2015-07-18 13:28:00

Je kwa vipi inawezekana kufuta umaskini: Mimi na wewe tujiulize!


Na tujiulize, Iwapo hotuba za viongozi majukwaani zinaonyesha hamu ya kufuta umaskini, kumbe kipingamizi ki wapi? Hilo ni swali msingi la wiki  hii katika Makala Dunia Mama , Mama Dunia mwenye kupokea wote wanaozaliwa na wanaofikwa na kifo, wote akiwakumbatiana kwa upendo mkuu na kuwafadhili. Tunaendelea na Mada Kuu: Jamii katika Maisha Mchanganyiko. Mara ya mwisho tulichambua juu ya  maana ya maisha matakatifu, na  je tunaweza jifunza nini kutoka kwa mtu maskini, mtu hohehahe wa mitaani.

Tulizama katika tafakari iliyotolewa na Papa Francisko,  alimoonyesha kujali jinsi watu hawa maskini, wanavyosetwa na wenye uwezo,  hadhi yao ikidharirishwa na hata kufanywa kama bidhaa za kuuzwa sokoni. Papa alikemea vikali tendo au majadiliano yoyote yale yanayomfikisha binadamu kuumuuza mwingine, akisema , kamwe isitokee dhulma hii ya binadamu  kufanywa  bidhaa ya kuuzwa na kununuliwa. Na mtu yeyote anayewatumia watu kwa njia yoyote ile  iwe moja kwa moja  kwa moja au kwa kificho,  kwa lengo la kutafuta kujitajirisha, anajue anatenda dhambi  kubwa ya  kuvunja heshima na haki za  binadamu mwenzake. Fedhuli huyo  anapaswa  kuwajibishwa  kisheria.  

Papa anasema , umaskini si kigezo cha  mtu kudhararuriwa. Heshima ya utu wa mtu haitokana na vile alivyo navyo, kwa kuwa heshima ya utu wake huumbwa nayo tangu mimba inapotungwa.  Papa alieleza hili, kupitia Mkutano wa Asasi ya Katoliki ya Kimataifa,  Caritas Internationalis, w akati wa Mkutano wake uliofanyika hapa Roma, hivi karibuni.  

Maoni ya Papa Francisco pia yanaturejesha katika mkutano wa Viongozi wa ngazi ya juu wa dunia, waliokuwa wamekusanyika huko   Addis Ababa  Ethiopia, uliokamilika Alhamisi iliyopita. Mkutano uliojumuisha Wakuu wa nchi na serikali, Mawaziri, Wawakilishi toka masharika makubwa duniani na Uwakilishi wa jamii na watunga sheria , kujadili jinsi inawezekana kupata fedha za kufadhili maendeleo endelevu kwa watu wote duniani.  Viongozi mbalimbali wa dunia waliweza kutoa mchango wao kwa jinsi wanavyoona inawezekana kuwa na mipango ya ufadhili kwa ajili ya kutomeza adha ya umaskini wa kukithiri kwa watu duniani.

Katika Mkutano huu,  Katibu Mkuu  wa Umoja wa Mataifa , Ban Ki-moon katika mkutano huo , ametoa wito kwa mataifa yaweke kando mambo na shughuli zote zenye kuleta utengano na mgawanyiko  miongoni mwa jamii , badala yake iwe kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya ubinadamu wote. Alipenda kusikia na kuona maoni yote yanaelekezwa katika ujenzi wa  dunia endelevu huru, yenye kuinasua dunia  dhidi ya uwepo wa pengo kubwa kati ya wenye navyo na wasiokuwa navyo yaani kati ya tajiri na maskini. Aliomba mabadiliko hayo yaanze mara moja katika mkutano huo muhimu wa kukabiliana na umaskini  wa kukithiri.

Ban Ki moon  pamoja na kufurahia  baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka  miaka kumi na mitano iliyopita, alionyesha pia kujali kwamba,  bado kuna mengi ya kufanikisha kwa ajili ya kuwaondoa binadamu wote katika hali za kutisha za umaskini.  Na alionyesha imani na dhamira yake katika mwendelezo wa  mapambano kwa yale yaliyobaki nyuma katika  kufikia ukomo wa malengo ya Maendeleo ya Milleni ayaliyowekwa tangu mwaka 2000. Hivyo mawazo ya Katibu Mkuu yalielekezwa zaidi katika  utendaji wa kipindi cha miaka kumi na tano ijayo baada ya awamu ya kwanza ya malengo ya maendeleo ya milenia yanayo kamilika mwaka huu 2015.  Bw Ban amewataka viongozi  duniani, hasa mataifa tajiri kujenga ushirikiano na mshikamano wa kweli kwa ajili ya kutokomeza umaskini  na kufanikisha yale yaliyotajwa  katika mkutano wa Rio + 20  wa mwaka 2012 nchini Brazil kwa ajili pia ya kulinda sayari.

Mpendwa msikilizaji , wakati mwingine, hushangaza , jinsi inavyokuwa vigumu kwa watu kubadilika kama inavyoshauriwa.  Suala hili la kufuta umaskini wa kukithiri miongoni mwa watu duniani , si hoja geni kwani imekuwepo  miaka nenda  rudi  lakini bila uwepo wa hatua za kuonekana katika utendaji kwa ajili ya kutokomeza  umaskini.  Dunia Mama anahoji, hadi lini, hili litaendelea kuwa wimbo wa viongozi wa duniani? ? Ni nini hasa kinacholeta ugumu katika kufuta umaskini, iwapo kila kiongozi aliyesimama kutoa mchango katika mkutano , kama ilivyokuwa  Addis, huoonyesha hamu kubwa ya kutaka kufuta umaskini katika uso wa dunia?

Je ni kama alivyosema Rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim, katika kikao cha Addis Ababa kwamba,  mataifa hayawezi  kukomesha umaskini uliokithiri kwa kuendelea na  mifumo ya biashara ya kimataifa  iliyopo sasa? Kwa nini mifumo hiyo inaendelea kuwepo kama inaathiri wengine? Kuna nini nyuma ya hiyo mifumo?  Jim Yong Kim,  ameomba  uwepo wa  ujasiri wa kufanya mabadiliko, kuwa na ari mpya, ubunifu mpya na ushirikiano mpya, katika  kufikia malengo ya dunia. Ameshauri nchi ziwekeze  kimkakati, hasa katika elimu ya watoto, huduma za afya na miundo mbinu, dhidi ya moyo wa kuthamani uwepo wa mali na ufahali wa utajiri, wenye kuzalisha athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

 Aidha  Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma, ameonyesha  hamu ya kujenga dunia iliyo huru dhidi ya njaa, maradhi na ujinga, kama ambavyo imekuwa ni wito kwa mataifa ya Afrika miaka 50 iliyopita , wakati wa mapambazuko ya uhuru  kwa nchi za Kusini mwa Afrika.  Dlamini Zuma anasisitiza,ili kuwe na mabadiliko chanya katika juhudi za kutokomeza umaskini unaorarua idadi kubwa ya wana wa Afrika,  "Afrika inahitaji mapinduzi katika ujuzi hasa katika sayansi, teknolojia, uhandisi na ubunifu. Anasema pamoja na mengi yanayotiliwa mkazo juu ya kuondoa umaskini uliokithiri ', ni  kuna umuhimu wa kuchambua kw akina nini hasa ni vinakwamisha ustawi endelevu kwa watu wa Afrika hasa wanaoishi vijijini.

Maoni haya yote si mageni , kwa kuwa hata waraka wa Kichungaji wa Papa Paulo V1 wa sita juu ya Maendeleo ya watu, uliotoewa hapo March 26, 1967, umeelezea vizuri sana juu ya maendeleo kamili ya mtu. Jinsi mtu maskini anavyohangaika kupata  uhakika wa chakula , huduma  za afya , elimu na ajira. Waraka huo pia ulizungumzia juu ya mpanuko  wa pengo kati ya maskini na tajiri, mkitaja   kati ya sababu ni mifumo mibovu ya kiuchumi inayotaji kufanyiwa marekebisho, kwa lengo la kujenga uwiano mzuri unaoweza kufuta pengo kubwa kati ya nchi tajiri na nchi maskini, kwa mtazamo wa ngazi ya chini kabisa kati ya mtu tajiri na maskini.  Na pia waraka huu wa mwaka 1967, unataja umuhimu wa utulivu wa kijamii katika kufanikisha maendeleo miongoni mwa jamii, kama pia ilivyosisitizwa na wafuasi wake, Papa Yohane Paulo 11 katika waraka wake wa Maisha ya binadamu (humanae Vita ) Papa Benedikto XV1, katika waraka wake wa Kichungaji wa Upendo katika ukweli wa Julai 7, 2009 na Waraka wa Kitume kwa Kanisa barani Afrika Afrika Munus, wa 2011 na pia waraka wa  Papa Francisko wa Injili ya Furaha na hotuba zake za hivi karibuni  Amerika ya Kusini ambako alitembelea mataifa matatu , Ecuador , Bolivia na Paraguay.

Si Viongozi tu hawa wakuu wa Kanisa , waliozungumza kwa nguvu suala hili la kukabiliana na umaskini wa kukithiri lakini pia hata viongozi mashuhuli wa kale katika uwanja wa siasa, kama Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania, Nkwame Nkurumah wa Ghana, akina Nelson Mandela,  Nickson wa Marekani n.k . Wote walitoa hoja ya watu kubadilisha mifumo ya maisha. Lakini inavyoonekana  binadamu hataki kubadilika. Katika vipindi vyote na lika zote ,  binadamu anaweka kiwambo masikio mwake kwa kila ushauri unaoonekana kuwa na mwelekeo wa kuziba njia ya faida binafsi. Ushauri huingia katika sikio la kulia na kutokea kushoto , ikiwa ni mtoko wa moja kwa moja usiorudi nyuma.

Kwa hali hiyo, Dunia Mama anahoji , je  inawezekana kweli kufuta umaskini wa kukithiri miongoni mwa jamii? Dunia Mama anatambua ukweli kwamba,  binadamu haiwezekani kulingana katika kila hali. Lakini kinacho zungumzwa ni uwezo wa kupata mahitaji msingi  kama chakula malazi na elimu na huduma za Afya.  Chakula ni chakula haijalishi mmoja kula ugali  au ubwabwa au chipsau kwamba mwingine ana gorofa na mwingine nyumba ya kawaida. Kinacho jalisha ni mmoja kulala ndani ya nyumba na mwingine kulala nje ukumbini kwa kuwa hawezi kumudu kujenga nyumba yake. Au mtu kuwa na chakula kingi kiasi cha kuharibika na kutupa jalalani wakati  jirani  anashindia mlo mmoja kwa siku, kutokana na mazingira yanayomzuia kuzalisha chakula cha kutosha .

Kwa mujibu wa takwimu za utajiri uliopo, kama kutakuwa na mgao mzuri wa utajiri huo, inawezekana kabisa kufuta umaskini wa kukithiri. Hichondicho wanachodai baadhi ya viongozi katika majukwaa. Lakini ili kufanikisha hilo ni lazima binadamu abadilike.  Watu wote  hsa wenye mamlaka na uwezo wa kihali, ni lazima kuitikia wito huu wa kufanya mabadiliko chanya katika maisha. Kukubali kugawana nawengine kinachopatikana. Haisemwi kama ni kugawana nusu kwa nusu lakini basi kuwe na mgao wa kuwmezesha kila mmoja kuishi katika hadhi ya kiutu. Mtu asilale nje au kulala njaa au kukosa huduma msingi za elimu na afya.  Ni wito wa kuacha kuifanya mioyo yetu migumu,  lakini kusikiliza na kuitikia wito wa kubadilika.  Ni kuachana na ubinafsi, na kuwa na utendaji kwa  manufaa ya wote.  Ni wito wa kuthamini utu wa mwingine kama una maana zaidi ya mali za dunia.. kama alivyoomba BabaMtakatifu Francisco wakati wa ziara yake ya Kitume Amerika ya kusini hivi .

Mpendwa msikilizaji, dunia mama anasema,viongozi watazungumza sana kwenye majukwaa. Lakini kama hakuna moyo wa dhati katika kufanya mabadiliko yote ni bure. Ingawani kweli kwamba ,jamii yote ya bindamu haiwezi kulingana katika yote , lakini inawezekana kupunguza mpanuko wa pengo katika ukosefu wa mahitaji msingi ya binadamu kama chakula, makazi  na huduma.  Bila kuwa na moyo wa kujali mahitaji ya wengine , kama ilivyoelezwa katika nyaraka  mbalimbali, umaskini wa kukithiri utaendelea kuwepo, likifanywa kuwa hoja mpya kila siku na kila mmoja katika wakati wake.

Papa asema akiwa nchini Paraguay kwamba, ni muhimu  kwa uongozi wa kiserikali na wanasiasa na watu wote , kutoa kipaumbele kwa maskini hasa kupitia mwendelezo wa  nia ya kujenga demokrasia imara,  kupambana na rushwa,  na yote yanayo momonyoa  demokrasia .  Papa alitaja kipimo cha kweli cha mafanikio na ustawi wa taifa ni hadhi ya wanyonge katika  uchumi wa taifa! Ni katika jinsi utu wa mtu unaheshimiwa, hasa  kwa wanaoishi katika mazingira magumu zaidi na wasioweza jitetea.  Papa alisisitiza,  kwamba utendaji wa  haki, hujenga upendo ulio imara zaidi kati ya mtu na mtu , na hivyo  hakuna  tena chuki wala wivu na hakuna anayeachwa nyuma, nje au kupuuzwa katika mipango yote ya Kijamii.

Kwa maoni hayo Dunia Mama pia leo hii  inawasihi watu wote waitikie wito hiìuu wa kufanya mabadiliko chanya katikamaisha ya kushirikishana na kugawana kinachozalishwa, kam ainavyombwa na viongozi wema.  Tuachane na kiburi cha ubinafisi na roho ya kujilimbikizia mali kama ndiyo maisha bora, lakini tuwe na roho  laini, katika kuwajali wengine, hasa katika muono wa kina kwamba yote tunayoyakumbatia hapa duniani siku moja tutakapolala moja kwa moja yote tutayaacha hapa.

Makala haya huandaliwa na T.J.Mhella

Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.