2015-07-13 09:38:00

Upendo na ukarimu ni utambulisho wa Mkristo!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 12 Julai 2015 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Uwanja mkuu wa De Nù Guazu. Baba Mtakatifu ametumia Altare maalum iliyotengenezwa kwa mahindi, kama kielelezo cha Familia ya Mungu kuenzi utunzaji bora wa mazingira kama nyumba ya wote sanjari na mshikamano miongoni mwa watu kwani hii ni kazi kubwa ambayo imefanywa kwa njia ya ushirikiano. Baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa mahindi yote yatagawa kwa maskini na wahitaji zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake katika Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa waamini kutoka ndani na nje ya Paraguay, amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa imani inayochipuka kutokana na ushuhuda wa imani tendaji uliooneshwa na wafuasi mbali mbali wa Kristo walioacha chapa ya kudumu, kiasi kwamba, leo hii wamekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa katika kumwilisha imani na urafiki.

Baba Mtakatifu anasema, Marko katika Injili ya Jumapili ya 15 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa anatoa dira na utambulisho wa Mkristo, unaomtaka kuwa mwepesi na wala wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala fedha za kibindoni na kukaa katika nyumba watakayowakaribisha kwa ukarimu. Baba Mtakatifu anasema, ukarimu ni utambulisho wa mfuasi wa Kristo. Wakristo wamejifunza kuwapokea na kuwakirimia wengine.

Yesu anawatuma wawili wawili si kama watu wenye nguvu, wamiliki wa mali, wakuu wa watu wakiwa na sheria na kanuni za kutekelezwa. Anawaonesha kwamba, safari ya Mkristo ni kusaidia kuongoa mioyo na roho za watu. Anawataka wajifunze kuishi katika ulimwengu mwingine kwa kuambata sheria mpya. Huu ni mwaliko wa kutoka katika kongwa la ubinafsi, hali ya kujifungia katika upweke; kinzani na migawanyiko; hali ya kujisikia kuwa bora kuliko wengine na kuanza kuambata mantiki ya maisha inayojikita katika sadaka na majitoleo; upendo na kiasi; kwa kuwapokea, kuwakarimu na kuwahudumia wengine.

Hapa Yesu anaonesha uwili unaofumbatwa katika safari ya mwanadamu yaani: maisha na utume. Anakaza kusema, mara nyingi Wakristo wamejikuta wakitoa kipaumbele cha pekee katika utume kwa kuangalia miradi inayopaswa kutekelezwa na harakati katika mchakato wa Uinjilishaji unaopania kuwaongoa watu wengi zaidi. Lakini jambo la msingi kutambua kwamba, Kanisa ni nyumba ya ukarimu, kwa wenye njaa, wenye kiu, wageni, walio uchi, wagonjwa na wafungwa.

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa ni nyumba ya wagonjwa wa ukoma, vilema; ni mahali panapotoa hifadhi hata kwa wale wenye mawazo yanayokinzana na yako; kwa wale wenye imani tofauti au iliyopotea; ni nyumba kwa wote wanaoteseka na kudhulumiwa; kwa watu wasiokuwa na fursa za ajira. Kanisa ni nyumba inayohifadhi tamaduni za watu mbali mbali, kiasi cha kulifanya kuwa na utajiri mkubwa; ni nyumba inayotoa hifadhi hata kwa wadhambi, kwani hakuna hata mtu mmoja anayeweza kutengwa na upendo wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, upweke hasi ni kati ya majanga ambayo yanaendelea kumwandama mwanadamu katika hija ya maisha yake. Huu ni upweke unaoweza kusababishwa na mambo mengi kiasi cha watu kujitenga na Mwenyezi Mungu, jirani na jumuiya katika ujumla wake. Kutokana na mwelekeo huu wa maisha, Yesu anaonesha mantiki na mwelekeo mpya kwa Mungu anayeguswa na maisha pamoja na mahangaiko ya watu. Huu ndio mwelekeo na Neno katika kukabiliana na hali mbali mbali zinazomwandama mwanadamu kwa kuwatenga wengine, kwa kujifungia katika upweke na kujitenga na wengine. Hili ni Neno linavunjilia mbali ukimya na upweke.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.