2015-07-16 15:39:00

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 16 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa


Tunaendelea na tafakari yetu ya kila Dominika na leo tuko tayari Dominika ya XVI ya mwaka B wa Kanisa. Mama Kanisa, katika masomo ya Dominika hii anatufundisha juu ya wajibu wa kuwa wachungaji: wema, watakatifu, wachapakazi na wa kweli kama Bwana alivyofanya na alivyokuwa, ndiyo kusema kuwajibika ili Kondoo wasibaki bila mchungaji.

Katika somo la kwanza toka kitabu cha Nabii Yeremia, Mungu kwa njia ya Nabii anawakemea wachungaji wanaoharibu na kutawanya kondoo wa malisho yake. Nabii anawakemea viongozi wa siasa akiwaambia waachane na matendo yao maovu vinginevyo atawapatiliza katika matendo yao hayo. Anawaalika wawe watu mfano, yaani waishi na waoneshe wema na utu mbele ya watu, ndiyo kutenda haki katika yote kwa ajili ya watu. Baada ya karipio la Mungu kuna ahadi kwa watu wake yaani anaahaidi kuwakusanya toka katika matawanyiko yaliyosababishwa na wachungaji wabaya na kuwatunza katika mazizi na malisho ya majani mabichi.

Mungu anawahaidi kuchipua katika ukoo wa Daudi mchungaji mwema ambaye atatenda kwa hekima na haki siku zote na atarudisha amani na usitawi wa taifa. Unabii huu umetimilika katika Agano Jipya kwa kuja kwake Mwana wa Mungu. Hata hivyo yafaa kukumbuka kuwa Mwana wa Mungu hatatumia mabavu bali nguvu ya kimungu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Ataunda ufalme wa haki na amani ambao si ufalme wa dunia hii bali ufalme wa Mbinguni. Nini wajibu wetu hivi leo? Je hivi leo, kuna hali kama ilivyokuwa wakati wa Nabii Yeremia?

Mpendwa, hali ya dhuluma na uharibifu wa kondoo na malisho yake ni jambo ambalo siku kwa siku linazidi kukomaa. Uchakachuaji wa mali ya umma na utendaji mbovu katika ngazi zote za kijamii na kiserkali, kivyama unajionesha wazi. Ukosefu wa mwelekeo dhabiti na dira safi ya uongozi ni chakula cha kila siku!

Mpendwa, wajibu wako ni kutazama upya wito wako wa ubatizo na kipaimara na kujidhatiti katika kusimama kidete dhidi ya madhulumu dhidi ya IMANI, dhidi ya haki kwa njia ya kuishi kweli za Injili. Wakati wetu huu ni wakati ambao unatudai kufikiri, kusali na kutafakari zaidi kabla ya kutenda.

Katika somo la Pili toka barua ya Paulo kwa Waefeso, habari njema inatujia kwa njia ya Damu Takatifu ya Yesu. Kwa tendo la kumwaga Damu yake msalabani wale wote waliokuwa wametengwa kwa sababu ya tamaduni, sheria na vizingiti mbalimbali sasa wako pamoja na Bwana katika jamii moja ya Wakristo. Kwa njia ya sadaka ya Yesu Msalabani uadui uliokuwepo kati ya mataifa umebomolewa na sasa sote ni wana wa Mungu. Kumbe, Kristo ni mpatanishi na mjenzi wa amani katikati ya watu akiondoa mipaka ya rangi, ukabila, na tabia nyinginezo ziletazo migogoro katika jamii. Wajibu wako mpendwa unayefuatilia tafakari hii ni kuweka katika matendo mausia ya Bwana na kuishi kweli kikombe cha mateso ya Bwana.

Mpendwa mwana wa Mungu, sehemu ya Injili ya Marko yatufundisha juu ya wajibu wa kuwahudumia watu yaani kuwalinda, kuwachunga na kuwasaidia kiroho ili waweze daima kujisikia wana wa Mungu kweli. Katika kazi ya kichungaji kuna kuchoka na kuzidiwa shughuli, lakini hakuna kukata tamaa. Tunapata mfano wa mchungaji mwema katika Bwana mwenyewe ambaye anawalisha watu Neno lake, anawajibika wakati wote chamsingi kuna watu, na wako katika mahitaji.

Jambo hili linaendelezwa na Mitume na hivi Mama Kanisa atualika daima sisi sote tuliobatizwa katika Utatu Mtakatifu kutenda kazi ya uchungaji usiku na mchana ili kondoo hata siku moja wasikose malisho mema. Kwa namna ya pekee makasisi mnaalikwa kujikita zaidi katika utume ili taifa la Mungu lilishwe kwa Neno la Mungu na sakramenti za wokovu na kwa namna hiyo, siku moja likilimiwe uzima wa milele.

Mpendwa ninakuombeeni mapendo kwa Mungu, ukaimalike katika uchaji na moyo wa kitume ukichuchumalia yaliyo ya juu ambayo ndiyo matunda ya ufufuko. Tukutane tena siku na wasaa kama huu Dominika ijayo. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.