2015-07-18 15:46:00

Sikilizeni kilio cha waathirika wa sekta ya madini duniani!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati huu Kanisa linaposikiliza kilio cha watu wanaoathirika na kuteseka kutokana na uchimbaji wa madini anasema, kuna haja kwanza kabisa ya kusimama kidete, kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu pamoja na kuungana na jumuiya za wale walioathirika na vitendo hivi.

Mkutano huu wa siku tatu, ulioanza, hapo tarehe 17 Julai unahitimishwa tarehe 19 Julai 2015 mjini Roma. Mkutano huu umeandaliwa na Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kushirikiana na mtandao wa waathirika wa sekta ya uchimbaji wa madini Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu anasema, hiki ni kilio kwa ajili ya watu waliopoteza ardhi, kilio cha utajiri na rasilimali inayoendelea kuwanufaisha watu wachache ndani ya jamii, wakati umma mkubwa unaogelea katika dimbwi la umaskini.

Ni kilio kinachotokana na uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji, kiasi cha kuhatarisha usalama wa maisha ya watu. Hiki ni kilio cha kinzani na misigano ya kijamii na wawekezaji; mambo ambayo wakati mwingine yanafumbiwa macho na viongozi wa serikali kitaifa na kimataifa; kundi ambalo lina dhamana ya kuhakikisha kwamba, linasimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu. 

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kuhusiana na changamoto aliyoitoa kwenye Waraka wake wa kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, unaohimiza ushirikiano na mshikamano kati ya watu kama sehemu ya mchakato wa kulinda na kutunza mazingira, nyumba ya wote, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Sekta ya madini inapaswa kuangaliwa upya ili kufanya mabadiliko makubwa yatakayosaidia kuleta maboresho ya maisha ya wananchi wengi duniani anasema Baba Mtakatifu Francisko. Mabadiliko haya yataziwezesha Serikali kupata mapato stahiki kutoka kwenye sekta ya madini pamoja na kuendelea kuchangia ustawi na maendeleo ya nchi zenye makampuni makubwa ya kimataifa. Hii ni sekta ambayo inaweza kuharakisha maendeleo ya watu wengi, tangu pale madini yanapochimbwa hadi yanapomfikia mlaji sokoni.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wadau wote wa sekta ya madini wanapaswa kutambua kwamba, wanaunda familia moja ya binadamu wanaohusiana na kuhamasishwa kulinda na kudumisha maisha kwa kujikita katika utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote. Watambue kwamba, mahusiano ya kibinadamu yanaambata udugu, haki na uaminifu; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kusema kwamba, ikiwa mambo haya yatapewa kipaumbele cha pekee, basi, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kupata ufumbuzi wa changamoto na matatizo yanayoendelea kujitokeza kutoka katika sekta ya madini duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.