2015-07-17 14:53:00

Baa la njaa na umaskini ni kati ya changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa


Mkutano mkuu wa tatu ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa kuhusu fedha na maendeleo umehitimishwa huko Addis Ababa, Ethiopia, kwa kuweka mikakati ya kugharimia mchakato wa maendeleo endelevu katika kipindi cha miaka kumi na moja kuanzia sasa. Wajumbe pia wameonesha utashi wa kuendelea kushirikiana katika kuchangia mchakato wa maendeleo, jambo ambalo lilileta mvutano mkubwa miongoni mwa wajumbe.

Protokali hii itakapokubaliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa itakuwa ni msaada mkubwa katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015. Agenda hii itatakiwa kupitishwa pia na viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa, katika Baraza kuu la Umoja wa Mataifa litakalofanyika mwezi Septemba, 2015 huko New York Marekani. Hatua iliyofikiwa huko Addis Ababa anasema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon inatia matumaini ya kuwa na sera na mikakati ya maendeleo endelevu kwa ajili ya wote kwa siku za usoni na kwamba, hakuna mtu yeyote anayepaswa kuachwa nje ya mkakati huu.

Hapa kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana kwa karibu zaidi sanjari na kudhibiti utakatishaji wa fedha chafu pamoja na kodi stahiki kulipwa kutoka kwa Makampuni makubwa, ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu. Ukwepaji wa kodi unaojikita katika rushwa na ufisadi ni kati ya mambo yanayoendelea kukwamisha maendeleo kwa nchi changa zaidi.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Bernadito Auza, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anasema, bado Jumuiya ya Kimataifa inakabiliwa na changamoto kubwa za umaskini na baa la njaa licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia. Changamoto hizi hazina budi kufanyiwa kazi baada ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Kimataifa kwa mwaka 2015. Kuna haja pia ya kuwa ni mbinu na mikakati shirikishi kwa wananchi kutoka nchi changa zaidi duniani katika uchangiaji wa mchakato wa maendeleo duniani sanjari na kuwajengea uwezo wa kiuchumi.

Umaskini na baa la njaa ni mambo ambayo yanapaswa kushughulikiwa kikamilifu na kamwe hayawezi kuchiwa mikononi mwa soko la kimataifa ili kuamua hatima yake. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yasaidie kufikia mafao ya wengi, kwa kujikita katika kanuni maadili, mshikamano na haki jamii inayoambata pia utashi wa kisiasa. Wanawake na wasichana washirikishwe katika kupanga, kuamua na kutekeleza sera na mikakati ya maendeleo endelevu.

Askofu mkuu Auza anasema ujumbe wa Vatican katika mkutano huu wa Addis Ababa kwamba, kuna haja kwanza kabisa kukusanya nguvu ili kupata rasilimali fedha; pili kuwa na sera na mikakati shirikishi katika masuala ya uchumi na utunzaji bora wa mazingira na tatu ni kuwa na vigezo vitakavyosaidia kupima matokeo ya maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano huu. Ni matumaini ya ujumbe wa Vatican kwamba, maamuzi yaliyofikiwa mjini Addis Ababa hayatabaki kwenye makaratasi bali yatasaidia mchakato wa kupambana na umaskini na baa la njaa duniani, ili kupata maendeleo endelevu, usawa pamoja na ushirikishwaji wa wote pamoja na kupania kuleta maendeleo ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.