2015-07-17 15:39:00

Wazazi na walezi, onesheni ushuhuda wenye mvuto katika kuhamasisha miito!


Wazazi na walezi ndio walinzi na wahamasishaji wa kwanza wa miito mbali mbali ndani ya Kanisa. Hao ndio wenye dhamana ya kusaidia mchakato wa kulea na kukuza miito ya maisha ya kitawa, ndoa na familia. Hayo yamesemwa na wajumbe wa kongamano la miito mitakatifu ndani ya Kanisa lililokuwa limeandaliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE na kufanyika huko Prague, Jamhuri ya Watu wa Czech.

Mkutano huu umewashirikisha wajumbe 70 kutoka katika nchi 19 za Ulaya na Marekani na kwamba, wajumbe wamepata nafasi ya kubadilishana: uzoefu, ujuzi na maarifa yanayopania kukuza na kudumisha miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Wamegusia vikwazo na changamoto wanazokabiliana nazo vijana katika kuamua miito ya maisha yao kwa siku za usoni. Imekuwa ni nafasi pia ya kusali kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu na kusaidia kubainisha mielekeo inayoweza kudumisha miito mitakatifu, ambayo inapata chimbuko lake katika maisha ya ndoa na familia.

Wajumbe wameangalia pia changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha ya ndoa na familia sehemu mbali za dunia na kusema kwamba, wazazi wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa kwanza wa Injili ya familia; kanuni maadili, imani na utu wema. Wajumbe wamesikiliza ushuhuda uliotolewa na Padre Kamil Skoda kutoka Jamhuri ya Watu wa Czech aliyekuwa ameambatana na wazazi wake. Kwa pamoja wameonesha jinsi ambavyo wazazi wanavyoweza kusaidia kukuza na kuimarisha miito ya Kipadre na kitawa miongoni mwa vijana.

Mkutano huu pia umeshuhudia watu mbali mbali wakitoa shuhuda za maisha yao kuhusu huduma ya Kanisa na utume kwa vijana wakati wa utawala wa Kikomunisti; ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia; hali ya maisha na ndoa Barani Ulaya pamoja na kanuni msingi zinazoweza kusaidia kuwafunda vijana katika masuala ya imani, maadili na utu wema; tayari kuonesha pia ukarimu wa kupokea, kulea na kukuza miito mitakatifu kuanzia ndani ya familia.

Wajumbe wamepata nafasi ya kufanya upembuzi wa kina kuhusu mgogoro unaoendelea kuzikumba familia mbali mbali Barani Ulaya na kwamba, vijana wanapaswa kusaidiwa ili kutambua, kuheshimu na kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, bila kufanya hivi kuna hatari kwa vijana kujikuta wakiwa wanamezwa na malimwengu na hivyo kushindwa kuthamini umuhimu wa maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Kwa upande wake Monsinyo Jorge Carlos PatrĂ²n Wong, Katibu mkuu wa Seminari katika Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri amegusia mikakati ya kichungaji inayoweza kusaidia kuwaongoza vijana katika wito na maisha ya kipadre. Wazazi wanapaswa kutambua kwamba, wao ni mashuhuda wa kwanza wa miito, imani na utakatifu wa maisha. Wao wanapaswa kulinda, kukuza na kuendeleza miito, ili watoto wao waweze kuwa na ujasiri wa kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.