2015-07-18 17:11:00

Umoja wa Mataifa waipongeza Tanzania kwa kuwalinda na kuwahudumia wakimbizi


Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi Duniani (UNHCR) limesema kuwa Tanzania imekuwa kimbilio salama la wakimbizi kwa sababu ni nchi salama, ni nchi tulivu, ni nchi yenye mahusiano mazuri ya kijamii na yenye kuongozwa na sera nzuri na za kibinadamu.

Aidha, shirika hilo, limeiomba Tanzania kutoa ardhi ya kutosha ili kuliwezesha shirika hilo kujenga miundombinu na huduma kwa ajili ya wakimbizi 78,000 ambao wamekimbia Tanzania katika miezi ya karibuni kutoka Burundi. UNHCR limetoa sifa hizo kwa Tanzania wakati Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Mheshimiwa Antonio Guterres alipomkaribisha Rais Kikwete kwenye makao makuu ya shirika hilo yaliyoko mjini Geneva. Kwenye makao makuu hayo, Rais Kikwete pia amelakiwa na watumishi wote wa shirika hilo ambao wametoka nje ya ofisi yao kumlaki kwa makofi na vifijo.

Mheshimiwa Guterres amemwambia Rais Kikwete: “Tunafurahi kuwa umefika kwenye makao makuu yetu na tunapenda kuishukuru Tanzania tokea wakati wa Mwalimu Nyerere mpaka wakati wako kwa yote ambayo mmetufanyia. Tanzania imekuwa ishara kuu ya matumaini na imekuwa mlinzi mkuu wa wakimbizi duniani.”amesema Mheshimiwa Guterres.

Viongozi hao wawili pia wamejadili hali ilivyo katika Burundi na Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Guterres kuwa watu wanaokimbia Burundi kuingi katika Tanzania, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wanakimbia kwa hofu tu lakini Burundi hakuna vita wala mapigano.“Hakuna tishio la usalama kuhalalisha uzalishaji wa wakimbizi, lakini tumewapokea. Hakuna kubwa la kufanya kwa sababu unaamka asubuhi, unakuta wamekwishaingia nchini.” Rais Kikwete pia amemwambia Mheshimiwa Guterres ambaye alipata kuwa Waziri Mkuu wa Ureno kwa miaka sita unusu: “Tutaendelea kuunga mkono wakimbizi. Tanzania siyo nchi tajiri na hivyo ni matarajio yetu kuwa Jumuia ya Kimataifa itatusaidia katika kuwatunza wakimbizi hao.”

Kuhusu ombi la UNHCR kupatiwa eneo kubwa la kujenga miundombinu na huduma kwa ajili ya wakimbizi hao 78,000, Rais Kikwete amesema kuwa ataangalia nini la kufanya kumaliza tatizo la msongamano wa wakimbizi hao. Wakimbizi wa sasa ni mkumbo wa nne wa wakimbizi wa Burundi kuingia kwa wingi nchini tokea Uhuru mwaka 1961. UNHCR ni moja ya mashirika 31 ya kimataifa yenye makao yake katika Jiji la Geneva ambalo pia ni mwenyeji wa mashirika ya kimataifa yasiyokuwa ya Serikali zaidi ya 250 na balozi za kudumu 250 za nchi 173. Balozi wa Kudumu wa Uswisi katika Ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) Mheshimiwa Bruno Favel anasema kuwa mji huo ni mji mkuu wa shughuli za kibinadamu na masuala ya afya.


 








All the contents on this site are copyrighted ©.