2015-07-15 10:38:00

Wajibu na mshikamano ni mambo msingi katika mapambano dhidi ya Ebola


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushikamana kwa dhati ili kupambana vyema na janga la ugonjwa wa Ebola Barani Afrika kwa kuimarisha miundo mbinu na huduma ya afya katika maeneo ambamo ugonjwa wa Ebola bado ni tishio kubwa kwa maisha na usalama wa wananchi. Hayo yamesemwa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernadito Auza, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, wakati alipokuwa anashiriki kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu mbinu mkakati wa kupambana na ugonjwa wa Ebola, tukio ambalo limefanyika, huko New York, Marekani.

Vatican katika matukio mbali mbali, imeendelea kuonesha mshikamano wa dhati na wananchi wanaoathirika na ugonjwa wa Ebola sehemu mbali mbali za dunia; kama alivyofanya Baba Mtakatifu Francisko kwenye hotuba yake kwa Mabalozi na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao mjini Vatican kunako mwaka 2015. Wakati huo, Baba Mtakatifu aliwaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanatoa huduma makini kwa waathirika wa ugonjwa wa Ebola pamoja na kukusanya nguvu ili kupambana na janga la ugonjwa wa Ebola.

Askofu mkuu Auza amebainisha mchango wa Kanisa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola, kwa kusema kwamba, Kanisa limekuwa mstari wa mbele kutoa msaada wa hali na mali kwa waathirika wa ugonjwa wa Ebola pamoja na familia zao. Kanisa limesaidia kuondokana na dhana ya kuwatenga wagonjwa wa Ebola, hali ambayo ilikuwa inawaongezea upweke na kwamba, kwa sasa Kanisa linaendelea kutoa huduma kwa watoto waliobaki yatima baada ya wazazi wao kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola.

Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na Vatican yamekuwa yakitoa msaada mkubwa kwa waathirika wa ugonjwa wa Ebola. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alichangia kiasi cha Euro Laki tano, ili kusaidia mchakato wa huduma makini kwa waathirika wa ugonjwa wa Ebola.

Katika mkutano huu, Jumuiya ya Kimataifa imefanikiwa kukusanya kiasi cha Dolla za Kimarekani billioni tatu na millioni mia nne, ili kupambana na ugonjwa wa Ebola duniani. Kwa mchango huu mpya, Umoja wa Mataifa kwa sasa una jumla ya kiasi cha Dolla za Kimarekani billioni 5, 18 kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ebola na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kupambana kweli na ugonjwa huu ambao umekuwa ni tishio kubwa kwa maisha na maendeleo ya watu, hususan huko Afrika Magharibi, anasema Alpha Condè, Mwenyekiti wa mkutano huu.

Zaidi ya wagonjwa elfu kumi na moja huko Afrika Magharibi wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola na kwamba, bado ugonjwa huu unatishia maisha ya watu wengi! Athari za ugonjwa wa Ebola zinajionesha katika sekta ya elimu, maisha ya kijamii, kiuchumi na kibiashara. Kumbe, kuna haja kwa wananchi kuendelea kuwa macho dhidi ya ugonjwa wa Ebola na kamwe wasifanye mzaha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.