2015-07-14 15:23:00

Vatican yapokea makubaliano ya nyuklia huko Vienna kwa mikono miwili


Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican, akijibu maswali ya waandishi wa habari mjini Vatican kuhusu mafanikio yaliyopatikana huko Vienna tarehe 14 Julai 2015 kwa Iran kutia sahihi mkataba wa Nyuklia na Kundi la Mataifa sita, kujumlisha moja, yaani Mataifa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, umepokelewa na Vatican kwa mikono miwili. Nchi hizi ni: Marekani, Uingereza, Ufaransa, Russia, China pamoja na Ujerumani.

Padre Lombardi anakiri kwamba, mkataba huu ni muhimu sana na ni wa kihistoria katika makubaliano ya kimataifa; changamoto na mwaliko wa kukusanya na kuendeleza nguvu ya pamoja ili kuweza kupata matunda yanayokusudiwa. Ni matumaini ya Vatican kwamba, mafanikio haya hayatajikita tu kwenye mpango wa udhibiti wa silaha za kinyuklia bali yataendelezwa hata katika nyanja nyingine za maisha.

Majadiliano kati ya nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Iran yamekuwa katika hali tete, ya vuta nikuvute na kwamba, uvumilivu na utashi wa pande zinazohusika zimeiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kufikia hatua hii muhimu katika historia ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huu umekuwa ukifanyika kwa takribani siku 16 sasa. Wachunguzi wa mambo wanasema mkataba huu ni muhimu sana katika mchakato wa kudhibiti ulinzi, usalama na amani, kitaifa, kikanda na kimataifa.

Mkataba huu utaiwezesha Iran kuanza kutumia fedha yake iliyokuwa imezuiliwa kutokana na vikwazo vya kiuchumi na kifedha. Lakini bado vikwazo vya silaha vitaendelea kutumika na kwamba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaendelea kudhibiti mchakato huu. Mkataba huu utakapoanza kutumika, Iran haitakuwa tena na uwezo wa kutengeneza silaha za atomic na ikiwa kama Iran itashindwa kutekeleza mkataba huu, vikwazo vyote vya kiuchumi na kifedha vitarejeshwa mara moja. Huu ni mwanzo wa ukurasa mpya wa kihistoria nchini Iran. Viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa wameonekana kuridhishwa na na hatua iliyofikiwa katika udhibiti wa silaha za nyuklia kutoka Iran. Baadhi ya nchi wanauangalia mkataba huu kwa jicho la "kengeza na wasi wasi mkubwa" mintarafu usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.