2015-07-16 15:15:00

Elimu ya dini shuleni ni muhimu sana kwa ajili ya kuwafunda wanafunzi maadili!


Askofu mkuu Alfred Martins wa Jimbo kuu la Lagos, Nigeria wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika iliyoadhimishwa hivi karibuni Barani Afrika, amesikika akisema kwamba, kuna haja kwa Serikali ya Nigeria kurudisha tena elimu ya dini shuleni, ili kusaidia kuwafunda watoto katika malezi bora, dhidi ya mmomong’onyoko wa kimaadili unaoendelea kuikumba jamii kwa kasi ya ajabu.

Askofu mkuu Martins anasema, kuna haja kwa viongozi wa Serikali kufanya tafakari ya kina, ili kuangalia ustawi na maendeleo ya watoto nchini Nigeria: kiroho na kimwili, tayari kufanya maamuzi machungu ili kusaidia kurekebisha mmong’onyoko wa maadili unaoendelea kuzinyemelea familia nyingi nchini Nigeria. Hii inatokana na ukweli kwamba, vijana wamekuwa wakiiga mambo mengi kutoka kwenye mitandao ya kijamii kiasi cha kuchanganyikiwa katika maisha, kuna tatizo kubwa la ukosefu wa ajira linalowapelekea baadhi ya vijana kujiunga na makundi ya watu wenye misimamo mikali, wakidhani kwamba, huko watapata ujira wa kuweza kujikimu maisha.

Mpasuko wa kijamii ni mambo ambayo pia yanachangia kuwa na kundi dogo la watu wenye nguvu ya kiuchumi, wakati ambato kuna bahari ya watu inaendelea kuogelea katika umaskini wa hali na kipato, matokeo yake ni vijana kukengeuka na hatimaye kupotoka kimaadili na iutu. Mfumo wa elimu nchini Nigeria unakabiliwa na changamoto nyingi kiasi kwamba, umefika wakati wa kufanya mabadiliko ya dhati, ili wanafunzi waweze kuandaliwa kikamilifu katika kutekeleza majukumu ndani ya jamii katika ujumla wao.

Kuna haja ya kukazia, kanuni maadili, uzalendo, umoja na mshikamano wa kitaifa, mambo ambayo kwa sasa yanalega lega kutokana na watu wengi kujikita katika udini na ukabila, usiokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wa Nigeria katika ujumla wao. Kanisa kwa upande wake, halina budi kuendelea kuwekeza katika utume wa familia, ili kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kweli familia ziweze kutekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa na jamii.

Askofu mkuu Martins anaitaka Serikali ya Nigeria kuwekeza zaidi katika somo la maadili na dini shuleni, ili jamii iweze kuwaunda wananchi na viongozi wanaosimamia: misingi ya haki na amani; ukweli na uaminifu; pamoja na kukuza ndani mwao uzalendo na uchaji wa Mungu, mambo msingi katika ustawi na maendeleo ya mtu: kiroho na kimwili.

Askofu mkuu Martins anaendelea kusema kwamba, kuna idadi kubwa ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wengine wengi wamebaki yatima kutokana na mashambulizi yaliyokuwa yanafanywa na Boko haram. Hili ni kundi ambalo linahitaji kuangaliwa kwa namna ya pekee, vinginevyo, matumaini yao kwa siku za usoni, yanaweza kusambaratika na hatimaye, kuwa ni kundi la hatari nchini Nigeria. Watoto na vijana wa kizazi kipya wafundwe barabara katika maisha adili na matakatifu, ili kweli waweze kuwa ni wananchi wema na watakatifu, wanaoweza kushiriki katika mchakato wa ujenzi na ustawi wa Nigeria. Kwa namna ya pekee kabisa, Askofu mkuu Martins wa Jimbo kuu la Lagos, Nigeria anawataka watoto na vijana kuiga mfano wa bora wa Yesu katika maisha na makuzi yao, kwa kuonesha heshima, utii na unyenyekevu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.