iliyotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI baada ya Sinodi maalumu ya Pili ya Bara la Afrika inalialika Kanisa la Afrika kuifanya sauti ya Kristo kusikika katika ulimwengu. Huo ni wajibu wa kuwafanya wakristo kuwa wakristo kweli, yaani, kuishuhudia kwa matendo imani wanayoikiri na kufundishwa. Wanapaswa kuweka muunganiko sawia katika ya maisha ya imani na uelewa wa imani. Kwa utangulizi huu mfupi napenda kukualika katika tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 16 ya mwaka B wa Kanisa.

Katika somo la kwanza yanajitokeza mambo mawili muhimu ya kutafakari. Kwanza tunapatiwa picha ya wachungaji ambao hawatimizi wajibu wao. Matokeo ya uzembe huu ni uharibifu na kulitawanya kundi. Wachungaji hawa wamewafukuza na pia hawakulijali kundi walilokabidhiwa. Kondoo ni mnyama mpole ambaye anahitaji uongozi na matunzo ya dhati; ni mnyama ambaye anakuwa katika hali ya kuzubaa wakati wote na hivyo anahitaji mchungaji atakayemhimiza na kumhamasisha aende mbele; na mwisho ni mnyama mkimya ambaye pasipo uangalifu hata anapovamiwa ni rahisi kuteketezwa na maadui zake. Mchungaji asiyejali kondoo ni maangamizo na balaa kubwa kwa viumbe hawa.

Sisi wanadamu tunafananishwa na Kondoo machoni mwa mwenyezi Mungu. Bila ulinzi na uangalizi wa Mungu tunabaki katika maangaiko na kupoteza matumani. Mwenyezi Mungu anamweka mwanadamu kuwa mjumbe wake wa kuufanya uwepo wake kusikika kwa wote. Hii inamaanisha kwamba pamoja na uhitaji wetu na uwepo thabiti na wa kudumu wa wema na upendo wa Mungu sisi nasi tunafanywa kuwa vyombo vya kuueneza wema wa Mungu. Mzaburi anapotuambia “Mimi nikutazame uso wako katika haki, niamkapo nishibishwe kwa sura yako”;  anataka kuonesha hamu hiyo ya mwanadamu ya kukirimiwa daima na wema na upendo wa Mungu. Wema na uzuri huo wa Mungu tumekirimiwa kupitia karama na vipawa mbalimbali ambavyo Mungu mwenyewe anampatia mwanadamu. Hivyo ni katika huduma zetu za kindugu ambapo tunatimiza jukumu la uchungaji ambalo mwenyezi Mungu anatuaminisha katika mabega yetu.

Jambo la pili tunalotafakari katika sehemu hiyo ya Neno la Mungu ni juu ya umilele wa wema na upendo wa Mungu. “Mshukuru Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake zadumu milele”. Nabii Yeremia anaweka mbele yetu picha ya Mungu asiyekata tamaa juu ya kondoo wake hawa ambao wametawanyika, ambao wamepigwa, na ambao hawana matunzo kutoka kwa wale aliowategemea. Anawakusanya, anawarudisha zizini. Neno la Mungu linaendelea kusema: “nao watazaa na kuongezeka”. Uzazi ni ishara ya uhai na udumifu wa kizazi. Mungu anaendelea kuwa na watu wake na kuwafanya wasitawi zaidi na zaidi.

Mwishoni unatolewa Unabii wa Mchungaji mwema ambaye atatoka katika ukoo wa Daudi. “Tazama siku zinakuja ... nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki”. Mchungaji huyu anaitwa mmiliki katika haki, atendaye kwa hekima, anayehukumu kwa haki. Huu ni utabiri wa ujio wa Kristo. Utenzi wa Nabii Isaya wakati wa mkesha wa Sherehe ya Noeli unamtanabaisha Kristo katika sifa hizo: “Tumepewa mtoto mwanamume; na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani ...”. Huyu ni Mchungaji anayekuja kuwatunza Kondoo kadiri ya mapenzi ya Baba aliye mmiliki wa kondoo. Namna yake ya uchungaji inayathibitisha maneno ya Mungu mwenyewe kupitia kinywa cha Nabii akisema: “Mimi mwenyewe nitawachunga kondoo wangu, nami nitawalaza”.

Somo la Injili linamtambulisha Kristo katika uhalisia huo unaotabiriwa na Nabii katika somo la kwanza. “Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio an mchungaji”. Somo la Injili linaanza kwa kuonesha mazingira ya watumishi ambao wametoka kuhudumia na hivyo wanatafuta nafasi ya kupumzika ili kujichotea tena na tena nguvu kiroho na kimwili. “Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha; mahali pasipokuwa na watu mkapumzike kidogo”.

Mapumziko ni hitaji la kawaida na haki ya mwanadamu. Kitendo cha Kristo kuahirisha mapumziko haya kwa sababu ya hitajiko la kundi  ni shule mpya kabisa na inayotufunulia kwetu haki ya Mungu ambayo inaongozwa na upendo wa kimungu; upendo ambao hauongozwi na mantiki za kibinadamu bali mapenzi ya Mungu. Hili ndilo linampatia Kristo hadhi ya kuwa Mchungaji mwema. Yeye mwenyewe anasema: “Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo”.

Utumishi wetu kama Wakristo unapaswa kuakisi matendo ya Kristo. Mwanadamu amewekwa kuwa mwangalizi wa wenzake. Mwenyezi Mungu anatupatia karama na vipawa mbalimbali ili tuhudumiane katika upendo. Hivi ndivyo tunavyofanywa kuwa wachungaji kwa niaba ya mwenyezi Mungu. Mfano wa wachungaji waovu na waharibifu tunaowasikia katika somo la kwanza unaweza kufananishwa na wakristo ambao wanashindwa kuwajibika kama wakristo katika nyajibu mbalimbali za kijamii zilizoaminishwa juu yao. Kwa upande mwingine utumishi unaoakisi utendajiwa Kristo ni sababu ya furaha na matumaini kwa jamii nzima.

Katika jamii yetu wapo watu mbalimbali ambao walisikia wito huu na kuuitikia kwa ukamilifu. Mfano ni mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania na pia mtumishi wa Upendo mwenyeheri Mama Teresa wa Calcutta. Maisha yao ya kila siku yaliaakisi imani yao ya kikristo waliyoipokea. Daima walikuwa tayari kujitoa kwa ajili ya ustawi wa wale ambao walitaraji kuonja wema na upendo wa Mungu kupitia utumishi wao uliotukuka. Tunaamini bado wapo wengi ambao wanaendelea kutenda katika mrengo huu na hivyo kuifanya jamii ya mwanadamu kuendelea kuuonja wema na upendo wa Mungu

Lakini kwa upande mwingine bado lipo la kutafakari na kuona kama kweli ukristo unajidhihirisha duniani. Ulimwengu wetu wa leo bado umejaa mahangaiko na mengi yanayokatisha tamaa. Tunashuhudia maovu mbalimbali; wapo bado watoto yatima ambao wanakosa matunzo; wapo wajane ambao wanaishia kupokonywa haki zao; yupo mlalahoi ambaye anaendelea kukandamizwa na utu wake kununuliwa kwa vipande vya kanga na peremende. Sisi Wakristo tunawekewa changamoto mbele yetu. Ni dhahiri kwamba kuna mahali mambo hayaendi sawasawa. Kwa upande mmoja tunakumbushwa kwamba hatujawajibika kama wajumbe wa Kristo wa kueneza habari njema ya wokovu lakini kwa upande mwingine tunapewa changamoto kubwa ya sisi wenyewe kushindwa kuakisi maisha ya kiinjili katika utendaji wetu wa kila siku.

Ni jambo linalokosa maelezo katika jamii ambayo ndani mwake tupo sisi Wakristo lakini bado wema wa Mungu unashindwa kudhihirika kati ya wanajamii. Ni taadhari kwetu kwetu kuwa imani yetu tuliyoipokea bado haijaakisiwa na maisha tunayoishi. Ipo wapi imani ya kikristo katika jamii ambayo watu wanaishi kwa kugawanyika kati ya walionacho na wale wasionacho? Mtume Paulo anaelezea ukristo kama sababu ya umoja kati ya wanadamu. “Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga”. Matendo yetu ya leo yanazidi kututenga kabisa.

Ni changamoto ya jamii ambayo inayo wakristo ndani mwake lakini inaweka matabaka kati ya watu. Wapo walio na haki zaidi ya wengine. Katika kumbi za mahakama nchini Italia kuna kifungu cha maneno: “sheria ni sawa kwa wote”. Lakini katika uhalisia tunaona kupindishwa sana kwa maneno kama haya na baadhi ya wanajamii kufanywa kuwa na haki zaidi ya wengine. Ipo wapi imani ya kikristo katika jamii ambayo nguvu za kiuchumi zinawekwa kati ya watu wachache ambao wanaendelea kusitawi na kunawiri huku wengine wakibaki kutaabika kutafuta walau mkate wa siku moja? Yapo mambo mengine mengi sana ya kutafakari ambayo yanaonesha jinsi tunavyoshindwa kumuakisi Kristo mchungaji mwema na hivyo nasi kushindwa kuwa wachungaji wema.

Tujitafakari leo; ipo wapi imani yetu, upo wapi utumishi wetu? Je, ukristo upo ulimwenguni? Kama ulimwengu unao wafuasi wa Kristo ambao ndiyo wanapaswa kuwa wachungaji wa kondoo, maasi, wasiwasi wa maisha na mengine yanayohatarisha wanajamii walio kondoo wa Mungu ni mashtaka kwa utendaji wetu ambao unawatawanya badala ya kuwakusanya, utendaji wetu ambao unawafukuza badala ya kuwatunza katika zizi, utendaji wetu ambao unawanyima malisho badala ya kuwalisha yaliyo mema. Dominika ya leo tunakumbushwa kutafakari juu ya uwiano kati ya imani tunayokiri na imani tunayoishi.

Na Padre Joseph Peter Mosha.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.