2015-07-17 15:07:00

Cheche za matumaini katika matumizi ya fedha na mali za Kanisa!


Taarifa ya bajeti ya Vatican kwa mwaka 2014 inaonesha pungufu ya kiasi cha Euro millioni 25, 621 na kwamba, Utawala wa mji wa Vatican umepata salio la kiasi cha Euro millioni 63, 519. Hizi ni takwimu ambazo zimetolewa na Kardinali George Pell na jopo la Sekretarieti ya uchumi; bajeti ambayo imeandaliwa na Kitengo cha masuala ya kiuchumi na kuhakikiwa na Sektretarieti kuu ya Vatican na wakaguzi wa fedha kutoka nje.

Itakumbukwa kwamba, mwaka 2014 umekuwa ni mwaka wa kipindi cha mpito katika utekelezaji wa sheria na kanuni za kimataifa kuhusu masuala ya fedha za umma, IPSAS. Bajeti ya mwaka 2014 imeandaliwa kwa kuzingatia vigezo vya sheria zilizopita kwa kuhusisha vitengo 64 vya Vatican. Wakuu wa Mabaraza na idara mbali mbali walitakiwa kuhakikisha kwamba, wanaingiza katika taarifa ya bajeti zao kadiri ya hali halisi kwa kuzingatia: weledi, ukweli na uwazi. Masuala yote yamehakikiwa kitaaluma kwa mwaka 2014, tayari utekelezaji wa bajeti kwa kuzingatia sheria na kanuni mpya zilizotolewa hivi karibuni.

Mageuzi kuhusiana na masuala ya mapato na matumizi ya fedha ya Kanisa, imekuwa ni changamoto pevu, lakini kwa sasa mambo yanaelekea kuwa shwari na kwamba, Sekretarieti ya uchumi mjini Vatican inaridhika kwa hatua iliyofikiwa hadi sasa. Kuna ushirikiano mkubwa kati ya Sekretarieti pamoja na vitengo mbali mbali vilivyoko mjini Vatican.

Bajeti ya mwaka 2014 ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na jopo la wafanyakazi wa Vatican hususan kitengo cha fedha na uchumi pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican. Baraza la kipapa la uchumi linawapongeza wote waliojisadaka na kuitekeleza kazi hii nyeti kwa weledi, ukweli na uwazi, kama kielelezo cha utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu umakini wa matumizi ya fedha na mali ya Kanisa.

Bajeti ya Vatican kwa mwaka 2014 inaonesha upungufu wa Euro millioni 25, 621. Hali si mbaya sana kwani katika kipindi hiki pia kumekuwepo na ongezeko la vitega uchumi, mchango kutoka kwa Makanisa mahalia kadiri ya sheria za Kanisa kwa kuchangia Euro millioni 21 pamoja na mchango kutoka Benki ya Vatican, IOR, Euro Millioni 50.

Rasilimali ghafi ya Vatican imeongezeka hadi kufikia Euro millioni 939 katika taarifa ya mwaka 2014. Mfuko wa Pensheni wa Vatican haukuingizwa katika bajeti hii, kumbe utatakiwa kuandaa taarifa yake na hatimaye, kuiwakilisha kwenye Baraza la Kipapa la uchumi. Takwimu zinaonesha kwamba, kiasi kikubwa cha bajeti ya Vatican kinatumika kwa ajili ya kulipa mishahara ya wafanyakazi. Jumla ya Euro millioni 126, 6 ni mishahara ya wafanyakazi 2, 880 wanaotekeleza nyajibu zao katika mabaraza, taasisi na vitengo 64 vya Vatican.

Utawala wa mji wa Vatican unaonesha kwamba, kumekuwepo na salio la kiasi cha Euro millioni 63, 519. Sehemu kubwa ya mapatao haya ni kutoka kwenye Makumbusho ya Vatican pamoja na vitega uchumi mbali mbali. Rasilimali ghafi ya Vatican imeongezeka pia hadi kufikia Euro millioni 63. 5. Wakaguzi wafedha kutoka nje wameridhishwa na taarifa iliyotolewa na kuamua kutoa cheti cha uthibitisho kwamba bajeti ya Vatican na utawala wa mjini wa Vatican kwa ujumla wake ni safi.

Baraza la kipapa la uchumi limetaarifiwa kuhusiana na bajeti ya mwaka 2015, iliyoandaliwa kadiri ya Sera mpya za usimamizi wa fedha na kupitishwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2014. Mwezi Mei, 2015, Baraza hili lilipokea mapendekezo ya Bajeti kwa kuonesha mapato na matumizi kwa vitengo 136 vitakavyosimamiwa na kukaguliwa na Baraza pamoja na Sekretarieti ya uchumi. Kuna dalili kwamba, bado kutaendelea kuwepo na upungufu wa fedha kama ilivyojionesha katika bajeti ya miaka iliyopita.

Kuna mafanikio makubwa yaliyofikiwa na tangu mchakato wa mageuzi kuhusu sera za mapato na matumizi ya fedha na mali ya Kanisa kupitishwa na Baba Mtakatifu Francisko. Kumbe bajeti ya mwaka 2015 pamoja na mapato na matumizi ni mambo msingi katika utekelezaji wa mchakato wa mageuzi haya ambayo bado yanahitaji muda ili kuweza kuona matunda yanayokusudiwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.