2015-07-15 08:56:00

Aliyekamatwa na "vigunia vya fedha Dodoma" arudishiwa fedha zake!


Ifuatayo ni taarifa ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kuhusu sakata la vigunia vye fedha vilivyopatikana Dodoma wakati wa mchakato wa mkutano mkuu wa 10 wa CCM, Dodoma: Napenda kutoa taarifa fupi kuhusu tukio lililotokea tarehe 11/07/2015 majira ya saa 10:00 hrs huko katika Hoteli ya St. Gasper hapa mjini Dodoma, kuwa wananchi walitoa taarifa majira ya saa 10:00 hrs kwamba kuna mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia amekamatwa na wananchi akiwa na fedha nyingi na kuna vurugu kubwa. Baada ya kupata taarifa hizo Jeshi la Polisi Mkoani hapa lilifika eneo la tukio ili kuona kama taarifa hizo ni za kweli.

Askari walithibitisha kuwa ni kweli walimkuta mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia ambaye alijulikana kwa jina la AMIT KEVALRAMANI mwenye umri wa miaka 31, Mhindi, Mfanyabiashara, Mkazi wa Dar es Salaam akiwa na fedha kiasi cha Tshs. 722,500,000/= ambacho alipohojiwa alisema kuwa tarehe 10/07/2015 alifika Dodoma kwa ajili ya ununuzi wa mazao ya nafaka. Alipofika Dodoma tarehe 10/07/2015 majira ya asubuhi alifikia katika Hoteli ya St. Gasper na tarehe 11/07/2015 aliamua kurudisha fedha benki kutokana na kuona mkusanyiko wa watu wengi wasioeleweka na wenye viashiria vya vurugu.

Akiwa katika harakati ya kurejesha fedha hizo benki, ndipo kundi la watu waliokuwa katika eneo la Hoteli ya St. Gasper walimtilia mashaka na kumzuia asiondoke na ndipo taarifa zilitolewa polisi. Mashaka ya watu hao yalitokana na vuguvugu za kisiasa/mchakato wa uchaguzi kati ya makundi mbalimbali kuwa kuna watu wanahonga wajumbe. Taarifa za aina hiyo ambazo hata Jeshi la Polisi lilikuwa limepokea bila uthibitisho.

Katika tukio hili na uchunguzi tulioufanya tumebaini kuwa hakuna kosa la jinai lililothibitika licha ya kukutwa na kiasi hicho cha fedha, tuhuma za rushwa ambazo ndiyo zilikuwa msingi wa ukamataji wa mtu huyo hazikuthibitika, kwa kuwa hakuna aliyeona akizigawa fedha hizo wala hakuna aliyedai kushawishiwa au kugawiwa fedha hizo. Aidha imethibitika fedha hizo ni mali yake halali na kwa kuwa hakuna ushahidi mwingine uliyo thibitisha vinginevyo amerejeshewa fedha zake.

Aidha tarehe 10.07.2015 majira ya saa 21:00 eneo la Railway Dodoma tulifanikiwa kuwakamata:-

1. HERERIMANA METHODE, MIAKA 21.

2. HATUNGIMANA ALEXIS, MIAKA 20.

3. NIYONGABO JUSTIN, MIAKA 20.

4. NTETURUYE ONESPHORE MIAKA 21.

5. BIKORIMANA LEVIS, MIAKA 21 wote ni Wakazi wa Mabanda Burundi kwa kosa la kuingia nchini na kuishi nchini bila kibali.

Watuhumiwa hawa walikuwa wanasafiri na treni kuelekea Dar es Salaam na walipofika Dodoma Askari wanaosindikiza treni waliwashtukia na walipowakamata na kuwahoji walijieleza kuwa ni raia wa Burundi. Tunaomba ushirikiano wa wananchi pale wanapoona watu ambao siyo raia wasiwakaribishe bali watoe taarifa kwa vyombo vya dola waweze kuhojiwa kwani hata kama waliingia Nchini na kuhifadhiwa katika makambi yaliyopo Nchini hawaruhusiwi kutoka kwenda mbali na kambi zao bila kuwa na kibali maalum.

Na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma.


 








All the contents on this site are copyrighted ©.