2015-07-15 14:40:00

Mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi na utumwa mamboleo


Kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 22 Julai 2015 mjini Vatican kunafanyika Kongamano na Warsha ya kimataifa inayoongozwa na kauli mbiu “Utumwa mamboleo na mabadiliko ya tabianchi: dhamana ya majiji” pamoja na “Ustawi, watu na dunia: namna ya kupata maendeleo endelevu kwenye majiji”. Ni kongamano na Warsha inayowashirikisha mameya kutoka majiji makuu duniani; viongozi wa serikali za mitaa na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, ambao wanataka kushirikishana mbinu mkakati utakaoyawezesha majiji kujifunga kibwebwe kupambana na mabadiliko ya tabianchi sanjari na utumwa mamboleo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Jumatano tarehe 15 Julai 2015 Askofu mkuu Marcelo Sànchez Sorondo; mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii anasema, kwa mara ya kwanza Wastahiki Mameya kutoka katika majiji makuu duniani wamealikwa mjini Vatican ili kushirikishana mawazo, sera na mikakati ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na utumwa mamboleo unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Kongamano hili ni mwendelezo wa juhudi za pamoja zilizoanzishwa hivi karibuni kwa kushirikiana na wakuu wa Jeshi la Polisi kutoka katika nchi mbali mbali pamoja na Maaskofu Katoliki ili kujikita katika kanuni maadili kwa ajili ya kuwalinda na kuwatetea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamiii. Dhamana hii inatekelezwa kwa umakini mkubwa na Mameya wa majiji kwani hawa ndio viongozi wakuu wa wananchi katika maeneo yao ya kujidai katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi pamoja na utumwa mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote anasema, mazingira ni kito cha thamani kwa ajili ya wote na kwamba, mazingira yana uhusiano wa pekee na maisha ya binadamu. Ongezeko la kiwango cha joto duniani linaendelea kusababisha ongezeko la kina cha maji ya bahari; ukame na mafuriko; dhoruba pamoja na majanga asilia. Hapa mwanadamu anahamasishwa kubadili mtindo wa maisha na maendeleo, kwa kuambata teknolojia rafiki kwa mazingira.

Madhara ya mabadiliko ya tabianchi anasema Baba Mtakatifu Francisko yamepekea baadhi ya watu kutumbukizwa katika utamaduni wa kutopea kwa imani, kutukuzwa kwa malimwengu na ubaridi wa imani mambo yanayoendelea kusababisha baadhi ya watu kutumbukizwa katika utumwa mamboleo na kazi za suluba; tatizo la kuwatelekeza wazee na kuwanyanyasa watoto, kwa mafao ya mtu binafsi.

Kumbe, kuna uhusiano wa karibu kati ya athari za mabadiliko ya tabianchi na kukengeuka kwa binadamu, changamoto ya kuambata kanuni maadili na utu wema kwa ajili ya mafao ya wengi. Mameya wa miji wanayo dhamana kubwa kutokana na ukweli kwamba, kuna ongezeko kubwa la watu wanaohamia mijini ili kutafuta riziki ya maisha. Mahusiano ya dhati kwa ajili ya mafao ya wengi anasema Askofu mkuu Sorondo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya mipango miji, ili kulinda, kutetea na kudumisha maisha ya mwanadamu. Hii ni dhamana ya kimaadili inayoheshimu na kuzingatia utunzaji na maendeleo ya nyumba ya wote.

Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni kundi ambalo linaathirika sana kutokana na mabadiliko ya tabianchi, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kutumia vyema maendeleo ya sayansi na teknolojia katika mapambano dhidi ya umaskini; kwa kujikita katika maendeleo endelevu; haki na amani pamoja na utunzaji bora wa mazingira kwa kudhibiti uchafuzi wa mazingira kutokana na uzalishaji wa hewa ya ukaa.

Ni matumaini ya Vatican kwamba, mameya wataweza kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao kwa kuhakikisha kwamba,  wanasiamama kidete, kulinda na kutunza mazingira; kwa kutunga sera makini katika masuala ya kiuchumi na kisiasa; kwa kuonesha ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi sanjari na kupambana kufa na kupona na biashara haramu ya binadamu.

Wahanga wa utumwa mamboleo wasaidiwe kuanza tena maisha mapya katika ngazi mbali mbali na kwamba, majiji na miji iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha mfungamano wa kijamii, usalama na utunzaji bora wa mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.