2015-07-18 16:30:00

Mh. Padre Natale Paganelli, S.X. ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Makeni


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Natale Paganelli, S.X., Msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki Makeni, Sierra Leone kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Makeni. Askofu mteule Paganelli alizaliwa kunako tarehe 24 Desemba 1956, Jimbo Katoliki la Bergamo, Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kikasisi, akaweka nadhiri zake za daima hapo tarehe 3 Desemba 1979. Tarehe 25 Desemba 1980 akapewa Daraja Takatifu la Upadre.

Katika maisha na utume wake kama mmissionari amekaa miaka 22 nchini Mexico na kunako mwaka 2005 akatumwa na Shirika lake la Wasaveriani kwenda Sierra Leone. Tangu wakati huo, amekuwa mkurugenzi wa miito, Gombera wa Seminari ndigo ya San Juan del rio, Mexico; Mlezi wa wanovisi, Mkuu msaidizi wa Shirika huko Mexico, Mkuu wa Shirika.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Henry Aruna kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo la Kenema, Sierra Leone kwa kumwamisha kutoka Jimbo Katoliki la Makeni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.