2015-07-14 14:10:00

Mheshimiwa Padre Emmanuel Fianu, S.V.D ateuliwa kuwa Askofu wa Ho, Ghana


Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi la kung’atuka kutoka madarakani lililowasilishwa kwake na Askofu Francis Anani Kofi Lodonu, wa Jimbo Katoliki Ho, Ghana kadiri ya sheria za Kanisa namba 401 Ibara 1. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu ameteua Mheshimiwa Padre Emmanuel Fianu, SVD, Katibu mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Neno la Mungu, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Ho, Ghana.

Askofu mteule alizaliwa kunako tarehe 14 Juni 1957, Jimbo Katoliki la Keta-Akatsi. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, akaweka nadhiri za daima kunako mwaka 1984 na hatimaye, kupadrishwa hapo tarehe 14 Julai 1985, Jimbo kuu la Accra, Ghana. Tangu wakati huo, amekuwa Paroko msaidizi nchini Togo. Kunako mwaka 1190 hadi mwaka 1994 akapelekwa masomoni, kwenye Taasisi ya Biblia, Roma. Kati ya Mwaka 1994 hadi mwaka 1996 akafundisha Seminari kati ya Togo na Ghana.

Kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2000 alitekeleza utume wake kwenye Makao makuu ya Shirika mjini Roma. Mwaka 2000 hadi 2004 akateuliwa kuwa Gombera wa Chuo cha Shirika mjini Roma; Jaalim na mlezi Seminari kuu ya Mt. Victor, Tamale. Mwaka 2001 hadi 2003 alikuwa pia Katibu mkuu na mratibu wa Kanda ya SVD Afrika na Madagascar. Mwaka 2004 hadi mwaka 2006 akateuliwa kuwa Mratibu wa Kanda ya AFRAM, yenye makao yake makuu mjini Accra, Ghana. Tangu mwaka 2006 akachaguliwa kuwa Katibu mkuu wa Shirika na baadaye akachaguliwa tena kuendelea na utume huu kunako mwaka 2012.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.