2015-07-15 15:25:00

Utu na heshima ya binadamu vinagusa kanuni maadili!


Utu na heshima ya mwanadamu katika majadiliano ya haki msingi za binadamu ni dhana inayoendelea kushika kasi kubwa katika medani mbali mbali za Jumuiya ya Kimataifa. Hiki kimekuwa ni kigezo na kanuni maadili katika majadiliano miongoni mwa watu binafsi na hata katika ngazi za kimataifa. Utu na heshima ya binadamu ni mambo ambayo yangusa undani wa mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; anayepeswa kuheshimiwa na kulindwa tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Utu wa mtu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu isiyokuwa na mbadala inayomwajibisha mwanadamu kutambua kwamba, yeye ni kiumbe jamii anapaswa kushirikiana na kushikamana na wengine katika haki, amani na upendo. Utu wa mwanadamu unagusa kanuni maadili hauwezi kupimwa kwenye maabara, bali unapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote. Sayansi ina wajibu wa kuhakikisha kwamba, inasaidia kudumisha na kuendeleza utu na heshima ya binadamu na wala si kinyume chake.

Ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernadito Auza, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, wakati alipokuwa anachangia kuhusu utu na heshima ya binadamu mintarafu afya ya uzazi kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Utu na heshima ya binadamu vinapaswa kuangaliwa kwa upendo mkuu, kwa kuwaheshimu wanawake wajawazito na kutambua mchango wao katika kutunza mimba, kulea na kuzaa watoto.

Baadhi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya uzazi hayaheshimu utu wa mwanamke na matokeo yake ni kuona mimba kama ugonjwa unaopaswa kunyofolewa kwa gharama yoyote ile! Mwili wa mwanamke unakuwa ni chombo cha kufanyia majaribio na kwamba, kuna baadhi ya wahudumu wa sekta ya afya wanataka kujitajirisha kwa njia ya sera zinazokumbatia utamaduni wa kifo, badala ya kusaidia kuimarisha mapendo kati ya bwana na bibi ili kulinda na kutunza zawadi ya maisha.

Wanawake waheshimiwe kwa dhamana na wito wao wa kubeba, kulea na kutunza mimba. Kamwe wanawake wasitumiwe kuwa ni “maabara ya kutungia mimba” kama biashara. Wanaume nao wanapaswa kutambua dhamana na wajibu wao na katika mchakato wa kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu, kushiriki na kuuendeleza. Inasikitisha kuona kwamba, leo hii wanawake na wanaume wanageuzwa kuwa ni vyombo vya biashara katika uzalishaji kwa njia ya chupa kwenye maabara.

Lakini watoto wanapaswa kutungwa katika mchakato wa upendo kati ya bwana na bibi wanaposhiriki tendo la ndoa na wala si watoto kuzaliwa kwenye maabara. Watoto ni watu wenye utu na heshima yao na wala si bidhaa inayoweza kuuzwa au kununuliwa sokoni. Tabia hii inakumbatia pia utamaduni wa kifo, jambo ambalo linakwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu. Ikumbukwe kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Wanandoa wasaidiwe kufahamu mpango wa uzazi kadiri ya mfumo wa miili yao yaani mpango wa uzazi kwa njia ya asili “Billing Ovulation Method”. Inayoheshimu utu  wa mwanamke, mwanaume na mtoto ambaye ni matunda ya upendo kati ya bwana na bibi. Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, ili kamwe asigeuzwe kuwa ni bidhaa wala kichokoo cha majaribio ya kisayansi na tamaa ya fedha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.