2015-07-15 15:10:00

Vigogo wakuna vichwa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na utumwa mamboleo


Mameya kutoka katika majiji makuu duniani wanaoshiriki katika Warsha ya siku mbili kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 22 Julai 2015 mjini Vatican, wanaongozwa na kauli mbiu “Utumwa mamboleo na mabadiliko ya tabianchi: dhamana ya majiji” pamoja na “Ustawi, watu na dunia: namna ya kupata maendeleo endelevu kwenye majiji”. Warsha hii imeandaliwa na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii inayopania kuwashirikisha Mameya katika mchakato wa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na kupambana na utumwa mamboleo; mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Kwa ufupi, Mameya hawa wanasema, wanapenda kuunga mkono juhudi za Baba Mtakatifu Francisko katika mapambano dhidi ya umaskini kwa kuwashirikisha watu katika sera na mikakati ya maendeleo; kwa kuanzisha fursa za ajira na kukuza vyanzo vya mapato; ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Mameya wanapania kulinda mazingira kwa kuwa na sera makini zaidi na nishati rafiki.

Ili kusimama kidete katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo, kuna haja wanasema Mameya kwa wadau mbali mbali kushirikiana na kushikamana kwa pamoja, ili kutokomeza uhalifu huu dhidi ya binadamu kwa kutetea: utu na haki msingi za binadamu. Ni wajibu wa wananchi wenyewe kutoka kifua mbele ili kusimama kidete dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kukazia usawa na maendeleo kati ya watu.

Jamii iwekeze zaidi katika mipango miji, sheria na kanuni za utunzaji bora wa mazingira kwa mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Utunzaji wa nyumba ya wote ni dhamana na wajibu wa kila raia ili kupambana na madhara yanayotishia ustawi na maendeleo ya binadamu kwani maendeleo endelevu yanajikita katika misingi ya haki, amani na utulivu na kwamba, mazingira na maisha ya mwanadamu ni mambo yanayotegemezana na kukamilishana.

Athari za mabadiliko ya tabianchi ni janga la kimataifa linalopaswa kushughulikiwa katika ngazi mbali mbali kwa kuwahusisha watu wote katika kulinda mazingira na kupambana na umaskini. Uhusiano huu hauna budi kujikita katika misingi ya ukweli na uwazi, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Kuwepo na mikakati makini ya kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa kuwa na usafiri wa umma unaoaminika.

Uchafuzi wa mazingira na utumwa mamboleo ni kati ya changamoto kubwa zinazoendelea kuikabili miji mikuu na kwamba, ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kufanikisha azma yake, kuna haja pia ya kuwashirikisha viongozi wa kidini, kisiasa na vyama vya kiraia. Warsha hii wanasema Mameya wa miji ni fursa pia ya kubadilishana uzoefu na mang’amuzi na sera mbali mbali zilizokwishafanyiwa kazi na matokeo yake kuonekana na wengi.

Lengo ni kuwahusisha na kuwajengea wananchi uwezo wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi sanjari na kusimama kidete kupinga utumwa mamboleo kwa kutetea utu na heshima ya binadamu. Wananchi wajivunie utunzaji bora wa miji yao. Teknolojia rafiki na ushirikiano kati ya miji mbali mbali anasema Mstahiki Ignazio R. Marino, Meya wa Jiji la Roma ni muhimu sana katika utunzaji bora wa mazingira. Wananchi wana haki ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko haya kwani hii ni changamoto kwa wakati huu na kwa ajili ya kizazi kijacho.

Warsha hii inatarajiwa kuibua sera na mbinu mkakati wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na kukomesha utumwa mamboleo. Ubinafsi na uchoyo umepelekea maeneo ya wazi kubinafishwa na baadhi ya watu ndani ya jamii; mambo ambayo yana athari kubwa katika utunzaji bora wa mazingira. Wahanga wengi wa utumwa mamboleo ni matokeo ya athari za mabadiliko ya tabianchi, mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee, kwa njia ya ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kisiasa, kwa kujikita katika kanuni maadili, utu wema na maendeleo ya wengi.

Athari za mabadiliko ya tabianchi kwa hakika ni kati ya changamoto kubwa kwa nyakati hizi na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika kadiri ya uwezo na nafasi yake, ili kupunguza uchafuzi wa mazingira. Watu wakiungana na kushikamana, sera na mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa inaweza kutekelezwa na mafaniko kuonekana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.