2015-07-14 10:49:00

Vijana wa Paraguay washerehekea Injili ya Furaha, Matumaini na Mapendo!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni tarehe 12 Julai 2015 alikamilisha hija yake ya kitume nchini Paraguay kwa kusherehekea Injili ya Furaha na matumaini pamoja na vijana kutoka ndani na nje ya Paraguay. Katika tafakari yake baada ya kusikiliza shuhuda zilizotolewa na vijana kutoka Paraguay, Baba Mtakatifu amekazia mambo kadhaa yanayopaswa kuwa ni dira na mwongozo wa vijana katika hija ya maisha yao ya imani na matumaini.

Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kuwa na moyo huru usiotingwa na malimwengu; umoja na mshikamano wa kidugu; matumaini kwa Yesu Kristo mkombozi wa dunia sanjari na kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni marafiki wa Yesu.

Mkutano wa Baba Mtakatifu Francisko na vijana ulipambwa kwa nyimbo na muziki, ulioshuhudiwa na vijana waliotaka kushirikisha ile Furaha ya Injili pamoja na kuendelea kusimama kidete kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kiinjili zikimwilishwa katika uhalisia wa maisha yao, kama walivyoshuhudia wao wenyewe. Ni vijana wanaowahudumia wazazi wao wagonjwa; wengi wao ni vijana ambao wameguswa na kutikiswa na umaskini na hali kutelekezwa na wazazi wao, lakini bado wana imani na matumaini katika maisha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, uhuru wa kweli ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambayo inapaswa kupokelewa kwa imani na matumaini, tayari kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Vijana wajitahidi kuwa na moyo huru usiozingirwa na malimwengu ambayo yanaweza kuwatumbukiza katika: unyonyaji, umaskini na utumwa mamboleo; matumizi haramu ya dawa za kulevya; upweke hasi na majonzi moyoni.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kumwomba Yesu ili aweze kuwakirimia moyo huru dhidi ya vishawishi vya dunia na fahari zake, bali kuwa kijana mwema na mfano wa kuigwa kila wakati. Baba Mtakatifu ametoa tafakari hii baada ya kusikiliza ushuhuda wa Manuel de Los Santos Aguiler, aliyeguswa na kutikiswa na umaskini, dhuluma, nyanyaso na matumizi haramu ya dawa za kulevya alipokuwa mjini. Akaamua kurejea kijijini kwake na huko akakutana na utume wa vijana ambao wamemsaidia kuona mwanga na njia mpya ya maisha.

Baba Mtakatifu amesikiliza kwa umakini mkubwa ushuhuda uliotolewa na Liz Fretes anayemhudumia mama yake mzazi ambaye ni mgonjwa mahututi kitandani pamoja na bibi yake ambaye kwa sasa ni mzee. Shida na magumu haya yamemwezesha kukomaa na kuimarika katika huduma ya upendo kwa jirani na imani kwa Mwenyezi Mungu. Liz anaendelea na utume wake kwa kushikamana na vijana wengine katika utume wa vijana, jambo ambalo Baba Mtakatifu Francisko amelipongeza.

Hakuna sababu ya kukimbia majukumu kama alivyofanya Pontio Pilato, bali kuonesha upendo na mshikamano wa kidugu. Liza anatekeleza ile Amri ya Mungu, waheshimu Baba na Mama yako ili upate miaka mingi na heri duniani. Liza angeweza kuamua “kuchanja mbuga” na kuwaacha wazazi wake wakiteseka, lakini anasukumwa na upendo ndio maana bado anaendelea kuwahudumia kwa furaha na matumaini makubwa. Mshikamano ni ngazi kubwa ya upendo.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, vijana wengi wanapokata tamaa, matokeo yake wanajikuta wakitumbukia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya, utumwa mamboleo na uhalifu mambo ambayo ni hatari kwa heshimana utu wao. Vijana watambue kwamba, Kanisa linapenda kuwasaidia na kuwajengea matumaini yanayojikita katika upendo unaowajibisha. Watmbue kwamba, Yesu ni chemchemi na nguvu katika maisha yao. Vijana wamkimbilie Yesu katika shida na mahangaiko yao ya maisha, ili aweze kuwasaidia kuota mambo makuu katika maisha kwa kujikita katika: imani, matumaini na mapendo; tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.