2015-07-14 14:33:00

Hija ya kitume ya Papa Francisko Amerika ya Kusini imewasha moto wa matumaini


Rais Sergio Mattarella wa Italia, kwa niaba ya wananchi wa Italia, amemwandikia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa shukrani na matashi mema pamoja na kumkaribisha tena nyumbani baada ya kutembelea Amerika ya Kusini. Ni matumaini ya Rais Mattarella kwamba, ujumbe wa matumaini na changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume huko Amerika ya Kusini, itakuwa imegusa nyoyo za watu wengi waliompokea kwa moyo wa furaha na shukrani.

Ni matumaini ya Rais Mattarella kwamba, wananchi wa Equador, Bolivia na Paraguay; mataifa ambayo Italia inayaangalia kwa moyo wa shukrani na matarajio; yataweza kuhamasishwa kwa maneno na changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume huko Amerika ya Kusini. Huu ni mwaliko wa imani na changamoto ya kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi, tayari kuanzisha mchakato wa majadiliano na ushirikiano wa kikanda kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.