2015-07-17 14:36:00

Kanisa linapenda kusikiliza kilio cha waathirika wa machimbo ya migodi duniani


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Ijumaa tarehe 17 Julai 2015 anasema kwamba, Baraza lake kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 19 Julai 2015 linafanya mkutano maalum na wawakilishi thelathini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaoathirika kutokana na uchimbaji wa migodi ya madini. Mkutano huu unaongozwa na kauli mbiu “Tukiwa tumeungana na Mwenyezi Mungu, tunasikiliza kilio”.

Mkutano huu unafanyika katika hali ya faragha, kama fursa maalum ya kusikiliza shuhuda mbali mbali zinazotolewa na watu wanaoathirika kutokana na uchimbaji wa madini sehemu mbali mbali za dunia. Ni fursa ya kushirikishana: uzoefu, mang’amuzi na kuibua mbinu mkakati unaoweza kutumiwa na Mama Kanisa katika kukabiliana na changamoto hizi ambazo kwa kiasi kikubwa zina athari kubwa kwa maisha ya watu.

Mkutano huu anasema Kardinali Turkson ni jibu la kilio kilichotolewa kunako mwaka 2013 wa kutaka kuangalia sekta ya uchimbaji wa madini, ambao unaendelea kusababisha madhara makubwa si tu katika mazingira husika, bali hata katika maisha ya wananchi wanaoishi katika maeneo haya. Mkutano wa mwaka huu unapania pamoja na mambo mengine kutoa dira na mwelekeo unaoweza kutumika kwa ajili ya kulinda na kutunza mazingira, kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake juu ya utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote.

Kanisa likisukumwa na huruma pamoja na upendo wa Mungu, linapenda kusikiliza kilio cha watu wanaoathirika na sekta ya uchimbaji wa madini, ili kweli haki iweze kutendeka. Kuna faida kubwa inayozalishwa na sekta ya madini, lakini inaishia mikononi mwa wajanja wachache. Mama Kanisa katika matukio mbali mbali ameendelea kufuatilia kuhusu uvunjifu wa haki msingi za binadamu, uharibifu na uchafuzi wa mazingira; ukosefu wa ulinzi na usalama pamoja na hatari ya ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini.

Kardinali Turkson anakaza kusema, hii ni changamoto inayowahusisha wadau mbali mbali, kitaifa na kimataifa; ili kuhakikisha kwamba, wahalifu na wachafuzi wa mazingira wanafikishwa kwenye mkondo wa sheria; Jamii inajifunza kusimama kidete kulinda na kutetea haki na mafao ya wengi; maendeleo endelevu; utu na heshima ya binadamu.  Muda wa hizi siku tatu, Kanisa linapenda kusikiliza kilio cha wale ambao pengine hawasikilizwi kamwe hata pale wanapopaaza sauti zao.

Baraza la Kipapa la haki na amani limepokea shuhuda za vitisho vya kifo, mateso na nyanyaso pamoja na dhuluma, kiasi kwamba, hata pale walipoondolewa kwenye ardhi yao, ili kupisha uchimbaji wa madini, hawajapata malipo yao halali. Wahusika wakuu ni wawekezaji katika sekta ya madini, wanasiasa na viongozi wa Serikali; makao makuu ya Makampuni ya kimataifa ya uchuimbaji wa madini. Upande wa maskini, wao wanataka kuona haki inatendeka; mafao ya wengi yanapewa kipaumbele cha kwanza; kanuni maadili zinatekelezwa na mazingira yanalindwa na kuendelezwa.

Ni jambo lisilokubalika anasema Baba Mtakatifu Francisko katika waraka wake wa kitume juu ya utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote kwamba, si haki baadhi ya mataifa kutajirika kwa kutumia mgongo na rasilimali ya nchi maskini duniani. Kanisa linapenda kuonesha uwepo na mshikamano wake wa dhati na watu wote walioathirika kutokana na athari za uchimbaji wa madini katika ngazi mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.