2015-07-18 17:03:00

Teteeni mafao na masilahi ya Bara la Afrika; Mabalozi wakumbushwa!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ni wajibu wa Mabalozi wa Afrika katika Umoja wa Mataifa kulitetea Bara hilo kwa sababu hamna mtu mwingine atakayetetea maslahi ya Afrika. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni wajibu wa kila nchi kuamua aina ya mfumo wa kisiasa ambao unaifaa nchi husika bila kulazimika kuwepo ukomo wa kiongozi kukaa madarakani. Rais Kikwete ametoa ufafanuzi huo, Alhamisi, Julai 16, 2015, wakati alipozungumza na Mabalozi wa Afrika wanaowakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa na mashirika yake mjini Gevena, Uswisi.

Rais Kikwete yuko nchini Uswisi kuendesha vikao vya Jopo la Watu Washuhuri Duniani ambalo linatafuta njia bora zaidi za kuiwezesha dunia kukabiliana na majanga ya magonjwa ya milipuko katika siku zijazo. Jopo hilo liliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Aprili 2, mwaka huu na Jopo lilifanya mikutano yake ya kwanza Mei mwaka huu mjini New York, Marekani.

Akijibu swali la Balozi wa Benin ambaye amelalamikia shutuma zisizokuwa halali zinazoendeshwa na nchi na mabalozi wake dhidi ya Afrika katika masuala mbali mbali zikiwemo haki za binadamu. “Hii ni kazi na wajibu wenu. Afrika inaposhambuliwa isivyo halali na mataifa mbali mbali inakuwa ni kazi yetu kutetea. Nyie ndiyo mko hapa kwa ajili ya kutetea heshima ya Afrika na kulinda misimamo ya Bara letu. Na uwezo huo mnao wa kutosha kabisa.” “ Ni lazima pia mkumbuke kuwa dunia hii ni katili sana. Msitegemee mtu yoyote wa kututeteeni na kutetea haki na matakwa yetu. Nyie mlioko hapa ndiyo wenye wajibu wa kututetea na kazi hiyo mnaiweza.”

Akijibu swali jingine ambalo mwuuliza amesema kuwa baadhi ya viongozi wa Afrika wamekuwa wanatumia visingizio mbali mbali ukiwemo ugaidi ili kuhalalisha kubakia madarakani, Rais Kikwete amesema kuwa ugaidi hauna uhusiano na uamuzi wa watu kubakia madarakani kwa muda mrefu. “Nchi zinatofautiana. Kuna baadhi ya viongozi wana hamasa ya kubakia madarakani, wengine hawana. Ni uamuzi wao wenyewe kama wana hofu ya kutoka madarakani ama hawana uhakika kabisa kuwa maisha yao yataendelea kuwa ya kawaida kama wakitoka madarakani.”

Balozi wa Zimbabwe ameipongeza Tanzania na Rais Kikwete kwa mchango wake mkubwa katika jitihada za kukabiliana na malaria na kuonyesha uongozi katika Jumuia za Afrika Mashariki (EAC) na Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) . Naye Balozi wa Rwanda amempongeza Rais Kikwete kwa uongozi wake katika EAC ambako Rais ni mwenyekiti.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.