2015-07-18 16:16:00

Waamini walioandikwa kwenye Orodha ya Watumishi wa Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu ameridhia majina ya waamini nane kuandikwa kwenye orodha ya watumishi wa Mungu, tayari kuanza mchakato wa kuwatangaza kuwa wenyeheri na hatimaye watakatifu. Kati ya watumishi wa Mungu wapya ni Askofu Giuseppe Carraro wa Jimbo Katoliki la Verona, aliyefariki dunia kunako mwaka 1980.

Ni mtu wa Mungu kutoka katika Familia maskini, akapadrishwa akiwa na umri wa miaka 24 na kuwekwa wakfu kuwa Askofu akiwa na umri wa miaka 54. Akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu Jimbo Katoliki Verona kwa miaka ishirini. Akawatumikia watu kwa unyofu, utakatifu wa maisha; akaonesha moyo na bidii ya sala na kukaza kuhusu utakatifu wa maisha ya Wakleri, ili waweze kushikamana na kuambatana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao, Kanisa na Familia ya Mungu wanayoihudumia katika Neno na Sakramenti za Kanisa.

Mtumishi wa Mungu Giuseppe Carraro ni kiongozi aliyewataka wakleri wake kuwa kweli ni watu wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo kwa njia ya mshikamano, umoja na udugu. Akawahudumia watu waliokumbwa na majanga asilia kwa moyo wa upendo na ubaba.

Watumishi wa Mungu wengine ni: Andrea Szeptycky, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Leopoli, nchini Ukraine aliyezaliwa tarehe 29 Julai 1865 na kufariki dunia tarehe 1 Novemba 1955.

Mtumishi wa Mungu Agostino Ramirez Barba, Padre wa Jimbo na mwanzilishi wa Shirika la Watumishi wa huruma ya Mungu. Alizaliwa tarehe 27 Agosti 1881, huko Mexico na kufariki dunia tarehe 4 Julai 1967.

Mtumishi wa Mungu Simpliano della Navitità, Padre na Mtawa wa Shirika la Ndugu wadogo wa Mtakatifu Francisko na mwanzilishi wa Shirika na Watawa Wafranciskani wa Mioyo Mitakatifu. Alizaliwa tarehe 11 Mei 1827 na kufariki dunia tarehe 25 Mei 1898.

Mtumishi wa Mungu Maria del Rifugio Aguilar y Torres, mwamini mjane na mwanzilishi wa Shirika la Watawa wa huruma wa Ekaristi Takatifu. Alizaliwa kunako tarehe 21 Septemba 1866 na kufariki dunia huko Mexico tarehe 24 Aprili 1937.

Mtumishi wa Mungu Maria teresa Dupouy Bordes, Mtawa wa Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu; mwanzilishi wa Shirika la Wamissionari wa Mioyo Mitakatifu ya Yesu na Maria. Alizaliwa tarehe 6 Mei 1873 na kufariki dunia nchini Hispania kunako tarehe 26 Mei 1953.

Mtumishi wa Mungu Elisa Micel, mwanzilishi wa Shirika la Watawa wa Katekesi vijijini wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Alizaliwa nchini Italia kunako tarehe 12 Aprili 1904 na kufariki dunia huko Frascati, Italia hapo tarehe 19 Aprili 1976. Mwishoni, ni Mtumishi wa Mungu Isabella Mèndez Herrero, mtawa wa Shirika la Wahudumu wa Mtakatifu Yosefu. Alizaliwa tarehe 30 Agosti 1924 nchini Hispania na kufariki dunia tarehe 28 Desemba 1953. Wote hawa wako tayari kwenye mchakato wa kutangazwa kuwa wenyeheri na hatimaye, kuwa watakatifu kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.