2015-07-18 15:58:00

Majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa ya Kipentekosti na Kanisa Katoliki


Mkutano wa awamu ya sita ya majadiliano ya kiekumene kimataifa kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kipentekosti, uliokuwa unafanyika mjini Roma kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 17 Julai 2015 umekamilika. Ni mkutano ambao umesimamiwa na Baraza la Kipapa la kuhamasisha umoja wa Wakristo kwa kushirikiana na viongozi wa Makanisa ya Kipentekosti. Kwa pamoja wameangalia juu yak arama ndani ya Kanisa; maana na umuhimu wake katika maisha ya kiroho; utambuzi na mwingiliano wake katika shughuli za kichungaji.

Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, majadiliano ya kiekumene yamekuwa yalikijita ktika Karama: kwa kuangalia msingi wa Makanisa haya; Utambuzi; Uponyaji na Unabii. Mkutano wa mwaka 2015 umejikita zaidi katika kuandika taarifa ya mwisho inayotarajiwa kuchapishwa rasmi mwanzoni mwa mwaka 2016. Itambukwa kwamba, majadiliano ya kiekumene na Makanisa ya Kipentekosti yalianza kunako mwaka 1972, ili kutoa nafasi kwa waamini kuheshimiana, kuthamiana na kuelewana katika masuala msingi yanayowaunganisha katika imani kwa Kristo na Kanisa lake. Wamegusia pia umuhimu wa sala katika maisha ya waamini.

Majadiliano ya kiekumene upande wa Kanisa Katoliki yanaongozwa na Askofu Michael F. Burbidge wa Jimbo Katoliki la Raleigh, Marekani. Mwenyekiti msaidizi ni Mchungaji Cecil M. Robeck kutoka katika Kanisa la “Assemblies of God” Marekani. Wakati wa mkutano wao hapa Roma, Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa umoja wa Wakristo amekutana na wajumbe pamoja na kubadilishana mawazo kuhusiana na mchakato mzima wa majadiliano ya kiekumene. Wamepata nafasi ya kutembelea na kusali kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya kuta.

Wajumbe wa mkutano huu wanasema, majadiliano yamefanyika katika hali ya utulivu, amani na heshima kubwa; mambo ambayo ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene; kwa kutambua shida, fursa na changamoto zinazowakabili Wakristo katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Kwa pamoja wanataka kumwomba Roho Mtakatifu awasaidie kutumia karama na mapaji yao kwa kujikita katika Uinjilishaji unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Wajumbe wanakaza kusema, kuna uhusiano mkubwa kati ya mafundisho ya Makanisa ya Kipentekoste na Kanisa Katoliki kuhusiana na karama pamoja na mapaji ya Roho Mtakatifu; karama zinazopaswa kutumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa zima. Karama hizi zimekuwemo ndani ya Kanisa tangu wakati wa Agano Jipya. Huu ni mwaliko wa kushikamana kwa pamoja ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ni changamoto ya kutubu, kuongoka na kujipatanisha, ili kweli Yesu Kristo aweze kuwa kweli ni Bwana na Mwalimu katika hija ya maisha ya waamini wake.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Brian Farrel, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa linalohamasisha umoja miongoni mwa Wakristo anasema, Waraka unaotarajiwa kuchapishwa hapo mwakani ni kutaka kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mwaliko wa kumwilisha Injili katika uhalisia wa maisha kwa kujikita na kuzama katika maisha ya sala, daima Mwenyezi Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza.

Askofu Bran Farrel anasema, waamini wa Makanisa ya Kipentekoste ni watu ambao wanajituma katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu, ili kuwashirikisha Watu wa Mataifa kwamba, wokovu unapatikana kwa kumwamini na kumwambata Kristo Yesu. Ni waamini wanaotaka kushuhudia na kumwilisha imani yao inayopata chimbuko lake katika neema ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.