2015-07-13 10:25:00

Vijana mwambateni Yesu, ili kupeperusha bendera ya ushindi!


Baba Mtakatifu Francisko Jumapili jioni, tarehe 12 Julai 2015 alihitimisha hija yake ya kitume nchini Paraguay na Amerika ya Kusini katika ujumla wake, kwa kukutana na kuzungumza na “bahari ya vijana” waliokuwa wamekusanyika katika eneo la Costanera, ambao wamechangamotishwa na Mama Kanisa kufurahi katika Bwana maana tuzo lao ni kubwa mbinguni. Baba Mtakatifu amepata fursa ya kusikiliza kwa makini shuhuda zilizotolewa na vijana na kuwataka vijana kujikita katika mambo makuu mawili: urafiki pamoja na mafungo ya maisha ya kiroho.

Mtakatifu Inyasi wa Loyola katika moja ya tafakari zake anasema kwamba, kuna bendera mbili ambazo zinatawala katika maisha ya mwanadamu, bendera ya kwanza ni ile ya Shetani na dendera ya pili ni ile inayopeperushwa na Kristo. Hapa mwamini kwa kutumia vyema utashi wake anaweza kuamua ni mahali gani anaweza kushabikia; kucheza maisha na Shetani kwa kuahidiwa kupata utajiri wa chapu chapu, sifa na heshima; utukufu na madaraka na hapa mtu anajipatia umaarufu na kuabudiwa na wengi hata kama hastahili.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba aliyokuwa ameandaa kwa ajili ya kukutana na vijana anaendelea kukaza, bendera ya ushindi inayopeperushwa na Yesu, haina makuu, bali inajikita katika upendo na huduma makini kwa jirani na kwamba, hapa waamini wanapewa changamoto kubwa na Yesu Kristo, kwani hapa hakuna cha mzaha.

Katika Maandiko Matakatifu, Shetani anasimuliwa kuwa ni “baba wa ubaya” ambaye amewadanganya wengi na kuthamini kwamba, kwa kuambata naye wangeweza kupata furaha ya kweli katika maisha, lakini ukweli wa mambo ni kwamba, wamejisikia watupu pasi na hata na chembe ya furaha moyoni. Shetani ni mzushi anayewaahidia watu matumaini ambayo kamwe hayatawasaidia kupata furaha ya kweli moyoni na huu ndio mkakati na mchezo wake mchafu anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Shetani anataka kuwagawa watu, kwa kutengeneza mazingira ya kinzani na migogoro, magomvi na vita. Ili kufanikisha azma hii, Shetani anawagonganisha na marafiki zao, kiasi hata cha kutosikilizana wala kusaidiana tena, kwani yote yalikuwa yanajikita katika mwonekano wa nje, yaani thamani ya mtu inaonekana kwa vitu anavyomiliki katika maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, upande wa Yesu hakuna ahadi ya kupata makubwa na wala hakuna furaha ya kweli inayoweza kupataikana katika utajiri wa chapu chapu; madaraka na kiburi. Badala yake, Yesu anawahidia wafuasi wake heri za Mlimani ambazo kimsingi ni mafundisho makuu ya Yesu, akiwataka kuwa maskini wa roho; kuwa na njaa na kiu ya haki; kuwa na huruma na moyo safi; pamoja na kujikita katika ujenzi wa misingi ya amani na kwamba, wana heri wale wote wanaodhulumiwa kwa sababu ya haki. Yesu anawaonesha wafuasi wake njia, ukweli na maisha, kama kielelezo makini cha mfumo wa maisha yake yanayojenga urafiki na muungano na Baba yake wa mbinguni.

Kwa njia hii waamini wanaopeperusha bendera ya Yesu wanajisikia kuwa kweli ni watoto wapendwa wa Mungu. Furaha ya kweli anasema Baba Mtakatifu inajikita katika uvumilivu; kwa kuheshimu na kuwathamini wengine; kwa kutohukumu wala kulaani wengine. Watakuwa na furaha ya kweli wale ambao wanathubu kuuvua utu wa kale na kujivika utu mpya; kwa kutumia kwa umakini mkubwa fursa mbali mbali zinazopatikana katika maisha; kwa kuwasaidia na kuwaokoa wengine kutoka katika shida na mahangaiko yao. Watakuwa na heri na furha kuu wale wanaoshikamana bila kuwatenga jirani zao.

Baba Mtakatifu anasema, Mtumishi wa Mungu Chikitunga kutoka Paraguay anaonesha ule utimilifu wa heri za mlimani; kuwa ni jambo ambalo linawezekana kabisa na kwamba, linaujaza moyo wa binadamu furaha na urafiki wa kweli mintarafu mtindo wa maisha ya Yesu. Huu ni mwaliko na changamoto ya kutoka katika ubinafsi, tayari “kujirusha” uwanjani ilikufahamiana na marafiki wapya, tayari kuwashirikisha urafiki unaomwambata Yesu, katika medani mbali mbali za maisha na hata katika mitandao ya kijamii; wakati wa kuserebuka au kujipatia moja baridi, moja moto!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.