2015-07-15 14:58:00

Msibeze uhuru wa kuabudu kwani hii ni rasilimali muhimu sana kwa binadamu!


Uhuru wa kuabudu ni kati ya changamoto kubwa zinazoendelea kuikabili Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu katika ngazi ya kitaifa na kimataifa kutokana na ukweli kwamba, utamaduni mamboleo unataka kuwaaminisha watu kwamba dini haina maana tena katika ustawi na maendeleo ya binadamu. Watawala wengi wanataka kuhakikisha kwamba, ushuhuda wa imani unaondoshwa katika maisha ya hadhara na kubaki kuwa ni tendo la binafsi, jambo ambalo ni hatari kubwa kwa mwanadamu.

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanachangamotishwa kuhakikisha kwamba katika maisha yao wanamwambata Mwenyezi Mungu, ili kweli aweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao ya kila siku. Hiki ni kielelezo cha kutambua kwamba binadamu ni kiumbe kinachomtegemea Mwenyezi Mungu na kwamba, Jumuiya ya waamini ni jambo muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya binadamu kiroho na kimwili na kamwe haiwezi kubezwa na kutengwa kana kwamba, ni “gari bovu”!

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, waamini wanaheshimu na kudumisha maridhiano, haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu na kamwe dini isigeuzwe kuwa ni chanzo cha kinzani, vita na mipasuko ya kijamii. Haya ni kati ya mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican wakati alipokuwa anachangia mada kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa usalama na maendeleo Barani Ulaya, OSCE. Mkutano huu umefanyika hapo tarehe 10 Julai 2015.

Monsinyo Camilleri amekazia kwa namna ya pekee maafikiano yaliyofikiwa huko Helsinki, miaka arobaini iliyopita na huo ukawa ni mwanzo wa kuzaliwa kwa OSCE, ambalo kwa sasa ni jukwaa linalojikita katika sheria, taasisi, sera na mikakati inayopania kutoa maamuzi msingi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu. Vatican kwa upande wake inapenda kuunga mkono juhudi hizi za kimataifa kama ilivyokuwa katika kipindi cha miaka arobaini iliyopita.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, jamii inajikita katika misingi ya haki na amani inayoshuhudiwa katika uhalisia wa maisha ya watu na wala si amani inayoning’inia kwenye shingo kama tai! Usalama, haki msingi za binadamu; utu na heshima ya binadamu ni mambo msingi katika mchakato unaopania kukoleza na kudumisha ushirikiano na mafungamano ya kijamii yanayojikita katika kanuni auni.

Hii ni nyenzo muhimu sana katika utunzaji bora wa mazingira na utu wa binadamu. Kumbe, uhuru wa kuabudu ni jambo muhimu sana na unaweza kuwa ni rasilimali kwa ajili ya kukuza na kudumisha ustawi na maendeleo ya wengi, huku watu wakiongozwa na dhamiri nyofu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.