2015-07-13 08:28:00

Papa : inawezekana kuwa na dunia yenye ubinadamu


Baba Mtakatifu Francisco Jumamosi 11 Julai majira ya saa kumi za Paraguay, alikutana na kuhutubia  wawakilishi wa vyama vya kijamii waliokuwa wamekusanyika kumsikiliza  katika uwanja wa Leon  Condou Asuncion, wakiwemo wasomi, walimu , wasanii , wafanya biashara, mameya , wanamichezo wanahabari, vyama vya wanawake , wakulima na watu mahalia.

Katika hotuba yake alisisitiza kwamba, inawezekana kuwa na dunia yenye ubinadamu zaidi, iwapo kila binadamu atazingatia utendaji wa haki.  Kila mmoja kukataa  dhulma , dharau na unyanyasaji kwa wengine hasa watu maskini na wanyonge wasiokuwa na nguvu za kujitetea.  Papa aliendelea ili hili liwezekane, watu wote wanapaswa kujenga moyo wa upendo kwa wengine , kuwapenda kama ndugu bila ya kuwatoa kama sadaka  ya kuteketezwa  katika madhabahu za fedha  na faida  binafsi .

Mkutano huu ulifunguliwa na burudisho la muziki wa ala wa vijana , ikifuatia na ushuhuda wa watu kadhaa waliowakilisha makundi mbalimbali kama wakulima , wenyeji,wafanya biashara Wakristo na vyama katoliki . Karibu shuhuda za wote katika ushuhuda wao ulizungumzia ,  matatizo na mapambano  na matumaini katika mchakato wa kuwa na  jamii bora, Paraguay.

 Papa Francisco alishukuru  ushahidi wao wa nguvu, kwa sababu  uliwakilisha mawazo ya watu wa Paraguay , na akasema,  jamii inayoishi katika hali ya ukimya tu wa kuwa watazamaji ni jamii iliyokufa. Mungu daima husaidia wale wanaojibidisha. Huwawezesha kuvishinda vikwazo vingi vinavyorudisha nyuma maendeleo yao kiroho na kihali. .

Papa aliendelea kueleza jinsi ilivyo muhimu kwa vijana  kupata ufahamu juuya  furaha ya kweli, kupitia njia za kuwa washupavu katika kutetea haki na ukweli kwa ajili ya kuwa na dunia yenye mshikamano na udugu zaidi.  Na kwamba, kuwa na  furaha na maridhiano si kukaa kivivu, kwa sababu "furaha thabiti  inahitaji kutenda kwa furaha kwa kujitolea na kujituma. Papa ameutaja kuwa  huo wito mkuu kimaadili unaomsukumu mtu kujibidisha katika kazi na maisha, na  si kuishi maisha kama mtu aliyepigwa ganzi . Papa  Francisko, aliwataka vijana wote kuwa msitari wa mbele katika shughuli za maendeleo, zinazolenga kuboresha maisha yao  na maisha ya wazazi wao na jamaa zao. Aliongeza inasikitisha kumwona kijana anaishi kama mstaafu.

Na aliwaasa kwamba, lika la ujana ni lika na kazi, lika la kuzikataa hali zote za unyonge zenye kuzorotesha maisha.  Ni lika la kupambana na umaskini  si kwa kufanya vita lakini kwa utendaji uadilifu, usikivu, unyenyekevu na haki . Na kwamba katika matatizo yao yote , mwenye kuwapa msaada wa kweli ni Yesu Peke yake. Na msaada huo hupatikana kupitia mazoea ya kusali, daima kutegemea  nguvu ya sala na kuishi na Yesu, kwa sababu Mungu ni "dhamana ya utu wetu kama binadamu."

Papa aliwataka kuliishi neno la  injili , kwa kuwa ni  chanzo cha uhai na roho ya jamii isiyokuwa na njaa au ukosefu wa ajira au ujinga au uonevu. Uzoefu wa kihistoria unatufundisha kwamba jamii yenye  ubinadamu zaidi inawezekana hata leo.  Mahali palipo na upendo kwa mwanadamu, na utayari wa kutumikia,  kuna uwezekano wa kujenga  mazingira yanayoweza kumwezesha  kila mtu kupata mahitaji yake muhimu  na hakuna mtu anayetengwa.

Upendo kwa maskini - Papa alihitimisha, ni ushuhuda  mwingine kwamba maendeleo endelevu yanawezekana kwa wote.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.