2015-07-16 09:09:00

Fuata nyuki ule asali kwani mshahara wa manyigu ni kung'atwa!


Ukipiga darubini ulimwenguni unapata picha ya sokoni penye mtimbwiliko wa watu, au kama vile kituo cha usafiri penye pilikapilika za watu. Watu wengi wanahangaika kutafuta maisha. Wakisikia mijini kuna nafuu ya maisha wanakimbilia huko. Wakisikia mahala kuna machimbo watamiminikia huko. Wakisikia kazi ya kuuza mkaa inalipa wanaingia misituni kuchoma mkaa. Wanaposikia eti uigizaji wa filamu au Muziki wa Injili una kipato basi watamwagikia huko. Wakigundua kuwa kilimo cha tangawizi kinalipa hapo wengi wanaanza kulima tangawizi.

Vijana wamegundua kuendesha bodaboda au bajaji hasa toyo kuna kipato basi wengi wamejazana huko. Wajasiliamali wa u-cd wakisikia mradi huo unalipa, hapo wengi watayumbia huko. Siyo ajabu anapotokea kiongozi fulani anayeahidi kuwapa watu nafuu ya maisha au “kuwajaza mapesa” hasa kama amewalambisha mkono kidogo, watu wengi watamfuata na kumshabikia, hata watamtungia na kumwimbia nyimbo na mashairi! Ama kweli maisha ni pilikapilika ya kutafuta utulivu na maisha mazuri.

Hali ya pilikapilika kama hizo ndiyo inayoelezwa katika fasuli ya Injili ya leo kwa maneno machache: “kulikuwa na watu wengi, wakija, wakienda hata haikuwapo nafasi ya kula.” Kabla ya kuziona pilikapilika hizo na mapendekezo muhimu yanayoweza kutupatia utulivu wa maisha tuyaone kwanza mazingira ya awali ya fasuli hii.

Wiki iliyopita Mitume walitumwa wawiliwawili kwenda kuhubiri Habari Njema na sasa wamesharudi. Baada ya “kutoa ripoti ya mambo waliyoyafanya na waliyoyafundisha” Yesu anawaambia: “Njoni ninyi peke yenu pahala pa faragha, mahali pasipokuwa na watu mkapumzike kidogo,” Neno la Kigiriki lililotumika ni heremon, lenye maana ya jangwa (heremo) walikokuwa wanakaa wamonaki – Waeremiti – walioacha malimwengu ili kumtafakari Mungu. Hivi Yesu anawaambia mitume wake wajitenge kidogo na kazi ya kichungaji na kukaa na kutulia pamoja na mwalimu wao. 

Desturi ya namna hii ilikuwa ni ya kawaida kabisa kwa Wayahudi, kwamba kipindi fulani walimu huwa pahali pa faragha pamoja wanafunzi wao. Hali hiyo ya wanafunzi kujitenga pamoja na mwalimu ilikuwa ni nafasi huru ya kujilegeza, ya ”kujibinafasi” au ”kujihyeka” na ”kujihyehela”. Ilikuwa ni fursa nzuri ya wanafunzi kufahamiana kiundani na kiumwandani zaidi na Mwalimu wao.

Kumbe, katika Biblia ukisikia kupumzika, palieleweka kuwa ni pamoja tu napo ni Nchi ya Ahadi (Nchi Takatifu). Waisraeli baada ya shuruba za utumwani Misri na pilikapilika za jangwani kwa takribani miaka arobaini wakafanikiwa kuingia nchi ya ahadi, yaani nchi ya mapumziko na ya raha. Ndiyo maana baada ya kuingia nchi ya ahadi, Yoshua akawaambia: ‘Likumbukeni Neno lile alilowaamuru Musa mtumishi wa Bwana, akisema, Bwana Mungu wenu, anawapa ninyi raha (mapumziko), naye atawapa nchi hii’” (Yoshua 1:13). Naye Salomoni anasali, “Na ahimidiwe Bwana, aliyewapa watu wake Israeli kustarehe vilevile kama yote aliyoyaahidi.” (I Wafal. 8:56). Kadhalika katika zaburi juu ya mchungaji, kuna kupumzika na kuwa na furaha ya kukaa pamoja na Bwana. “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu, mbele ya malisho mabichi atanipumzisha.” (Zab. 23:1-2). Hii ni furaha ya kukaa pamoja na Bwana, ya kuwa na amani ya roho, utulivu na furaha ya kuwa  wewe mwenyewe.

Kwa hiyo, Yesu anawatakia wafuasi wake furaha hiyo ya kupumzika na kutulia na kuwa katika umwandani na Mungu. Anawaambia wanafunzi wake “Twendeni pahala pa pekee pa kupumzika.” Wakaingia katika mashua yaani katika maisha ya jumuia au maisha ya kanisa. Kumbe, mapumziko yanaanza unapokuwa na Yesu ndani ya jumuiya (mashua) na mnaposafiri pamoja na Yesu kuelekea pahala pa ahadi, pahala pa furaha amani na utulivu wa ndani.

“Watu wakawaona Mitume wakienda zao na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu.” Yaonekana watu waliwashtukia mitume walivyokuwa wanaondoka na Yesu, wakatambua kuwa huko waendako kuna dili, yaani kuna lengo linaloeleweka. Kwa hiyo, wakavutika kuwafuata kwa miguu. Yaonekana watu hawa waligundua kuwa kuna kitu kizuri kinachofanyika katika jumuiya hii ya Mitume, na hivi sasa wameondoka kwenda kufaidi peke yao, ni afadhali kuwakimbilia maana “Fuata nyuki ule asali na mshahara wa manyigu ni kung’atwa.” Kwa hiyo, endapo Mitume waliambiwa wajitenge pahala pa faragha peke yao kupumzika, basi yaonekana watu hawa walikuwa katika pilikapilika za maisha wakienda na kurudi bila malengo. Hivi watu hawa walikuwa wanatafuta amani, utulivu na umaana wa utu wa maisha.

Kumbe, katika mazingira ambayo jumuiya hii mpya ya mitume inapojitenga na kupata utulivu kuna watu wengine wanaotafuta utulivu na wanavutika nayo. Watu hawa, wanakimbia mbio hadi wanawatangulia Mitume kufika waendako. Hapa tunajifunza kwamba, wakati mwingine watu wa kawaida wanatangulia kuelewa mambo kwa haraka zaidi ya Mitume au wachungaji. Huu ndio ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha Uinjilishaji mpya!

“Naye (Yesu) aliposhuka mashuani akaona mkutano mkuu akawahurumia.” Yawezekana aliwaonea huruma kwa vile hawakuelewa wanachotaka, au pengine walifika hapo kwa ushabiki tu. Yaonekana walikata matumaini na walikuwa na njaa ya kuelewa mambo muhimu ya maisha,  ndiyo maana Yesu anaanza kuwafundisha mambo mengi: “anawaona kuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi.”

Yesu anatufundisha wafuasi wake wote tabia ya kutoa kipaumbele cha kujali na kuwaonea watu huruma na kushughulikia mahangaiko yao. Kwanza amewahurumia Mitume waliotoka kwenye pilikapilika za kichungaji anawatakia kupumzika. Sasa anawaona walala hoi hawa waliomkimbilia na kumtangulia kufika anakotaka kupumzika, anawaonea huruma na kuanza kuwafundisha.

Aidha, anataka kutufundisha kwamba maisha yoyote yale yanaweza kupoteza muungano, na umwandani na Kristo, hivi yabidi daima kuangalia mafundisho na kazi zako zote zina msingi upi. Zaidi tena katika matendo mema unayofanya huna budi kuyaunganisha na lengo la Mwalimu, ili yaongozwe na Neno lake, yaani kuunganisha maisha yako na Kristo, na kutafuta amani ya roho.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.